.jpg)
Wachezaji Mussa Hassan Mgosi, Hilary Echessa na Athuman Idd 'Chuji' jana walianza mazoezi na kikosi cha Simba kinachojiandaa kuikabili Wydad Casablanca ya Morocco katika mechi yao ya raundi ya tatu ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, baada ya kukosa mazoezi ya siku ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.
Taarifa Kocha wa vijana wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni, aliiambia NIPASHE jana kuwa mshambuliaji Mbwana Samatta, ambaye ameuzwa kwa klabu ya TP Mazembe, hakuwepo mazoezini jana kwa sababu anasumbuliwa na ugonjwa wa malaria. Hata hivyo, Makamu mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alikaririwa redioni jana, akisema kuwa Samatta yuko na timu yake mpya ya Mazembe mjini Lubumbashi na Emmanuel Okwi yuPo Afrika Kusini alikokwenda kufanya majaribio katika klabu ya Kaizer Chiefs ya huko.
Chuji aliyetua Simba hivi karibuni akitokea kwa mahasimu wao Yanga, alijumuika na Echessa aliyetangazwa kutemwa baada ya mkataba wake kumalizika; pamoja na Mgosi, ambaye alikaririwa akisema kuwa hatarejea hadi kwa barua baada ya kuwa amesimamishwa na uongozi kwa utovu wa nidhamu, katika siku ya pili ya mazoezi jana.
Chini ya kocha mpya wa Simba, Moses Basena kutoka Uganda, nyota hao pia walijumuika na nyota waliokuwepo kwenye mazoezi ya kwanza juzi kama Abdulhalim Humoud, ambaye ameuzwa kwa Azam FC na Patrick Ochan aliyeuzwa kwa TP Mazembe.
Kocha mpya wa Simba, Moses Basena, alisema kuwa kikosi chake kitakuwa tayari kuwakabili Wydad katika mechi yao ya raundi ya tatu ya ligi ya klabu bingwa baada ya wiki moja.
Akizungumza na NIPASHE jana, Basena alisema kuwa baada ya kukutana na wachezaji wake kwa mara ya kwanza juzi jioni, amegundua kwamba wengi wao walikuwa tayari na mazoezi magumu kwa sababu hawakuwa wamepumzika kama ambavyo walitarajiwa baada ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kumalizika mwezi uliopita.
Basena alisema kuwa amefurahishwa na hali waliyokuwa nayo wachezaji wake kwenye mazoezi mepesi ya kwanza ambapo ameona dalili za kukamilishwa kwa programu yake fupi yatatimia.
"Wamenivutia, ni siku ya kwanza ya mazoezi lakini hawaonyeshi kama walikuwa nyumbani. Wote walikuwa tayari kwa mazoezi na walifanya yale niliyowaambia," alisema kocha huyo ambaye alijiunga Simba hivi karibuni na Jumamosi kuacha rasmi kazi ya kuwa kocha msaidizi wa kikosi cha timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’.
Alisema kuwa baada ya mazoezi ya siku tatu, timu yake itaingia kambini na angependa wapate mechi moja ya kujipima nguvu kabla ya kwenda kuwavaa Wydad kwenye uwanja huru utakaotangazwa baadaye na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).
Alisema kuwa anaamini programu yake ya dharura ikikamilika, wachezaji wake watakuwa tayari kuwavaa wapinzani wao na kusonga mbele katika michuano ya ligi ya klabu bingwa.
Katika mazoezi ya kwanza yaliyosimamiwa na kocha huyo, wachezaji 18 walihudhuria, wawili wakiwa wapya na walianza kwa kufahamiana na baadaye kwenda kufanya mazoezi ya darasani na kumalizia mazoezi ya uwanjani ambayo yalichukua zaidi ya dakika 30.
Mechi ya Simba dhidi ya Wydad itachezwa kati ya Mei 27 na 29 na mshindi atatinga 8 bora na kuwa kundi moja na vigogo Al Ahly ya Misri, Mc Alger ya Algeria na Esperance ya Tunisia.
Simba walipata nafasi ya kucheza raundi ya tatu dhidi ya Wydad baada ya rufaa yao dhidi ya Mazembe waliostahili kucheza hatua hiyo kuondolewa na CAF baada ya kubainika kuwa walimtumia mchezaji Janvier Besala Bokungu kutoka Esperance bila kukamilisha taratibu za uhamisho.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment