.jpg)
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela
Jalada la uchunguzi wa sakata la watu wawili waliodaiwa kufa baada ya kula egg chop katika mgahawa mmoja Mikocheni jijini Dar es salaam, tayari limekabidhiwa kwa wakili wa serikali kwa hatua zaidi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, aliliambia NIPASHE hivi karibuni kuwa, uchunguzi wa tukio hilo kwa upande wa polisi umekamilika na tayari jarada hilo limeshakabidhiwa kwa wakili wa serikali mapema wiki iliyopita.
Kenyela alisema awali, jalada hilo lilikuwa kwa Mkuu wa Upelelezi wa wilaya hiyo na baadaye ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kinondoni ambaye baada ya kukamilisha kazi yake ya upelelezi liliwasilishwa kwa wakili.
Alisema kwa sasa wanasuburi hatua zitakazochukuliwa zaidi na wakili wa serikali kama kuna kesi ya kujibu au la.
“Yeye ndiye atakayetoa maana ya kisheria iwapo watuhumiwa wanakesi ya kujibu au la kwa kuzingatia vielelezo na maelezo mbalimbali yaliyopo kwenye jalada tutakalomkabidhi wiki ijayo kuanzia Jumatatu,” alisema.
Kenyela alisema wakati jarada hilo likishughulikiwa kwenye ofisi yake tayari walikuwa wameshapokea ripoti za uchunguzi zilizokuwa zikifanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambao walikuwa wakichunguza kama egg chop hizo zilikuwa na sumu yoyote.
Pia alisema ripoti ya uchunguzi wa maiti uliofanywa na madaktari mara baada ya tukio hilo pamoja na ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali nayo walikabidhiwa.
Alisema ripoti ya Mkemia Mkuu ilitokana na sampuli zaidi ya 15 za mabaki ya chakula na miili ya marehemu zilizokabidhiwa kwao ili kuzichunguza.
Katika hutua nyingine, NIPASHE imeshuhudia duka hilo likiwa limefunguliwa na likiendelea na biashara kama kawaida.
Kwa mujibu wa Meneja wa duka hilo, Zakaria Gabriel, Aprili 3, mwaka huu TFDA iliwapatia kibali cha kuwaruhusu kuuza baadhi ya bidhaa walizokuwa wakiziuza awali.
Gabriel alisema baada ya polisi kufanya uchunguzi wao, walibaini kuwa mayai yalikuwa na bakteria aina ya Samonera ambao humfanya mtu aharishe na sio kumsababishia kifo.
“Uchunguzi wa TFDA ulibaini vifo vya watu hao havikuhusiana na vyakula vyetu hivyo walituruhusu tuendelee na biashara kwa baadhi ya bidhaa zitokanazo na ngano wakati zile za nyama ziendelee kusimama kwa kuwa uchunguzi unaendelea,” alisema.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa duka hilo, Exaud Kiwali, alisema athari wanazozipata ni pamoja na wateja wao kuwa na hofu na bidhaa zao hivyo ameomba uchunguzi unaoendelea kufanyika ukamilishwe mapema.
NIPASHE imekuwa ikipiga simu TFDA mara kwa mara kwa ajili ya kujua hatua walizofikia za uchunguzi, lakini mara zote wamekuwa wakipewa taarifa tofauti.
Tukio hilo lilitokea mwezi Februari mwaka huu baada ya watu kula egg chop hizo kwenye duka la kuuzia mikate la Royal Oven Bakery lililopo Kawe, jijini Dar es Salaam.
Waliokufa ni Kharafa Shaban na mtoto wake Faidha Shaban (4) na wengine saba walijitokeza kwa nyakati tofauti na kueleza kuwa, nao walipatwa na tatizo la kuharisha na kutapika baada ya kula chakula hicho.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment