.jpg)
Wakati serikali ikisisitiza kuwa itatoa kibali cha kuzika maiti za watu wanne kati ya watano waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi karika jaribio la kuvamia mgodi wa North Mara,
Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimesema kitagharimia mazishi ya marehemu hao.
Serikali itangaza jana kuwa maiti ambao ndugu zao hawatajitokeza kuzichukua katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime zilikohifadhiwa kati ya leo na kesho, basi zitazikwa na halmashauri.
Msimamo huo wa serikali ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele, wakati akizungumzia kuhusu hatua ya ndugu hao kuendelea kususa kuchukua maiti tangu walipouawa Mei 16, mwaka huu.
Henjewele alisema miili hiyo bado imehifadhiwa hospitalini hapo mpaka sasa kutokana na ndugu hao kushawishiwa kukataa kuichukua kwa madai ya kupinga kwa kitendo cha kuuawa na polisi kwa kupigwa risasi.
Henjewele, alisema endapo kutakuwa na utata ukataojitokeza wakati wa mazishi hayo, serikali itatoa kibali kingine cha kufukuliwa kwa miili hiyo.
Maiti hizo ni za Chacha Ngoka, wa kijiji cha Kewanja , Emmanuel Magige, wa kijiji cha Nyakunguru, Mwikwabe Marwa, na Chawali Bhoke wa Mugumu wilayani Serengeti.
Hata hivyo, wakati serikali ikiweka msimamo huo, Chadema kimekubali kugharimia mazishi ya miili ya watu hao.
Kwa mujibu wa chama hicho, mazishi hayo yanatarajiwa kufanyika kesho baada ya kufanyika uchunguzi utakaoshirikisha daktari maalum atakayepelekwa na chama hicho.
Miili ya watu hao itaagwa katika uwanja wa Saba Saba wa mjini Tarime.
Hata hivyo, Mwanasheria wa Chadema Mabere Marando, alisistiza kuwa miili ya marehemu hao iko salama na inaweza kukaa zaidi ya miezi sita bila kuharibika tofauti.
Akizungumza na wafiwa kwa niaba ya uongozi wa chama hicho kitaifa, Marando aliwaeleza kuwa miili ya marehemu aliitazama jana jioni baada ya kuingia mjini Tarime na kuishuhudia ikiwa salama.
"Wamekufa kisiasa kwa sababu waliuawa na askari ambao wanaongozwa na CCM, pia mgodi ule una manufaa zaidi kwa chama tawala na si wananchi," alisema Marando.
Alisema kama mgodi huo hauongozwi kisiasa zaidi iweje ndani ya mgodi kuwe na kambi ya polisi badala ya kituo cha polisi kukaa nje ya mgodi ili kila raia apate huduma za kipolisi katika kituo hicho.
"Iweje serikali tena polisi waje kushauri wafiwa kuzika,na kuwarubuni kuwa watagharimia mazishi. Ni misiba mingapi inatokea hawajawahi kuhusika. Kila siku magari barabarani yanaua kutokana na ubovu wa barabara lakini hawajawahi hata kugharimia msiba wowote. Wanawarubuni kwa kuwa kuna kitu walichokishtukia," alisema Marando.
Alisema ataanza kufuatilia taratibu za kufanyia uchunguzi miili hiyo ambapo alisema ataenda kuzungumza na Jeshi la Polisi ili wapange ni jinsi gani uchunguzi huo utafanyika na aliwashauri wafiwa kuandaa mtu mmoja mmoja ambaye ataingia kuangalia jinsi uchunguzi utakavyokuwa unafanyika.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake