ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 6, 2011

Bunge kuchunguza ufisadi wa Sh200 bilioni za Meremeta

Waandishi Wetu
BUNGE, kupitia Kamati yake ya Nishati na Madini litachunguza ufisadi wa zaidi ya Sh205.9 bilioni unaodaiwa kufanywa kupitia Kampuni ya uchimbaji madini ya Meremeta iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).Kamati Ndogo ya Madini ya Bunge itafanya uchunguzi wa uhalali wa malipo ya Dola za Marekani 132 milioni (sawa na Sh205.9 bilioni kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambacho ni Sh1,560 dhidi ya Dola) ambazo zilitoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwenda Ned Bank ya Afrika Kusini ikiwa ni malipo ya mkopo wa Dola 10milioni uliokuwa umechukuliwa na Kampuni ya Meremeta Ltd.


Hatua hiyo imekuja baada ya mvutano wa muda mrefu, ulisababishwa na hoja zilizokuwa zikitolewa na Serikali kwamba suala la Meremeta lisingeweza kufanyiwa uchunguzi kutokana na “sababu za kiusalama.”

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi na kuthibitishwa Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel umebaini kwamba Spika wa Bunge, Anne Makinda ameridhia kufanywa kwa uchunguzi huo kupitia Kamati Ndogo ya Nishati na Madini ya Bunge.
Pendekezo la kuundwa kwa Kamati hiyo ndogo lilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, January Makamba wakati akitoa maoni ya Kamati yake kuhusu Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Julai 15, mwaka huu, wakilenga kuchunguza nafasi ya Kampuni ya Pan African Energy katika mchakato wa uzalishaji wa gesi ya Songosongo.

Awali, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe alikuwa amewasilisha barua kwa Katibu wa Bunge akitoa taarifa ya hoja ya kuunda Kamati Teule ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza tuhuma za ufisadi kupitia kampuni hiyo ya uchimbaji wa dhahabu ya Meremeta.
“Spika ameona kwamba ni bora suala hilo la Meremeta likafanyiwa kazi na Kamati Ndogo ya Nishati na Madini ambayo itaundwa kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake mengine,” alisema Joel simu jana.

Alisema hatua hiyo itaepusha gharama kubwa ambazo zingeweza kutumika kama Bunge lingeamua kuunda kamati teule kama Zitto alivyokuwa amependekeza.
 “Hili linafanyika kwa mujibu wa kanuni na kwa kuwa tayari kamati ilikuwa imependekeza kuundwa kwa kamati ndogo, basi Spika aliona ni vyema jukumu hili likafanyike hukohuko,” alisema Joel na kuongeza:
“Tayari nimezungumza na Mheshimiwa Zitto kuhusu uamuzi huu wa Spika lakini nitamjulisha kwa barua rasmi na pia Mwenyekiti wa Kamati naye atajulishwa maelekezo hayo ya Spika.”

Kwa upande wake, Makamba alisema kamati husika tayari imeishapendekezwa kwa Spika, lakini hakuwa tayari kuwataja wajumbe wa kamati hiyo.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba miongoni mwa wajumbe wa Kamati hiyo ndogo waliopendekezwa ni Mbunge wa Simanjiro (CCM) Christopher Ole Sendeka ambaye amejipambanua kuwa miongoni mwa wanasiasa wanaopiga vita ufisadi nchini.
“Kamati yetu ina uwezo wa kufanya kazi hizi wala sina wasiwasi hata kidogo, lakini sijapata maelekezo ya Spika hivyo siwezi kuingia kwa undani kuhusu jambo hili hadi hapo nitakapokuwa nimepata maelekezo hayo,” alisema Makamba.

Hoja ya Zitto

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) alikuwa ametoa hoja ya kutaka iundwe kamati teule ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza ufisadi huo.

Zitto alitoa taarifa ya mdomo bungeni Julai 13, mwaka huu kwa mujibu wa Kanuni ya Bunge Namba  117 (2)-(a) inayomruhusu kutoa taarifa ya kusudio lake la kuwasilisha hoja ya kutaka Bunge liunde kamati teule. Julai 15, mbunge huyo alimwandikia Spika Makinda barua kutoa taarifa ya hoja husika.
“Kuna haja ya kujua uhalali wa ongezeko la Dola milioni 122 zilizoongezeka katika malipo hayo," alisema Zitto katika barua yake kwenda kwa Spika.Alisema kitendo cha kurejesha mkopo huo pamoja na faida ya zaidi ya asilimia 1,000 kinaashiria kuwepo kwa ufisadi wa fedha za umma na ni jambo ambalo haliwezi kuvumilika lipite bila kuwekwa wazi.

 Zitto alielezea kushangazwa kwake na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi kutolifafanua suala hilo kwenye majumuisho ya bajeti yake kwa mwaka 2011/12, hivyo kusema kuwa upo umuhimu wa Bunge kuliweka wazi suala hilo kwa wananchi.

Fedha hizo zilichukuliwa kupitia kampuni ya Meremeta ambayo iliundwa na Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Afrika Kusini ya Triennex PTY, hivyo kuchukua mkopo huo wa Dola 10 milioni, lakini kiasi kilichorejeshwa baadaye ndicho kinachotia shaka.Zitto alisema katika kurejesha fedha hizo, Serikali iliamuru BoT iilipe Nedbank na ilitekeleza agizo hilo mwaka 2004.

Meremeta ilikotokea 
Suala la Meremeta ni la muda mrefu na mara nyingi Serikali imekuwa haiko tayari kulizungumzia kwa maelezo kwamba ni suala ambalo lina maslahi ya kiusalama kwa taifa.

Awali, Serikali ilisema kwamba Meremeta Ltd ni kampuni ya Kitanzania iliyokuwa ikimilikiwa na JWTZ kwa ajili ya mradi wake wa Nyumbu, Mkoa wa Pwani. Taarifa za usajili zilizotolewa na Msajili wa Makampuni wa Uingereza na Wales zinabainisha kuwa kampuni hiyo iliandikishwa nchini humo mwaka 1997 na baadaye ilifilisiwa huko huko Uingereza mwaka 2006.

Taarifa ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ya Mei 31, 2005 inabainisha kwamba Meremeta Ltd ni tawi la kampuni ya kigeni iliyosajiliwa Tanzania, Oktoba 3, 1997 na kwamba hisa 50 za kampuni hiyo zilikuwa zinamilikiwa na Kampuni ya Triennex (Pty) Ltd. ya Afrika Kusini, wakati hisa 50 zilizobaki zilikuwa zinamilikiwa na Serikali ya Tanzania.

Utata mkubwa kuhusu umiliki wa Meremeta Ltd unatokana na taarifa ya Brela ambayo pia inazitambua kampuni mbili za Kiingereza ambazo ni London Law Services Ltd na London Law Secretarial Ltd kuwa wamiliki wa hisa moja kila moja ndani ya Meremeta.
Licha ya Serikali kutokuwa mmiliki pekee wa kampuni hiyo, BoT ililipa madeni yote ya Meremeta badala ya kusaidiana na washirika wake ambao kisheria wanaonekana kuwa walikuwa wakimiliki hisa katika kampuni hiyo.

Serikali Tanzania ilikuwa ikimiliki asilimia 50 ya hisa na kwa mujibu wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), uhalali wa malipo hayo ulikuwa na walakini kwani kiutaratibu Nedbank Ltd ilitakiwa iachwe idai fedha zake kutoka kwa mfilisi wa kampuni hiyo kama ilivyo kwa wadeni wengine.

Mwananchi

No comments: