Friday, May 20, 2011

Tarime hali tete, polisi wamwagwa kila kona

Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya limetangaza kuzuia maandamano, mikutano na mikusanyiko yoyote ya kisiasa kwa kipindi hiki kwa maelezo kuwa hali ya usalama wilayani Tarime si ya kuridhisha kwa sasa.
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Kamishina Msadidizi, Constantine Massawe, aliliambia NIPASHE jana asubuhi mjini Tarime kuwa hatua hiyo imechukuliwa na Jeshi hilo kuanzia juzi Mei 18 mwaka huu kutokana na vurugu zinazotokana na kuuawa kwa watu watano kwa kupigwa risasi na polisi katika mgodi wa North Mara wilayani humo.

Alisema Chama cha Mapinduzi CCM, ambacho kiliomba kufanya mkutano wa hadhara mjini Tarime juzi ambao ulipangwa kuhutubiwa na Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama ulizuiwa kutokana na sababu hizo za ki usalama.
Aidha, Kamanda huyo alisema licha ya CCM kuzuiwa kufanya mikutano wilayani Tarime pia chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema ambacho kiliomba kufanya mikutano katika mji wa Nyamongo na Tarime mjini pia kilizuiawa kufanya hivyo kwa sababu hizo.
“Hali ya usalama katika wilaya ya Tarime kwa sasa si ya kuridhisha hivyo tumezuia mikutano na maandamano yoyote ya kisiasa kwa wakati huu hadi hali itakapokuwa shwari,”alisema Masawe.
Katika hatua nyingine, Jeshi Polisi nchini limeanua kugharamia mazishi ya watu watano waliouawa na polisi katika wilaya ya Tarime kufuatia vurugu za uvamizi wa mgodi wa dhahabu huko Nyamongo wa North Mara.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Oparesheni Jeshi la Polisi nchini, Paulo Chagonja, wakati alipokuwa akizungumza na ndugu wa marehemu waliokuwa katika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya hiyo.
Chagonja aliwataka ndugu hao kuzika marehemu hao kwa kile alichodai kuwa kama ni kufa tayari watu walishakufa na hata kama wasipozikwa hawawezi kupata uhai.
Aidha, alisema kuwa serikali iko tayari kusaidia gharama za mazishi pamoja na kutoa ubani kwa ndugu wa marehemu ikiwa kama njia mojawapo ya pole.  Alisema kuwa watu hao waliuawa kwa bahati mbaya kwani haikuwa nia ya askari hao kuua na kwamba waliouawa ni wavamizi na si majambazi kama ilivyokuwa ikiripotiwa hapo awali.
 Aliwataka ndugu wa marehemu kuungana pamoja ili miili ya marehemu ifanyiwe uchunguzi na kisha ikazikwe lakini ndugu wa marehemu waligoma kwenda kufanya uchunguzi kwa kile walichodai kuwa hawana utaalamu wa kufanya uchunguzi huo.
 Hata hivyo, alisema kuwa baada ya mazishi serikali itaunda tume kutoka makao makuu itakayoshirikiana na ndugu wa marehemu ili kutafuta chanzo cha mauaji hayo,na kwamba atakae bainika kuhusika kwa namna moja ama nyingine serikali haitasita kumchukulia hatua hata kama ni kiongozi wa serikali.
 Ndugu wa marehemu hao waliendelea kusema kuwa ni jambo la ajabu serikali tena Jeshi kugharamia mazishi ya watu waliowaua kwa madai kuwa ni majambazi.
 “Jamani iweje, jambazi likazikwa na serikali? Na kama ni jambazi iweje polisi mseme mtatoa ubani? Hatuziki mpaka kieleweke ili iwe fundisho kwa Jeshi kuua watu ovyo,”walisema ndugu wa marehemu.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake