ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 21, 2011

Bomani: Gamba litapasua CCM

Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali, Jaji Mark Bomani
Mwandishi wetu
WAKATI mfululizo wa vikao vya CCM vya Kamati ya Maadili, Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), vinaanza leo Mjini Dodoma, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali, Jaji Mark Bomani amekitaka chama hicho kuachana na mpango wa kujivua gamba akisema utakipasua.

Moja ya agenda kubwa na ambayo imekuwa ikiwasumbua makada, wafuasi na hata wapinzani wa chama hicho ni hiyo ya kujivua gamba yenye lengo la kukisafisha kwa kuwaweka kando wanachama na viongozi wake wanaosadikiwa kukumbatia vitendo vya ufisadi na kukipaka matope mbele ya jamii.

Jaji Bomani akionekana kuguswa na utekelezaji wa mpango huo, ametoa waraka alioupa kichwa cha habari: “Majibu juu ya Hali ya Nchi.” Katika suala la kujivua gamba alisema: “Chama Cha Mapinduzi kimejiingiza kwenye mtego mkubwa wa kujivua gamba. Kwa maoni yangu, CCM ingeachana na dhana ya kujivua gamba ambayo hatima yake ni mpasuko na mfarakano mkubwa usio wa lazima ndani ya chama hicho.”

Jaji Bomani alishauri kwamba kwa kuwa CCM kitafanya uchaguzi wa ngazi zake zote mwakani, ingekuwa nafasi nzuri kwake kujisafisha.
Tayari kikao cha Nec cha Agosti, mwaka huu kilikwishaamua kwamba watuhumiwa wote wa ufisadi wakiwemo wa Richmond, kashfa ya rada na Kagoda wawajibike wenyewe au wasubiri kufukuzwa katika nyadhifa zao katika kipindi cha siku 90 ambazo zimekwishapita.

Hadi sasa CCM inaonekana kuchelewa kuwachukulia hatua watuhumiwa hao ambao wamekuwa wakitajwa kukipotezea chama hicho mvuto kutokana na wananchi kuchukia ufisadi na mafisadi, hali ambayo inadaiwa kuwa ilichangia kukipa matokeo mabaya kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Lakini, kada huyo ambaye aliwahi kugombea urais kupitia chama hicho mwaka 1995, alisisitiza kwamba kwa sasa hivi kingeweza kuteua kamati, jopo teule au kikosi kazi (task force), kupitia upya mwenendo wote wa kupata uongozi.

“Utaratibu huo ungekipa chama sura au gamba jipya kwa kutumia maadili mazuri ya kukipatia viongozi bora bila ya vurugu zozote.”

Jaji Bomani alisema jopo la namna hiyo linaweza kufanya kazi hiyo na kuikamilisha ndani ya miezi michache, kabla ya uchaguzi wa mwakani.Mpango wa chama kujivua gamba ulitangazwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete katika maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwake ambayo aliyatumia pamoja na mambo mengine, kueleza umuhimu wa chama kujihuisha kwa kujivua gamba ili kuwaacha njiani watu wote wachafu wenye tuhuma za ufisadi.

Watu hao ni wale ambao hawaendani wala kushabihiana na historia ya chama hicho ambacho kilirithi miiko na maadili ya viongozi kutoka TANU ambayo, uadilifu ilikuwa ni kigezo kikuu kwa mwanachama.    

Serikali iachane na ATCL
Jaji Bomani akigusia uchumi, aliitaka Serikali kuachane na suala la kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) akitaka iachie watu na makampuni binafsi kutoa huduma hiyo ya usafiri wa ndege akisema: “Serikali sasa hivi haina uwezo wa kutoa huduma hiyo.”

“Huwezi kutoa huduma ya usafiri wa ndege kwa ndege moja au mbili! Wenzetu Emirates hivi majuzi wameagiza ndege mpya 50 kwa mpigo! Wacha hao wenye uwezo wa usafiri wa ndege wahudumiwe na kampuni au mashirika ya binafsi.”

Bomani alisema kitu ambacho kinatakiwa kupewa kipaumbele nchini ni huduma ya reli na barabara... “Huu ndiyo wa wananchi walio wengi na wenye nafuu. Juhudi za Serikali zielekezwe kwenye kufufua na kuendeleza usafiri wa reli ili mizigo isafirishwe kwa gharama nafuu ya reli, barabara na maji.”
Ataka nishati mbadala

Akizungumzia huduma ya nishati alisema ahadi zilizotolewa na Wizara ya Nishati na Madini mara kawa mara hazionekani kutekelezwa kwa kiwango kinachoridhisha hivyo kupunguza imani ya wananchi.

“Nishati ambayo haijapewa msukumo wa kutosha ni nishati ya jua (solar power) na nishati upepo (wind power). Hizi ndizo nishati ambazo zinaweza kupatikana mahali kwingi nchini na kuwakomboa wananchi vijijini," aliongeza.

“Mfano hai ni maendeleo ya nishati ya jua India. Nishati za jua na upepo licha ya kuwa za nafuu ni nishati ambazo haziathiri mazingira. Mbona hazichangamkiwi?”

Kuhusu madini, alisema sekta hiyo nayo haijashughulikiwa vya kutosha akitoa mfano wa Waziri wa Nishati na Madini (William Ngeleja), ambaye aliliahidi Bunge kwenye mkutano wa bajeti kwamba ifikapo mwanzoni mwa Septemba, mwaka huu kampuni za madini hasa dhahabu zingekuwa zinatozwa mrabaha wa asilimia nne ya jumla ya mapato yake (gross revenue) lakini hadi sasa haijafanyika.

"Kitu hiki kingeleta manufaa makubwa. Lakini, leo hii ni Novemba! Hili nalo limefikia wapi?," alihoji.

Aliipongeza Kampuni ya Barrick African Gold kwa uamuzi wake wa kuuza baadhi ya hisa kwa Watanzania kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kuanzia mwezi ujao.

Uamuzi huo wa Barrick ulikuwa moja ya pendekezo muhimu la Kamati ya Bomani iliyoundwa na Rais Kikwete, ambayo pamoja na mambo mengine ilipewa kazi ya kudurusu mikataba ya madini na kuishauri Serikali kuona namna ambavyo nchi ingenufaika.

Mwananchi

No comments: