Friday, October 28, 2011

Zitto apelekwa India chini ya 'ulinzi mkali’

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akimpa pole Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhumbili kabla ya kupelekwa India. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Kabwe Zitto aliyekutwa na vijidudu 150 vya malaria na kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), amepelekwa India kwa ajili ya matibabu zaidi.

Hata hivyo, tofauti na matarajio ya wengi kuwa angefikishwa uwanjani hapo na gari la wagonjwa baada ya hali yake kuripotiwa kuwa si nzuri, Zitto alifika uwanjani hapo majira ya saa 8:55 alasiri akiwa katika gari la Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambalo pia Katibu Mkuu Blandina Nyoni alipanda.


Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na maofisa wengine wa Ofisi ya Bunge walikuwapo uwanjani hapo kumsindikiza.

Gari hilo lilikuwa miongoni mwa magari matatu yaliyokuwa katika msafara wa kumsindikiza mbunge huyo, yakiongozwa na pikipiki ya polisi.

Mara baada ya kufika uwanjani hapo, Zitto alishuka mwenyewe garini na kutembea, lakini hakuna mwanahabari aliyepewa upenyo wa kumkaribia, kwani `alitoroshwa’ haraka na kuingizwa chumba cha wageni mashuhuri uwanjani hapo.

Zitto, mmoja wa wabunge machachari nchini, baadaye majira ya saa 10:48 alionekana akitembea kwenda kupanda ndege akiwa ameambatana na kaka yake, Salum Mohammed na muuguzi mmoja kutoka MNH.

Hata hivyo, habari ambazo gazeti hili imezipata kutoka kwa mmoja wa watu wa karibu wa Zitto, zinasema kuwa mbunge huyo wa Chadema ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani bungeni, anasumbuliwa na maumivu ya kichwa kutokana na mishipa midogo ya kichwa kubana.

“Kinachomsumbua sana kwa sasa ni kubana kwa mishipa midogo ambayo inaungana na macho na pua na hii ndiyo inayomfanya kupata maumivu makali ya kichwa. Hivyo wameona ni heri akafanyiwe uchunguzi zaidi, lakini kuna uwezekano akafanyiwa upasuaji,” alisema.

Chanzo cha habari kinabainisha zaidi kuwa, hali yake ilikuwa inaendelea vizuri kiasi kutokana na kupatiwa matibabu ya malaria, hivyo kushusha joto na homa.

“Amepewa matibabu na homa imeshuka kwa sasa, jana usiku (juzi) aliweza kula vizuri na mpaka anaondoka hali yake si mbaya,” kimeeleza chanzo hicho.

Kabla ya kuondoka jana jioni, mchana Zitto alitembelewa hospitalini hapo na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Zitto, kabla ya kuhamishiwa Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU) cha MNH, alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan.

Hata hivyo, taarifa zilizotolewa baada ya kufanyiwa uchunguzi Muhimbili alibainika kuwa anasumbuliwa na malaria kutokana na kuwa na wadudu 150 ambao ni wengi kwa mtu kuweza kuwahimili.

Ugonjwa wa Zitto umekuja huku kukiwa na wimbi kubwa na viongozi zaidi kulazwa katika hospitali za ndani na nje ya nchi kwa uchunguzi wa afya na wengine wakiugua magonjwa mbalimbali.

Katika hospitali ya Muhimbili, Mbunge mwingine, Clara Mwatuma wa Viti Maalumu (CUF), naye alikuwa amelazwa akisumbuliwa na vidonda vya tumbo.

Wakati wabunge hao wakiwa MNH, viongozi wengine wamelazwa nje ya nchi, wakiwamo Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe aliyelazwa nchini India, kama ilivyo kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami ambaye alipelekwa Jumanne wiki hii kwa uchunguzi wa afya yake.

Wengine ni Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya ambaye amelazwa nchini humo kwa miezi kadhaa sasa baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake