.jpg)
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imesema sheria ya kura ya maoni ifanyiwe marekebisho ili kuondoa mapungufu yaliyojitokeza wakati wa kura ya maoni ya kuamua kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyofanyika Julai, mwaka jana.
Hayo yameelezwa katika ripoti ya kura ya maoni iliyotolewa Zanzibar na Mwenyekiti wa tume hiyo, Khatib Mwinyichande jana.
Ripoti hiyo imesema Sheria namba 6 ya mwaka 2010, ifanyiwe tena marekebisho baada ya kujitokeza mapungufu wakati wa zoezi la kura ya maoni iliyofanyika kwa mara ya kwanza tangu Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964.
Alisema sheria hiyo haijaeleza masuala ya msingi kuhusu kura ya maoni ikiwemo utaratibu wa kampeni kabla ya kufanyika kwa kura hiyo.
Aidha, alisema sheria hiyo haijasema namna ambavyo kura zinatakiwa kuhesabiwa baada ya wananchi kukamilisha kazi ya kupiga kura.
‘’Sheria ya kura ya maoni ifanyiwe marekebisho ili kuondoa mapungufu yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wake. imeeleza ripoti hiyo
Hata ripoti hiyo imeleeza kwamba zoezi hilo la kura ya maoni lilifanyika katika mazingira huru na haki kutokana na kutawaliwa na uwazi wakati wa upigaji kura na utoaji wa matokeo yake.
Ripoti hiyo yenye kurasa 38 imesema kwamba wapiga kura wengi hawakujitokeza kutokana na kukosa elimu ya wapiga kura kutolewa kwa kiwango kidogo na kuna baadhi ya maeneo wananchi hawakupata elimu ya uraia kutokana na tatizo la ukata wa fedha.
“Elimu ya wapiga kura haikufika katika maeneo tete hali ambayo ilipelekea kura nyingi katika maeneo hayo kuharibika na kujitokeza wapiga kura kidogo” Ripoti imeleeza.
Mwenyekiti huyo alisema katika ripoti yake madaftari ya wapiga kura yalibandikwa nje ya vituo kwa lengo la kuwapa fursa wapiga kura kuangalia taarifa zao yalichanwa au kubanduluwa na watu wasiofahamika na kusababisha usumbufu kwa wapiga kura kufahamu vituo vyao vya kupigia kura.
“Kuna baadhi ya vituo madaftari ya wapiga kura yaliyokuwa yamebandikwa nje ya vituo kuwapa fursa walpiga kura kuangalia taarifa zao yalichanwa ama kubanduliwa na watu” imeongeza Ripoti hiyo.
Aidha, imeelezwa kwamba waangalizi wa zoezi hilo kupitia vyama vya siasa Zanzibar walikuwa wakilazimisha kupewa taarifa kinyume na sheria zinazosimamia kura hiyo.
Imeelezwa kambwa kutokana na elimu ya uraia kutolewa kwa kiwango kidogo kura 8,721 sawa na asilimia 3.0 ziliharibika katika zoezi hilo .
Ripoti hiyo imeeleza watu 114,630 hawakujitokeza kupiga kura yakuamua Zanzibar kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa kati ya watu 407,669 waliokuwa wamejiandikisha baada ya kujitokeza watu 293,033 sawa na asilimia 71.90 ya watu waliopiga kura
Hata hivyo Ripoti hiyo imeeleza kwamba asilimia 66.40 walipiga kura ya ndio ya kuunga mkono mabadiliko ya muundo wa serikali na asilimia 33.60 walipiga kura ya hapana wakati wa zoezi hilo .
Hata hivyo tume hiyo imesema marekebisho hayo yana umuhimu mkubwa kwa vile sheria hiyo ya kura ya moani ndio itakayoamua mambo mbali mbali ya nchi ambayo yatahitaji kuamuliwa na wananchi kabla ya utekelezaji wake.
Kura ya maoni ilifanyika Julai Mwaka jana ikiwa ni utekelezaji wa azimio la Butiama la Halmashauri kuu ya CCM (NEC) kutaka iitishwe kura ya maoni kabla ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kama muafaka wa kumaliza mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake