ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 21, 2011

Mitambo ya Dowans yanunuliwa

Afisa mtendaji Mkuu wa kampuni ya Kimarekani ya kuzalisha umeme Symbion Power, Paul Hinlks (Kushoto) akizungumza kwenye mkutano na waandishi habari jijini Dar es Salaam jana.
Kampuni ya Marekani ya kufua umeme, Symbion Power LLC, imetangaza rasmi  kuwa imetia saini kununua mitambo ya DOWANS.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana mchana, Mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Paul Hinks alisema, wataalamu wa kampuni hiyo, wamethibitisha kuwa mitambo hiyo yenye uwezo wa kutoa megawati 120, iko katika hali nzuri kabisa na wanapandekeza kwa Tanesco ili mitambo hiyo iweze kutumika hapa nchini na hivyo angalau kupunguza tatizo la umeme linaloikabili nchi kwa sasa.

“Tunauwezo wa kuitumia mitambo hii popote pale Duniani, lakini tunakusudia kupendekeza kwa Tanesco waridhie mitambo hii itumike hapa nchini” alisema Hinks.
Alisema, ili kuhakikisha kuwa hakuna tatizo lolote linaloweza kutokea baada ya mitambo hiyo kuanza kazi, kampuni yake itashirikiana na kampuni ya kimataifa ya Kimarekani ya ProEnergy Services (PES) ambayo inauwezo na uzoefu mkubwa katika sekta ya umeme.
“PES inajishughulisha na uzalishaji umeme sehemu mbalimbali duniani itakuwa mbia wa kutoa huduma ya uhandisi na uendeshaji wa mitambo” alisema.
Alisema, Symbion Power inao uzoefu mkubwa katika miradi ya umeme ambayo inafadhiliwa na serikali ya Marekani kama vile yale ya Millenium challenge corporation (MCC)
“Lakini pia kampuni yetu inajishughulisha na usambazaji umeme vijijini hapa Tanzania inayojumuisha takriban kilometa 3,000 ya miundombinu ya kusambaza umeme” aliongeza.
Alisema, mzungumzo baina ya DOWANS na kampuni yake, yalikuwa magumu sana ukizingatia historia ya mradi wenyewe na kwa sababu hiyo “ilibidi kufanya uchunguzi wa kina ili kujirisdhisha na kila kipengele cha makubaliano na pia ubora wa mitambo na tumejiridhisha kuwa mitambo hii iko katika hali nzuri.”alisisitiza.
Naye mwenyekiti wa Symbion kanda ya Afrika, balozi mstaafu wa Marekani katika nchi mbalimbali, Joe Wiliams, alisema mitambo iliyonunuliwa na kampuni yake imekaa bila kutumika takriban miaka mitatu sasa wakati nchi inakabiliwa na mgao wa umeme.
“Hii inaleta changamoto katika uchumi wa nchi, sisi tutafarijika sana ikiwa TANESCO itahitaji huduma hii kutoka kwetu tena kwa bei nafuu” alisema.
Naye Balozi wa Marekani nchini,  Alfonso Lenhardt, katika taarifa yake iliyosomwa na afisa wa ubalozi huo anayeshughulikia, biashara na uchumi  “alisema, tumefurahishwa sana na kapuni ya Kimarekani Symbion kuwekeza nchini kwa kununua 112 megawati kwani umeme ni muhimu katika kilimo, viwanda, elimu na afya.
Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilisema jana kuwa ununuzi wa mitambo ya kampuni ya Dowans haitaathiri kesi ya msingi iliyofunguliwa na kituo hicho.
Mmoja wa maofisa wa LHRC ambaye hakutaka jina lake liandikwe aliliambia NIPASHE kuwa kituo hicho kilifungua kesi kupinga serikali kutoa tuzo kwa kampuni hiyo na sio kuzuia mitambo isiuzwe.
Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) iliamuliwa na Mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa masuala ya biashara kuilipa Kampuni ya Dowans Sh. Bilioni 94 kwa kuvunja mkataba wake. Mapema mwaka huu, wanaharakati walifungua kesi Mahakama Kuu kupinga serikali kutoa tuzo kwa Dowans ili kuiwezesha kulipwa Sh. bilioni 94.

CHANZO: NIPASHE

No comments: