Saturday, October 29, 2011

Simba kwisha habari yao!-Habari Leo

Image
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga wamewafunga wapinzani wao wakubwa Simba kwa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Bao pekee la Yanga katika mchezo lilifungwa na mshambuliaji Davis Mwape kutoka Zambia katika dakika ya 75 baada ya mabeki Victor Costa na Juma Nyosso kujichanganya na mpira kumkuta mfungaji aliyefunga kwa shuti kali akiwa ndani ya eneo la penati.

Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 24 kutokana na michezo 12 iliyocheza, hivyo kuendelea kujikita katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kuu, huku Simba ikiendelea kubaki kileleni kutokana na kuwa na pointi 27, tatu zaidi ya Yanga. 


Simba iliuanza kwa kasi mchezo huo huku ikifanikiwa kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Yanga na kama mshambuliaji wa timu hiyo, Emmanuel Okwi angekuwa makini, basi angeweza kuiandikia timu yake bao la mapema katika dakika ya pili baada ya kupaisha mpira aliopewa na Saidi Nassoro kutoka upande wa kulia.

Mlinzi Chacha Marwa wa Yanga nusura ajifunge mwenyewe wakati akitaka kuokoa shuti la mshambuliaji Emmanuel Okwi katika dakika ya tatu, na kuwa kona ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

Yanga wakajibu mapigo katika dakika ya 11 baada ya mshambuliaji Mwape kupiga shuti akiwa nje kidogo ya eneo la penati baada ya kupokea pasi kutoka kwa Nurdin Bakari, lakini shuti lake likaishia mikononi mwa kipa Juma Kaseja.

Simba iliyoonekana kumiliki vizuri mpira hasa katika sehemu ya kiungo kwa kuwatumia wachezaji wake Shomari Kapombe, Amri Kiemba na Jerry Santo ilikosa bao la wazi katika dakika ya 13 wakati mshambuliaji Okwi akipaisha juu ya lango la Yanga baada ya kupokea pasi nzuri ya Felix Sunzu.

Ukuta wa Yanga, hasa mlinzi Marwa alionekana kujichanganya na kama washambuliaji wa Simba wangekuwa makini basi wangeweza kutumia udhaifu huo kupata bao la kuongoza. Sunzu aliyeonekana kuisumbua sana ngome ya Yanga aligongeana vyema na Kapombe na Juma Jabu lakini shuti lake lilidakwa na kipa wa Yanga, Yaw Berko.

Amri Kiemba katika dakika ya 14 alikosa bao la wazi akiwa peke yake na kipa Berko baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Sunzu lakini shuti alilopiga liligonga nyavu za pembeni.

Mshambuliaji Kenneth Asamoah alipiga shuti dhaifu na kudakwa na kipa Kaseja baada ya Godfrey Taita na Mwape kugongeana vizuri kabla ya mpira kumfikia Asamoah.

Simba walipata pigo baada ya beki wake wa kulia Nassor Saidi kutolewa nje baada ya kuumia wakati akijaribu kucheza mpira wa juu na nafasi yake kuchukuliwa na Patrick Mafisango.

Mwamuzi Oden Mbaga alimuonesha kadi ya njano Oscar Joshua katika dakika ya 39 baada ya kumchezea rafu Okwi, huku akimuonesha tena kadi ya njano kiungo Santo katika dakika ya 44 kutokana na kumfanyia faulo kiungo Haruna Niyonzima wa Yanga.

Kipindi cha pili Simba waliendelea kuliandama lango la Yanga na nusura mshambuliaji Sunzu afunge katika dakika ya 47 baada ya kupokea krosi kutoka kwa beki Jabu, lakini kichwa kizuri alichokipiga kilipaa juu kidogo ya lango la Yanga.

Katika dakika ya 62, wachezaji wa Simba walimzonga mwamuzi Mbaga wakilalamikia kunyimwa penati baada ya Okwi kuangushwa ndani ya eneo la penati na mwamuzi kuamuru faulo kupigwa nje kidogo ya eneo hilo.

Timu zote zilifanya mabadiliko kadhaa wakati Simba iliwaingiza Haruna Moshi, Mwinyi Kazimoto kuchukua nafasi za Kiemba na Ulimboka Mwakingwe, Yanga nao iliwatoa Hamisi Kiiza na kumuingiza Idrisa Rashidi.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwanufaisha zaidi Yanga kwani katika dakika ya 75 waliweza kuandika bao hilo pekee kupitia kwa mshambuliaji Mwape.

Baada ya bao hilo, Yanga walimtoa Mwape na kumuingiza Jerry Tegete kabla ya dakika za mwisho kumtoa Asamoah na kumuingiza Rashidi Gumbo, hata hivyo mabadiliko hayo hayakuweza kubadili sura ya mchezo huo.

Yanga: Yaw Berko, Godfrey Taita, Oscar Joshua, Chacha Marwa, Nadir Haroub, Juma Seif, Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Davis Mwape/Jerry Tegete, Kenneth Asamoah/Rashidi Gumbo, Hamis Kiiza/Idrissa Rashidi.

Simba: Juma Kaseja, Nassor Masoud/Patrick Mafisango, Juma Jabu, Juma Nyosso, Victor Costa, Jerry Santo, Shomari Kapombe, Amri Kiemba/Haruna Moshi, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Ulimboka Mwakingwe/Mwinyi Kazimoto.

Katika matokeo mengine, Toto African ya Mwanza ilishindwa kuutumia vema uwanja wa nyumbani CCM Kirumba baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Coastal Union, matokeo ambayo pia yameikumba Polisi Dodoma kwenye uwanja wa Jamhuri baada ya kubanwa mbavu na JKT Oljoro.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake