SIKU chache baada ya Bunge kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 bila wabunge wa Chadema kushiriki mjadala huo, Kamati Kuu ya chama hicho imeunda kamati ndogo ili kuomba kukutana na Rais Jakaya Kikwete.
Nia ya mkutano wa kamati hiyo ndogo na Rais Kikwete ni kutaka kumweleza msimamo wa chama hicho kuhusu sheria hiyo na mchakato mzima wa Katiba mpya.
Hatua hiyo imetokana na maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana juzi Dar es Salaam kuzungumzia mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na mchakato wa Katiba mpya baada ya sheria hiyo kupitishwa na Bunge Ijumaa.
Wajumbe wa Kamati hiyo ya watu saba na nafasi zao kwenye mabano, ni Freeman Mbowe (Mwenyekiti na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni), Said Arfi (Makamu Mwenyekiti Bara na Mbunge Mpanda Mjini), Said Issa Mohammed (Makamu Mwenyekiti Chadema Zanzibar) na Dk Willibrod Slaa (Katibu Mkuu).
Wengine ni Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari, wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho. Mbowe ndiye atakayeongoza kamati hiyo ndogo.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana katika ofisi za makao makuu ya Chadema, Dar es Salaam, Mbowe alisema hatua hiyo inatokana na maazimio ya Kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho ambayo imedai kuwa Serikali ya CCM haina dhamira ya kweli ya kuunda Katiba mpya.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema katika kikao hicho masuala mbalimbali yalizungumzwa, ikiwa ni pamoja na namna Muswada wa Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2011 ulivyopitishwa na Bunge kuwa Sheria na kudai kwamba kitendo cha Chadema na wabunge wengine kususa mjadala, ni cha kishujaa kwa kuwa sheria hiyo haikufuata taratibu na kanuni za Bunge.
“Muswada uliopitishwa kuwa sheria na Bunge hauwatendei haki Watanzania, Kamati Kuu imejadili kwa kina na kuona kwamba ingawa Bunge limepitisha sheria, bado kuna fursa ya kitaifa kutokubaliana na hatua hiyo, ambayo haikuzingatia maoni ya wadau, tumeona CCM haina dhamira ya kuunda Katiba mpya,” alisema Mbowe.
Alidai kuwa CCM imekuwa ikipotosha hoja ya Chadema kuwa ingepewa ridhaa ingeanza mchakato wa kupata Katiba mpya ndani ya siku 100 na si kuunda Katiba ndani ya siku hizo, hivyo Kamati Kuu kuamua kuunda Kamati ndogo ya viongozi wa chama na baadhi ya wabunge kukutana na Rais Kikwete kwa nafasi yake ya urais na si uenyekiti wa CCM.
Yatumia vitisho Ingawa hakubainisha wazi ni lini wanatarajia kuonana na Rais Kikwete, Mbowe alisema, “Mchakato wa kuonana naye umeanza leo (jana) na ni mapema, katika nafasi yake ya kwanza aliyonayo ikiwa atakubali kuzungumza nasi, akikubali marekebisho tutaungana nao katika mchakato, vinginevyo tutarudi kwa wananchi na tusije kulaumiana”.
Mbowe alisema sheria hiyo ina upungufu mwingi na kama hautarekebishwa, Katiba mpya haitatoa majibu kwa maswali ya Watanzania, hivyo Kamati Kuu kukiagiza chama kufuatilia majibu ya Bunge kuhusu mchakato huo, ili kujiridhisha na kuonya kuwa Katiba si suala la chama fulani bali jamii nzima.
Katika hatua nyingine, Mbowe alisema Kamati Kuu ililaani na kusikitishwa na kile alichokiita hatua ya CCM na CUF kupotosha umma kuhusu msimamo wa Chadema juu ya Muungano na kueleza kuwa hotuba ya Lissu bungeni, ndiyo msimamo wa Chadema na kamwe chama hicho hakiwachukii Wazanzibari bali kinasimamia haki.
“Suala la Serikali tatu lilikuwa ajenda ya CUF, sasa nashangaa wenyewe wanakula matapishi ya CCM, hatuwachukii Wazanzibari wala Muungano, bali suala hili linapaswa liwe la kitaifa,” alisema Mbowe.
Kwa mujibu wa Mbowe, Kamati Kuu hiyo pia iliitaka Polisi kuondoa agizo la kuzuia maandamano na mikutano ya hadhara ya chama hicho ya kuelimisha umma kuhusu mchakato wa Katiba mpya, kwa kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, aliwaangiza viongozi wa CCM kutoa elimu, hivyo nao wasizuiwe.
Alipoulizwa kuhusu msimamo wa Chadema katika suala la Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, Mbowe alisema maoni waliyotoa wabunge wa Chadema wakati wa mjadala wa ripoti hiyo bungeni ndio msimamo wa chama hicho.
Awali Katibu Mkuu, Dk Slaa aliwapongeza wabunge wa Chadema na waliowaunga mkono kususia Muswada wa Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa kuwa sheria, kwa kuwa wangebaki ndani wangehalalisha kupatikana Katiba kwa mchakato aliouita haramu.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, akizungumza katika mkutano huo kuhusu sababu za kususia mjadala bungeni, alisema hawakuwa tayari kuona hatua ya kupitishwa kwa Muswada ambao alidai ulikuwa mpya na ulipaswa kufanyiwa marekebisho makubwa kwa kusomwa mara ya kwanza na si ya pili kama ilivyofanyika.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment