ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 13, 2011

Waeritrea waomba hifadhi ya ukimbizi TZ

Wachezaji 13 wa timu ya Red Sea ya Eritrea iliyokuwa ikishiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati 'Castle Kagame Cup 2011' iliyomalizika Jumapili, wamejisalimisha wenyewe kwenye ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kuomba hifadhi ya ukimbizi nchini.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo kwa vyombo vya habari jana, imesema kuwa wachezaji hao ambao walitakiwa kuondoka nchini Julai 9 kwa ndege ya shirika la Kenya, hawakuonekana kwenye uwanja wa ndege katika siku hiyo ya safari.
Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa Idara ya Wakimbizi inaendelea kuwahoji wachezaji hao kabla ya kutoa uamuzi juu ya ombi lao.
Ilisema kuwa mahojiano hayo ni sehemu ya utaratibu unaotekelezwa kufuatana na sheria za nchi na za kimataifa kuhusu watu wanaoomba hifadhi na baada ya mahojiano hayo ambayo yalitegemewa kukamilika jana, taratibu nyingine zitafuatwa.
'Mahojiano haya ya awali yanafanywa ili kujua sababu zilizowafanya wachezaji hawa kutorejea kwao, na kujua kama sababu hizo zinaweza kuwapa sifa ya kupewa hadhi ya ukimbizi na sheria za kitaifa na kimataifa," ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Msemaji wa Wizara hiyo, Isaac Nantanga.
Taarifa hiyo ilisema kuwa hivi sasa, wachezaji hao wanahifadhiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na pasi zao za kusafiria zinashikiliwa na Idara ya Uhamiaji.
Juzi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alitangaza kuwa wachezaji 13 wa timu hiyo na viongozi wao wametoweka kusikojulikana baada ya kumalizika kwa mashindano hayo.
Kikosi cha timu hiyo kilikuja nchini kikiwa na msafara wa watu 26 na 13 kati yao wameshaondoka nchini na kurejea kwao Eritrea.
CHANZO: NIPASHE

No comments: