.jpg)
Nahodha wa Simba Nico Nyagawa amesema kuwa hivi sasa wanajifua kwa nguvu zaidi ili kujiimarisha na kwenda kuliwakilisha vyema taifa katika mechi yao ya ugenini ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itakayochezwa mjini Lubumbashi mwishoni mwa wiki hii.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Nyagawa alisema kuwa lengo lao ni kwenda kupata matokeo mazuri katika mechi dhidi ya mabingwa mara mbili mfululizo wa ligi ya klabu bingwa Afrika.
Nyagawa alisema kuwa wamejiandaa kuwashangaza wote wanaoipa Simba nafasi finyu ya kusonga mbele dhidi ya Mazembe, vigogo wa Afrika ambao mwanzoni mwa mwaka huu waliandika rekodi kwa kuwa timu ya kwanza barani kufika fainali ya Kombe la FIFA la Dunia la Klabu ambapo walivaana na mabingwa wa Ulaya, klabu ya Inter Milan ya Italia.
"Tuko sawa na tunaendelea na mazoezi, kocha ameandaa programu mbalimbali za kutuongezea makali, mazoezi ni magumu lakini tunapambana nayo kwa sababu tunajua kuwa tuna mechi ngumu mbele yetu," alisema Nyagawa.
Aliongeza kuwa hali ya hewa ya jiji la Arusha inawasaidia kutochoka mapema mazoezini na hivyo kutekeleza ipasavyo maelekezo yote wanayopewa na kocha.
Alisema kuwa kila mchezaji amepania kuifikisha Simba mbali katika michuano hiyo kwani wanaamini kuwa hiyo ni njia mojawapo ya kupata timu za kuchezea nje ya nchi.
"Ushindi wa mechi yetu iliyopita ya ligi pia umesaidia kutuimarisha na kila mmoja yuko vizuri kiakili, sasa tunaiwaza mechi hiyo kubwa ambayo itatuweka katika ramani ya soka endapo tutafanya kile tunachokitarajia," aliongeza Nyagawa.
Kocha Patrick Phiri alisema kuwa timu yake iko katika hali nzuri na wanaamini kuwa mazoezi wanayoyafanya yatawaimarisha na hatimaye kwenda kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Phiri alisema kuwa kiungo Hillary Echessa aliyekuwa majeruhi, tayari ameanza mazoezi na akiendelea vyema atakuwepo katika mipango yake ya kuivaa TP Mazembe Jumapili. Simba ambayo imefanikiwa kusonga mbele katika mashindano hayo makubwa katika ngazi ya klabu barani Afrika baada ya kuifunga Elan de Mitsoudje ya Comoro mabao 4-2 imeweka kambi jijini Arusha ambako ilikwenda kucheza mechi ya ligi kuu dhidi ya wenyeji AFC.
Kikianzia safari yake jijini Arusha, kikosi cha wachezaji 20 kitaondoka nchini mwishoni mwa wiki hii kuelekea Kongo.
Simba na Mazembe watarudiana Aprili 3 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wakati huohuo, Woinde Shizza anaripoti kutoka Arusha kuwa Kocha Msaidizi wa Simba, Amri Said ‘Stam’ alisema kuwa uwanja ‘mbovu’ wanaoutumia kufanyia mazoezi jijini humo ni mzuri sana kwao kwani wanaamini kuwa hawataathirika sana kama watakutana na hali kama hiyo nchini Kongo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake