Mussa Juma, Samunge
MAOFISA mbalimbali wa serikali za nchi za Afrika Mashariki, akiwamo Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wa Kenya, Joseph Kikwai Koshoi jana walitua Samunge kupata kikombe cha tiba, huku wakieleza maajabu ya dawa hiyo ya Mchungaji Ambilikile Mwasapila.
Koshoi aliyekuwa na polisi wa Kenya, akiambatana na familia yake alisema amefika Samunge kupata tiba baada ya kuona maajabu ya tiba hiyo kwa watu wa nchi yake wakiwamo maofisa polisi ambao alidai walikuwa mahututi na sasa wamepona.
"Na mimi ninakuja na familia kupata tiba hii kwani ni ya ajabu. Kuna wafanyakazi walikuwa mahututi, lakini baada ya tiba wamepona... Tena sasa watakuja maofisa wengi tu kutoka Kenya," alisema Koshoi ambaye ni mkazi wa Kisumu, Kenya.
Maofisa hao walitua Samunge jana na kabla ya kupata kikombe walikwenda kutambulishwa na kupeana mkono na Mchungaji Mwasapila kama ilivyo kawaida kwa watendaji wengine wa serikali wanaofika hapa.
Waliopata kikombe yafikia milioni nne
Serikali kupitia Idara ya Takwimu, jana ilifikisha Samunge Dodoso za kutambua watu wote wanaofika Samunge kupata kikombe huku, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Masai Kaskazini, Mchungaji Joel Nangole akieleza idadi ya waliopata kikombe imefikia milioni nne.
Akizungumza katika ibada iliyofanyika hapa jana, Mchungaji Nangole alisema idadi hiyo ni kubwa na hivyo kulazimu kanisa kushirikiana na serikali kuwa na utaratibu wa kutambua watu wote waliopata tiba Samunge na uraia wao.
Awali, akizungumza Meneja wa Takwimu na Mratibu wa Sensa Mkoa wa Arusha, Margaret Martin alisema amefika Samunge kuanzisha utaratibu wa kuratibu watu wote wanaopata tiba.
Martin alisema mpango huo, utawezesha serikali na wadau wengine kama Benki ya Dunia kujua idadi ya watu wanaofika Samunge kupata tiba na kuona mahitaji yao ni kiasi gani katika nyanja mbalimbali.
"Hapa kuna watu wa uhamiaji, polisi na idara nyingine. Tunataka kukusanya takwimu zote kuanzia sasa ili tujue idadi kamili kama ambavyo leo imeelezwa watu wamefikia milioni nne," alisema Martin.
Alikabidhi mfano wa madodoso hayo ya awali kwa maofisa wa serikali na pia kufanya mazungumzo na Mchungaji Mwasapila kuhusu mpango huo.
Babu awatoa hofu wajawazito
Mchungaji Mwasapila amewatoa hofu wajawazito akisema dawa yake haina madhara kwao.
Alisema dawa hiyo licha ya kutokuwa na madhara, inawasaidia kina mama wenye matatizo ya kutoshika mimba akisema baada ya kuinywa hupona na kushika mimba.
"Mkinywa dawa ondoeni hofu, kunyweni dawa itawasaidia kupona na nimepata simu nyingi kuna ambao walikuwa na matatizo ya ujauzito na wamepata mimba," alisema Mwasapila.
Vurugu za uongozi Samunge kuendelea leo
Vurugu za uongozi Samunge leo zinatarajia kuendelea baada ya Mwenyekiti aliyetimuliwa, Michael Lengume kusisitiza kuwa hatambui kuondolewa na mkutano mkuu na leo ataingia ofisini.
"Mimi ndiye Mwenyekiti na nitamwandikia barua huyo aliyedai kuteuliwa kukaimu nafasi yangu, nitamjulisha kuwa mimi bado ni mwenyekiti na serikali na halmashauri vinanitambua," alisema Lengume.
Lengume alikanusha kutafuna fedha za ushuru wa magari yanayotua Samunge kiasi cha Sh27 milioni na za ujenzi wa shule ya sekondari.
"Haya ni majungu, yanaendelezwa na viongozi walafi ili wanufaike na fedha za ushuru, mimi siyo mtunza hazina wa kijiji iweje waseme nimekula fedha?" alisema Lengume.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment