ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 13, 2011

Ngeleja sasa aja na bajeti ya 1.2 trilioni

Symbion, NSSF wapewa miradi ya kuzalisha Nchi nzima
Neville Meena, Dodoma
KAMPUNI ya Symbion Power ya Marekani na Shirika la Hifadhi ya Jamii nchini (NSSF) wamepewa zabuni ya kuingiza nchini mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura, katika mpango ambao Serikali itauwasilisha bungeni leo.
Symbion Power ni kampuni ambayo ilinunua mitambo iliyokuwa ikimilikiwa na kampuni ya Dowans Tanzania, imepewa zabuni ya kuzalisha megawati 205 za umeme, wakati NSSF wataingiza mitambo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 150.


Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, iliyowasilishwa na kujadiliwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo Mwananchi limeiona, mpango wa dharura kati ya Agosti 2011 na Desemba 2012 itaigharimu Serikali Sh1.24 trilioni.

Miradi inayotarajiwa kutekelezwa ni ya dharura itakayozalisha megawati 1,032 zikiwemo 572 kati ya sasa na mwezi Desemba mwaka huu na megawati 460 zaidi ifikapo Desemba 2012.

“Ili kukabiliana na mgawo wa umeme kwa kipindi cha dharura, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi, pamoja na taasisi za umma itatumia uwezo wa mitambo iliyopo nchini kukodisha na kununua mitambo ya kufua umeme itakayotosheleza mahitaji ya sasa na baadaye,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ya Ngeleja.

Hata hivyo mpango huo wa Serikali ambao unatarajiwa kujadiliwa bungeni leo, nusura ukataliwe na Kamati husika kutokana na kile wajumbe wa kamati hiyo walichosema kuwa ni kuchelewa kuwasilishwa mbele yake ili ijadiliwe kama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alivyoahidi.

Kamati hiyo ilikutana na upande wa Serikali kwa mara ya kwanza juzi, zikiwa zimebaki siku mbili  kabla Ngeleja hajarejea bungeni leo ili kutafuta ridhaa ya Bunge kupitisha bajeti ya wizara yake, baada ya kufanya marekebisho yenye lengo la kuliwezesha Taifa kuondoka gizani.

Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Pinda iliondoa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bungeni Julai 18, mwaka huu baada ya wabunge wengi, wakiwemo wa upinzani na wale wa CCM kuweka msimamo wa kutoiunga mkono kwa maelezo kwamba haikuwa na majibu ya matatizo ya uhaba wa umeme nchini.

Pinda alitumia kipengele cha 55 (3) (b) pia cha 59(1) vya  kanuni za kudumu za bunge toleo la 2007, ambavyo vinampa nafasi ya kuliambia Bunge sababu za kuahirisha bajeti na muda ambao utatumika katika kuirekebisha.

Pinda aliomba muda wa wiki tatu kwa ajili ya Serikali kujipanga upya, kauli ambayo aliitoa wakati Shirika la Umeme nchini (Tanesco) likiwa limetangaza mgawo wa umeme usio na kikomo kutokana na uhaba wa maji kwenye mabwawa ya kuzalishia nishati hiyo.

Ilikuwa ni ahadi ya Pinda kwamba katikia mchakato huo, Serikali ingeshirikiana na wabunge kupitia kamati za kisekta ambazo baadaye zilitajwa kuwa Kamati ya Nishati na Madini, Kamati ya Fedha na Uchumi na Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, lakini hadi juzi hakuna kamati hata moja ambayo ilikuwa imeshirikishwa katika mkakati huo.

Hali hiyo ndiyo ilisababisha Kamati ya Nishati na Madini juzi kugomea mpango huo wa Serikali kwa maelezo kwamba, haikuwa na muda wa kutosha kuujadili huku baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakihoji sababu za kuchelewa kushirikishwa kwao.

"Jana (juzi), huko hali ilikuwa mbaya sana, wajumbe walichachamaa wakawaambia watendaji wa Serikali kuwa wamekaa muda wote huo halafu wanaleta mpango wao wakati zikiwa zimebaki siku mbili tu, wakasema hawataki," kilieleza chanzo chetu cha habari na kuongeza:

"Lakini busara zilitumika ikaonekana kwamba, tujadili tu ili tuone kama kuna jambo la kusaidia, ndo leo (jana) tunaendelea."

Taarifa ambazo Mwananchi limezipata bungeni zilidai kuwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba ilishaomba kukutana na uongozi wa Wizara zaidi ya mara tatu, lakini kila walipotaka kufanya hivyo, upande wa Serikali ulisema hauko tayari.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, wiki hii aliomba mwongozo wa Spika, akihoji sababu za Serikali kutokutana na kamati husika tangu kuahirishwa kwa mjadala wa hotuba ya Nishati na Madini, lakini Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema: "muda bado unaruhusu Serikali kukutana na kamati husika”.

Mwananchi limedokezwa kuwa huenda bajeti hiyo ikapata wakati mgumu wakati bunge litakapokaa kama kamati, kutokana na ukweli kwamba ni kamati ya Bunge ya kisekta moja tu iliyopata fursa ya kushiriki mchakato wa maandalizi yake, tena nyakati za mwisho tofauti na matarajio ya awali ya kushirikishwa kwa kamati tatu.

Umeme unaotarajiwa
Kwa mujibu wa mpango huo wa Serikali, umeme unaotarajiwa kupatikana kutokana na mpango wa dharura ni megawati 572, kiasi ambacho ni zaidi ya megawati 272 ya kiasi cha megawati 300 kinachohitajika.

Mbali na Symbion na NSFF, wanaotarajiwa kuzalisha megawati 355, kiasi kingine cha umeme kinatarajiwa kutokana na uzalishaji wa kampuni za IPTL ambao wameongeza megawati 80 baada ya kuanza kuzalisha kwa uwezo wake wote na nyongeza ya megawati 37 kutokana na mtambo wa sasa wa Symbion ambao unazalisha megawati 75 kwa sasa kutokana na uhaba wa gesi.

Ngeleja aliiambia kamati kuwa, Symbion wanatarajia kutumia mafuta ya Jet A-1 ili kuzalisha megawati 37  ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, wakati kampuni ya Agrreko imepewa dhamana ya kuwezesha upatikanaji wa megawati 100.

“Serikali imeidhamini Tanesco kukodi mitambo hiyo kupitia Benki ya CRDB na mitambo tayari imeingia Tanzania. Kampuni ya Aggreko International itazalisha umeme kwa mkataba wa mwaka mmoja,” inaeleza sehemu ya mpango huo.

Symbion wanatarajiwa kufunga mitambo yao nchini katika muda usiozidi miezi minne na kwa mujibu wa taarifa ya Serikali, mitambo hiyo itaongizwa kwa awamu ambapo mwezi Septemba italeta mitambo ya megawati 45 ambayo itafungwa Ubungo jijini Dar es Salaam.

Mingine ni ule wa megawati 110 utakaoletwa nchini Oktoba 2011 na kufungwa mjini Dodoma, wakati mtambo wa mwisho utakaowasili nchini  Desemba, mwaka huu. Mitambo hiyo, kila mmoja utakuwa na  uwezo wa kuzalisha megawati 50 itafungwa mjini Arusha.

Gharama za mpango
Kwa mujibu wa Mpango wa Dharura wa Serikali wa Kukabiliana na uhaba wa Umeme ambao Mwananchi limeuona, gharama za kununua umeme wa dharura kati ya mwezi Agosti na Desemba, mwaka huu ni Sh523 bilioni, wakati mauzo ya umeme yatakuwa ni Sh115 bilioni tu.

“Hii ni sawa na tofauti ya Shilingi bilioni 408 ambazo Tanesco itakopa kwa udhamini wa Serikali,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ya Waziri Ngeleja kwa kamati ya Bunge.

Bajeti ya Wizara hiyo ambayo iliwasilishwa Julai 15, mwaka huu na kukataliwa na wabunge ilikuwa ni zaidi ya Sh600 bilioni na kutokana na nyongeza ya sasa, bajeti nzima itakuwa zaidi ya Sh1 trilioni.

Kwa mujibu wa mpango huo, miradi hiyo itakayotekelezwa katika muda wa kati na muda mrefu itagharamiwa na kwa taratibu za kawaida zinazoruhusu Tanesco kukopa na Serikali kuongeza uwekezaji, sekta binafsi na wananchi kushiriki kwa kuongeza bei ya umeme.

Taarifa zaidi zinasema sehemu ya fedha za sasa zinatokana na mkopo wa dola za Kimarekani milioni 250 kutoka benki ya Stanbic ambao ulisainiwa wiki iliyopita baina ya benki hiyo na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo.

Wakati Pinda akiondoa hoja ya wizara hiyo Bungeni Julai 18, alisema Serikali inakwenda kutafuta fedha na ingelazimika kupunguza posho za watumishi wake ili kukomesha tatizo la umeme.

"Hata ikibidi tukate posho zetu, tubane matumizi ya magari, ili mradi tufanikishe mpango wa kuwapatia Watanzania umeme wa kuaminika," alisema Pinda.

Mvutano kikaoni
Hata hivyo kulikuwa na mvutano miongoni mwa wajumbe wa kamati ya Nishati na Madini ya Bunge na serikali kutokana na gharama za uwekezaji ambazo Serikali inatakiwa kilipa kwa megawati 272 za ziada.

“Katika mpango huo wa dharura ni kama kuna megawati 272 ambazo ni extra (ziada) na hizi tunatakiwa eti kuzilipia capacity charges (gharama za uwekezaji) hata kama tutakuwa hatuzitumii, nadhani hapa sisi hatutakubali,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.

Jana, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliendelea kufanya vikao vyake na Serikali, wakiwemo watendaji wa Tanesco ambao waliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Semindu Pawa na Mkurugenzi Mtendaji, William Mhando.

Baada ya kumaliza kikao na watendaji wa Serikali, Kamati hiyo iliendelea na kikao hadi majira ya jioni, hivyo kusababisha kikao cha Kamati ya wabunge wa CCM kilichokuwa kimepangwa kufanyika jana saa 8.00 mchana kuahirishwa hadi saa 2.00 usiku.

Baadhi ya wabunge wa CCM ambao walifika ukumbi wa Pius Msekwa jana mchana walilazimika kuondoka baada ya kutoonekana kwa dalili ya kufanyika kwa kikao hicho na mmoja wao alisikika akisema kilikuwa kimeahirishwa hadi usiku.

Kikao hicho kilichoitishwa na Katibu wa wabunge hao wa chama tawala, Janester Mhagama kilitarajiwa kuweka mikakati ya kupitisha bajeti hiyo iliyoachwa kama ‘kiporo’.

Kanuni yatenguliwa
Maandalizi ya kuwezesha bajeti ya Nishati na Madini kujadiliwa leo yalianza jana asubuhi pale Spika wa Bunge, Anne Makinda alipomwita Lukuvi kwa ajili ya kutoa hoja ya kutenguliwa kwa kanuni ya 28 ili kuruhusu wabunge kukutana Jumamosi.

Hoja hiyo iliungwa mkono, kisha kupitishwa na bunge, hivyo kuruhusu bunge kukutana leo kuanzia saa 3.00 asubuhi katika kikao ambacho kitaanza bila maswali na majibu.

Spika Makinda akijibu mwongozo ulioombwa na Mnyika, alisema kikao kitaanza saa 3.00 na hakuweka ukomo wa muda wake akisema lengo ni “kutoa fursa nzuri kwa wabunge kujadili hoja hiyo kwa ukamilifu”.

Mnyika alikuwa ameomba mwongozo akitaka Spika aseme ni saa ngapi kikao hicho kitamalizika akihofia kwamba iwapo kingemalizika saa saba mchana, wabunge wasingepata muda wa kutosha kuihoji Serikali.

Kwa mujibu wa Spika, kikao cha leo kitaanza kwa Waziri Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima, kujibu hoja zote za wabunge walizotoa Julai 15 na Julai 18, 2011 na baada ya hapo Bunge litakaa kama kamati kupitia vifungu vya bajeti ya wizara hiyo.

No comments: