
Rais wa taasisi ya Global Football, Patrick Steenberge (kushoto) akitoa maelezo baada ya mazoezi ya mchezo wa `American football` kwa vijana wa Kitanzania mjini Arusha jana.
Timu za wachezaji wa mpira wa American Football wa Kimarekani kutoka vyuo vikuu vya Marekani na Mexico, jana zilianza kutoa mafunzo ya siku mbili ya mchezo huo kwa wanafunzi zaidi 1000 wa shule za msingi na sekondari za jijini hapa ambapo kesho watacheza mechi baina ya nchi mbili hizo.
Rais wa Global Football, Patrick Steenberge, alisema jana wakati akizungumza na wanahabari katika uwanja wa Tanzania Game Trackers kuwa mafunzo hayo ya siku mbili yanamalizika leo.
Alisema kesho kutakuwa na mechi kati ya timu ya Chuo Kikuu cha Drake cha Marekani na timu kutoka Chuo Kikuu cha Conadeip All Stars ya Mexico.
Alisema msafara mzima una jumla ya watu 195 wakiwapo maofisa wa timu, wanahabari na mashabiki na kauli mbiu yao ni ‘Tupande Kileleni.’
Alisema mshindi atapewa kikombe na mchezo huo utafanyika katika uwanja wa mpira wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa kuanzia saa 7 hadi saa 10 jioni na kwamba utarushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha ITV na televisheni ya Marekani.
Steenberge alisema mechi ya kesho itakuwa ni ya kwanza na aina yake kufanyika Afrika na Tanzania kwa namna ya pekee.
Alisema pamoja na mechi hiyo watatoa misaada kwa mradi wa watoto yatima na kusaidia kijiji cha Sokoine kilichopo mkoani Singinda kupata maji.
Wageni hao wanatarajiwa kupanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea Mbuga ya Wanyama ya Tarangire.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Bodi ya Utalii Tanzania, (TTB) Geofrey Tengeneza, alisema ujio wa ugeni huo ni matokeo ya matangazo ya TTB yanayotolewa nchini Marekani wakati wa ligi kuhamasisha utalii nchini.
Alisema ujio wa wachezaji hao utahamasisha watalii wengi kutoka nchi hizo na zingine kuja na ni matarajio ya Bodi yake kwamba baada ya muda mfupi watalii wengi watakuja nchini.
Wakati huo huo, Woinde Shizza anaripoti kuwa Jeshi la Polisi hapa Arusha limesema kuwa limeimarisha ulinzi kwa ajili ya wageni waliowasili kwa ajili ya kushiriki mchezo wa American Football utakaofanyika kesho jijini hapa.
Akiongea na waandishi wa habari mkoani hapa, kamanda wa polisi wa mkoani hapa, Thobias Andengenye, alisema kuwa ulinzi huo uko katika sehemu mbalimbali ikiwemo mahala watakapofikia wageni, watakakotembelea na kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ambapo mchezo huo utafanyika.
"Tumeweka ulinzi wa kutosha kwaajili ya ugeni huu, kwani ugeni huu ni mkubwa na ni wa kimataifa, hivyo mbali na sisi jeshi la polisi pia tunaomba ushirikiano kutoka kwa wananchi wa mkoani hapa," alisema Andengenye.
Baada ya mechi hiyo wageni hao watatembelea vituo mbali mbali vya utalii ikiwemo mbuga za wanyama kama Tarangire na kupanda Mlima Kilimanjaro.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake