ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 23, 2011

Wazanzibari waliorejea kutoka Loliondo watoa ushuhuda wao

Kundi la kwanza la watu waliopata tiba ya maajabu katika kijiji cha Samunge Luliondo ambao walitoka Zanzibar wamerejea visiwani huku wakidai afya zao zimeimarika vizuri tangu kunya kikombe cha dawa hiyo.
Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti katika mitaa ya Mbweni, Chukwani, Kiembesamaki na Kikwajuni mjini Zanzibar, walisema matatizo yaliyokuwa yakiwasumbua wanahisi yameondoka kutokana na mabadiliko makubwa ya afya yanayojitokeza katika miili yao tangu kupata dawa hiyo.
“Mwanangu alikuwa akisumbuliwa sana na matatizo ya moyo na sukari, lakini tangu kurejea Zanzibar kutoka Loliondo, amepata nafuu kubwa na anaendelea kucheza kama kawaida,” alisema Rukia Mohammed, mkazi wa Kikwajuni mjini Unguja.

Hata hivyo, alisema pamoja na dawa hiyo kutolewa kwa bei rahisi, gharama za usafiri ni kubwa hadi kufika kijijini hapo kupata tiba kutoka kwa Mchungaji mstaafu, Ambilikile Mwasapile.
Naye mama mmoja ambaye alijitambulisha kuwa ni mwathirika wa Ukimwi, na kuomba jina lake lihifadhiwe, mkazi wa Kiembesamaki alisema kwa muda mrefu alikuwa akitumia vidonge vya kurefusha maisha (ARV's).
Alisema baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa tiba hiyo katika Kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro, aliamua kufuata tiba hiyo.
“Tangu nirejee nimepata matumaini mapya, afya yangu imeimarika, kabla ya kwenda huko, nilikuwa muda mwingi nimelala na hata kula yangu ilikuwa ya matatizo, lakini sasa najisikia sijambo,” alisema.
“Kesho natarajia kumsafirisha baba kuelekea Loliondo kwa muda mrefu amekuwa ndani akisumbuliwa na maradhi ya baridi. Nimepata matumaini baada ya watu waliokwenda huko na kupata tiba kueleza afya zao zimeimarika vizuri,” alisema.
Hata hivyo, wakizungumzia dawa hiyo, baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Zanzibar walisema wanashangazwa na serikali hadi sasa kutoa taarifa ya wazi juu ya uwezo wa kutibu wa dawa hiyo au la hasa kwa maradhi ya Ukimwi.
Abrahaman Hassan, mkazi wa Mkunazini, alisema ni jambo la kushangaza mashirika ya kimataifa kama lile la Afya Duniani (WHO), hayatajoa taarifa yoyote kuhusiana na uwezo wa dawa inayotolewa na mchungaji huyo.
Kwa upande wake, Mwajuma Ramadhan, mkazi wa Jang’ombe, alisema wakati umefika kwa Wizara ya Afya kufuatilia kwa karibu uhakika wa dawa hiyo na kuifanyia vipimo vya kitaalamu ili wananchi wawe na uhakika na matumizi yake.
CHANZO: NIPASHE

No comments: