.jpg)
Kikosi cha timu ya Simba
Wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, Simba, leo inaelekea Visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi maalumu ya kujiandaa na mechi yake ya raundi ya tatu dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco itakayochezwa kwenye uwanja wa PetroSport Mei 28 jijini Cairo nchini Misri.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema kuwa timu hiyo ikifika Zanzibar itaendelea na programu yake maalumu iliyoandaliwa na mara watakapokuwa tayari watacheza mechi mbili za kirafiki na timu za huko.
Mtawala alisema kuwa wachezaji wao wote waliosajiliwa kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika wameripoti kambini isipokuwa mshambuliaji aliyeuzwa, Mbwana Samatta, ambaye yuko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na timu yake mpya wa TP Mazembe.
"Mipango inaendelea vyema na taratibu za kuomba viza tayari tumeshaanza ili tukamilishe safari yetu ya kuelekea Cairo kuivaa Wydad," alisema katibu huyo wa Simba.
Alisema kwamba tayari wameanza mazungumzo na timu za Zanzibar Ocean View na KMKM ili waweze kuipa Simba majaribio na wanadhani itamsaidia kocha wao mpya, Moses Basena, kuona wachezaji wake kabla ya kuelekea Cairo katika mechi hiyo ya kusaka nafasi ya kucheza hatua ya makundi.
Baada ya Simba kushinda rufaa yake dhidi ya waliokuwa mabingwa watetezi wa mashindano hayo Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ilieleza kwamba Simba na Wydad Casablanca watacheza mechi moja kwenye uwanja wa ugenini kwa timu zote, ambazo zitatakiwa kujigharamia usafiri wa kwenda na kurudi nchini kwao pamoja na malazi wakiwa nchini humo ambako mechi yao itachezwa.
Endapo dakika 90 zitamalizika na mshindi hatapatikana, timu hizo zitaenda katika hatua ya matuta ili kupata timu itakayosonga mbele kwenye michuano hiyo.
Simba ikiwa na Basena ilianza mazoezi mapema Jumatatu chini ya Mganda huyo ambaye mechi hiyo dhidi ya Wydad Casablanca ndio utakuwa mtihani wake wa kwanza ndani ya kibarua chake kipya baada ya kuachana na timu ya taifa ya Uganda, The Cranes.
Kikosi cha Simba kitakachokwenda Cairo kinatarajiwa kuondoka na ndege ya kukodisha ya serikali.
Mara ya mwisho Simba kufika hatua ya makundi kwenye mashindano hayo ilikuwa ni 2003 wakiwa chini ya kocha kutoka Kenya, James Siang'a, baada ya kuwavua ubingwa, Zamalek ya Misri.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment