ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 29, 2011

Siri ya Makinda kuteua timu ya wabunge hawa


  Kuanza kukutana Jumatatu
  Wasomi nao watoa angalizo
Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo
Wakati kamati teule iliyoundwa kumchuguza Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo, ikitarajia kukutana kwa mara ya kwanza Jumatatu ijayo, wasomi na wadau mbalimbali wametoa hisia zao juu ya aina ya wabunge walipewa kazi hiyo.
Wasomi mbalimbali waliozungumza na NIPASHE wamesema kuwa ni vema kati hiyo ikaachwa ifanye kazi kwa uhuru, na kutaka ichambue kila kitu ili ukweli ujulikane.
Huku maoni hayo yakitolewa, tathmini ya walioteuliwa inaonyesha kuwa ni wabunge wakimya, ambao hawaonyeshi kufunikwa na hisia kali za kiharakati, jambo linaloelezwa kwamba ndiyo sababu hasa za Spika Anne Makinda, kuwapendelea kuliko wabunge ambao tayari wana majina makubwa.

Kwa hatua hiyo, Makinda anaonekana kutaka kujenga historia yake mpya mbali ya kile kilichofanywa kwenye Bunge la Tisa lililoongozwa na Spika Samuel Sitta.
Kadhalika, mwelekeo huu wa Makinda unaonyesha kuwa ni kuepuka kuteua wabunge ambao wanaweza kwa njia moja au nyingine kufungamanishwa na siasa za makundi ambazo zimekuwako ndani ya siasa za Tanzania kwa muda mrefu kwa sasa.
Mwelekeo huu unafanana na mbinu za Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, wakati alipoteua mawaziri wake aliposema kuwa hakuwa anaanza awamu mpya ya serikali, kwa maana hiyo kukwepa kufungwa na yaliyofanywa na watangulizi wake.
Mwaka 1995 alipokuwa anatangaza baraza la mawaziri la kwanza baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo alisema kuwa mawaziri wake walikuwa ni wa serikali ya awamu tatu ingawa hakuwa ameulizwa swali la kwa nini alikuwa amewaacha mawaziri wengi wa awamu ya pili ambao alikuwa mmoja wao.
Hatua ya Mkapa alitaka kuonyesha kwamba awamu yake ilikuwa ni tofauti na ya pili, kwani ziilingia sura nyingi mpya katika baraza hilo, kuanzia Waziri Mkuu Mpya, Frederick Sumaye, na mawaziri wengine wengi na manaibu wao.
Dhana kama hiyo ndiyo inaelekea kumkaa Makinda, kwamba wabunge aliowateua kuunda kamati teule ya Jairo, hakuwapa fursa hata wale walioibua hoja hiyo bungeni wala wabunge wenye majina makubwa.
Wabunge walioibua hoja hiyo ni Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo, ambaye Julai 18, mwaka huu wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Nishati na Madini, aliwasilisha barua ya Jairo ya kuchangisha fedha.
Shellukindo alimtuhumu Jairo kuwa alikuwa ameandika kwa taasisi zilizochini ya wizara hiyo akizitaka kuchangiha Sh. milioni 50 kila moja ili kufanikisha kupitishwa kwa bajeti ya wizara, fedha zilizodaiwa kuwa zililenga kuwahonga wabunge.
Hata hivyo, hoja hiyo baada ya kutaka kuzimwa kiaina na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kwa kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Lodovic Utouh, wabunge wote waliwasha moto bungeni nao hawakuteuliwa na Spika Makinda kuwa wajumbe wa kamati teule.
Miongoni mwa wabunge hao ni pamoja na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe; Mbunge wa Simanjiro (CCM) Christopher ole Sendeka na Zainabu Vullu wa Viti Maalum CCM.
Spika Makinda hakuwateua hawa si kwa bahati mbaya, kwani historia ya Bunge la Tisa inaonyesha wazi kuwa Zitto aling’aa kwenye suala la madini (Buzwagi) hadi akateuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya kupitia sheria za madini; Sendeka alikuwa mjumbe wa Kamati ya Richmond na Beatrice pia hawezi kuwekwa mbali na aliyofanya aliyekuwa Mbunge wa Bumbuli (CCM), William Shellukindo.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ramo Makani, alisema hivi sasa wajumbe wa kamati wanapumzika kwa wiki moja ili kupunguza uchovu wa shughuli za Bunge.
Alisema: “Tumejipa muda wa kupumzika kwa sababu tulikuwa na kazi kubwa ya kuhudhuria shughuli za Bunge, lakini hata kazi inayotukabili ni kubwa, kwa hiyo tunaanza kazi Septemba tano.”
Alipoulizwa mkoa ambao kamati yake itakutana, Makani ambaye pia ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini (CCM), alisema: “Itategemea tu, tunaweza kukutana Dar es Salaam au kwingineko, tutajua baadaye.”
Wakati huo huo, wakitoa maoni yao kuhusiana na kamati hiyo baadhi ya wasomi walisema, endapo itaachiwa huru pasipo kuingiliwa na serikali, itafanya kazi nzuri.
“Ninaamini kamati itafanya kazi nzuri endapo itaachwa huru, bila kuingiliwa na serikali na pia tunaiomba isiogope kuwaweka wazi viongozi wote ambao kwa namna moja ama nyingine, watakuwa walihusika,” alisema Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Donath Olomi na kuongeza:
“Haiwezekani mambo haya yawe yanafanyika bila hata ya waziri husika kufahamu, hivyo tunaiomba tume (kamati) ichunguze kwa makini na endapo ikigundua kama na waziri naye alihusika, isisite kumwajibisha.”
Kwa upande wake, Dk. Azaveli Lwaitama, ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, aliiomba kamati hiyo ieleze kama ni kawaida kwa serikali kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia kupitisha bajeti za wizara.
“Tunaiomba kamati pamoja na yote, pia itueleze kama ni kawaida kwa serikali kukusanya fedha za kupitisha bajeti,” alisema na kuongeza:
“Kadhalika, itueleze kama utaratibu huo haukiuki dhana ya Bunge ya kuidhinisha mapato na matumizi ya serikali. Lakini mbali na hilo, itueleze utaratibu huo una maana gani.”
Alisema kila mwaka Bunge limekuwa likiidhinisha matumizi yote ya serikali, zikiwemo posho na mishahara ya watumishi wa kila wizara, zikiwemo fedha za maandalizi ya bajeti kwa mwaka unaofuata.
Naye Dk. Benson Bana, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa UDSM, alisema haoni kama kuna kitu kipya ambacho kitatofautiana na kile ambacho kilifanywa na kamati iliyopita isipokuwa anachoona ni Bunge kutaka kuingilia mamlaka ya Serikali.
"Uamuzi wa Bunge kuunda kamati nyingine ni kuingilia mhimili wa dola (Serikali), mambo haya yataleta sokomoko na kama walitaka kufanya hivyo, wangeunda kamati kabla serikali haijaunda tume yake," alisema.
Dk. Bana alifafanua: "Wangeunda mapema mara tu baada ya mbunge (Beatrice Shellukindo), kutoa ushahidi wa barua bungeni ... wanavyorudia wanataka tu kuingilia mamlaka nyingine."
Alisema: "Na huyo mbunge alizipataje documents (nyaraka), za serikali na kuziwasilisha bungeni? Lazima naye aulizwe alitumia njia gani kuzipata."
Kamati hiyo ilitangazwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, mwishoni mwa wiki iliyopita muda mfupi kabla ya kuahirisha Mkutano wa Nne wa Bunge, mjini Dodoma.
Wajumbe wanaounda kamati hiyo Makani ambaye ni Mwenyekiti ni Gosbert Blandes (Karagwe-CCM), Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF), Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema) na Martha Umbulla (Viti Maalum-CCM).

Spika Makinda pia alizitaja hadidu rejea za kamati hiyo kuwa ni kuchunguza utaratibu uliobainika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilisha uwasilishaji wa hotuba za bajeti za wizara bungeni.
Nyingine ni kamati hiyo kuangalia uhalali wa utaratibu huo kisheria ama kikanuni, iwapo fedha hizo kama zinakasimiwa katika bajeti husika pamoja na kuangalia matumizi halisi ya fedha husika.
Pia kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu uchunguzi alioufanya kuhusiana na agizo la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa taasisi zilizo chini yake kwa ajili ya kukamilisha uwasilishaji wa bajeti ya wizara hiyo bungeni.
Vile vile, kuchunguza mfumo wa serikali kujibu hoja zinazotolewa bungeni na utaratibu wa kuliarifu Bunge matokeo ya utekelezaji wa hoja hizo.
Kadhalika, kamati hiyo imepewa rejea ndogo ndogo, kuangalia usahihi wa utaratibu uliotumiwa na Luhanjo katika suala la Jairo, ili kubaini kama utaratibu huo umeathiri dhana ya haki na madaraka ya Bunge.
Hadidu rejea nyingine ni kuangalia nafasi ya mamlaka ya uteuzi kwa ngazi ya makatibu wakuu katika kushughulikia masuala ya nidhamu ya anaowateua na kuangalia mambo mengine yoyote yanayohusiana na masuala hayo.
Kamati hiyo itafanya kazi kwa muda usiozidi wiki nane na itawasilisha taarifa yake wakati wa Mkutano wa Tano wa Bunge, utakaoanza Novemba 8, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: