Wednesday, May 25, 2011

TIBA YA BABU SAMUNGE:Mwingine adai kupona Ukimwi

Abdallah Ally (38) anayedai alikuwa akiugua ugonjwa wa Ukimwi lakini sasa amepona baada ya kupata dawa kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapila, akisaidia kugawa vikombe dawa hiyo kwa wagonjwa wengine katika kijiji cha Samunge, Loliondo, mkoani arusha jana. Picha na Mussa Juma
Mussa Juma, Samunge
MKAZI wa Kijiji cha Galapo, Babati, mkoani Manyara, Abdalah Ally (38), aliyekuwa mgonjwa wa Ukimwi, amedai kupona ugonjwa huo na kinga zake za mwili (CD4) kuongezeka baada ya kunywa dawa ya Mchungaji, Ambilikile Mwasapila.Ally anakuwa mtu wa pili kujitangaza kupona Ukimwi baada ya kunywa kikombe cha dawa hiyo, baada ya Wilia John Lengume wa Samunge aliyekuwa wa kwanza kutangaza kupona ugonjwa huo baada ya kupata dawa hiyo.


Akizungumza jana kijijini hapa, Ally alisema kwamba amekuwa akitumia Dawa za Kupunguza Makali ya Ukimwi (ARV), tangu mwaka 2009 kabla ya kupata kikombe cha Babu, Januari 5, mwaka huu.

Akiwa na vyeti vya vilivyoonyesha kwamba alikuwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), Ally alisema kuwa Aprili 22, 2009 alipimwa na kukutwa na maambukizi hayo wakati huo akiwa mfungwa katika Gereza la Babati.

Alisema alipima afya yake Februari 25, mwaka huu wilayani Babati na katikia Kituo cha Msalaba Mwekundu na kukutwa hana tena VVU. Alipima tena katika Hospitali ya Wilaya ya Babati ambako pia alikutwa kinga yake ya mwili ni ya kutosha na hana tena VVU ndipo alipoamua kuacha kutumia ARV.

Alidai kwamba hata baadhi ya maofisa wa afya waliokuwa wakisimamia matibabu yake wilayani Babati walishangazwa na kupona kwake kwa tiba ya Mchungaji Mwasapila na hilo liliwafanya nao kufunga safari kuja Samunge Aprili 28, mwaka huu kupata kikombe.

"Ninavyo vyeti vinavyothibitisha kuwa sina tena Ukimwi na mwezi huu pia natarajia kupima kuona afya yangu ipo vipi," alisema Ally.
Alisema kuwa kabla ya kufungwa, alikuwa dereva wa magari makubwa huku akidokeza kwamba kilichosababisha kifungo chake kilichoanza Machi 9, 2009, ni kesi ya kukutwa na pombe haramu ya gongo nyumbani kwake ambayo ilikutwa na polisi Machi 15, 2003 ambayo alidai kuwa iliwekwa nyumbani kwake na mkewe.

"Baada ya kukamatwa, kesi ilifikishwa mahakamani na baadaye faili lilipotea hivyo nikaacha kuhudhuria kesi. Lakini baadaye hukumu ilikuja kutolewa nikiwa sipo mahakamani, ndipo nikaja kukamatwa na kufungwa miezi tisa," alisema Ally.

Alisema akiwa gerezani ndipo alipopimwa na kukutwa na VVU na Julai 7, 2009, alianza kutumia dawa huku vyeti vyake vikionyesha majina ya dawa alizokuwa akitumia na tarehe alizohudhuria kliniki ya watu walio na VVU, Babati.
"Nikiwa uraiani nilianza kupata taarifa za kuwepo kwa tiba hapa Samunge, ndipo nilipojikusanya na kuamua kuja. Baada ya kupata kikombe nilirejea Babati," alisema Ally na kuongeza kuwa ameamua kurejea tena Samunge ili kumsaidia Mchungaji Mwasapila kazi ya kugawa vikombe ikiwa ni ishara ya shukrani kwake.

Maofisa afya kumchunguza zaidi
Baada ya kujitangaza kupona maradhi hayo, maofisa afya wa Zahanati ya Samunge wameahidi kumfanyia Ally uchunguzi wa kina kuthibitisha ukweli wa madai yake.Akizungumza jana kijijini hapa, Mganga wa Zahanati hiyo, Elias Lubida alisema watafuatilia ili kupata taarifa za afya yake za awali na sasa.

"Kuna ambao wanatoa ushuhuda kama huu lakini, kikubwa ni lazima ufanyike uchunguzi wa kuridhisha wa afya zao na taarifa kamili za walipopima na matokeo na matokeo ya sasa," alisema Dk Lubida.
 Taarifa za mgonjwa huyu, zimekuja wakati bado taasisi mbalimbali za afya zikiongozwa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) na Taasisi ya Utafiti wa Tiba Magonjwa ya Binadamu (NIMR) zikiendelea kuchunguza tiba ya Mchungaji Mwasapila.

Hata hivyo, baadhi ya wagonjwa wa VVU walioripotiwa kunywa dawa ya mchungaji huyo wamefariki dunia na wengine afya zao zimeimarika jambo linaloongeza changamoto kwa wataalamu sekta ya afya katika utafiti zaidi wa tiba hiyo.
Mchungaji Mwasapila amekuwa akisisitiza kuwa dawa hiyo aliyodai kuoteshwa na Mungu ina uwezo wa kutibu magonjwa sugu ukiwapo Ukimwi ingawa amekuwa akiwashauri wenye Ukimwi kuendelea kutumia ARV baada ya kunywa dawa yake.

Mamia waendelea kufurika Samunge
Mamia ya watu wameendelea kufika na kupata kikombe cha tiba hapa Samunge, wakiwamo raia kutoka Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya.

Watu hao, akiwamo mwanasiasa mashuhuri wa Kenya, Daniel Ole Muya aliyetua Samunge kwa helikopta jana, walipata tiba na kuondoka. Hadi jana mchana, magari mengi yalikuwa yameondoka Samunge.

Kutokana na foleni kupungua nyakati za mchana, Msaidizi wa Mchungaji Mwasapila, Frederick Nisajile ametoa wito kwa wenye magari kufika Samunge mchana badala ya usiku kama ambavyo wamekuwa wakifanya.

"Wakifika mchana wanapata dawa na kuondoka mapema. Lakini usiku, inawalazimu kulala hapa bila sababu ya msingi," alisema Nisajile.

Waliofariki Samunge wafikia 98
Watu wengine sita wamefariki hapa Samunge kati ya Mei 16 hadi 21, mwaka huu kabla ya kupata tiba ya Babu. Miongoni mwao ni raia wanne wa Kenya.
Dk Lubida aliwataja waliofariki kutoka Tanzania kuwa ni pamoja na Suzan Masunga (5) mkazi wa Shinyanga na Edneki Mollel (20) mkazi wa Wilaya ya Arumeru, Arusha.
Wakenya waliofariki ni Joyce Wambvoi (45) mkazi wa Naivasha, Sara Chepkoich (76) mkazi wa Bomet, Pauli Kiruwi (61) mkazi wa Molo na Stivin Kamao (52) mkazi wa Mwariga.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake