ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 20, 2011

Kawawa ahofia usalama wa wabunge mjengoni



Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa, ameonyesha hofu ya wabunge kupata madhara iwapo patatokea hatari katika ukumbi wa Bunge, kutokana na mfumo wa kieltroniki uliopo kwenye milango ya jengo hilo.
Kawawa alionyesha hofu hiyo baada ya kuomba mwongozo kwa Spika bungeni jana, ambapo alisema katika kuimarisha usalama bunge limeweka milango inayotumia mfumo wa eletroniki, lakini wakati wa kikao cha kamati yake kilichofanyika katika ukumbi wa utawala namba133, Katibu wa kamati hiyo alikuwandiyo pekee mwenye uwezo wa kufungua mlango. Alisema kwa kutumia kadi ya electroniki kila mtu aliyekuwa akiingia ndani Katibu huyo alikuwa akilazimika kuinuka na kwenda kumfungulia mlango, jambo ambalo lilipoteza usikivu wa kazi ya kamati.
“Vile vile kiusalama si vyema mtu mmoja ndiyo awe mfungua mlango, kwa sababu kama lolote linaweza kutokea wabunge tunaweza kupata madhara,” alisema na kuongeza:

“Juzi nilikwenda kupata huduma katika ofisi za utawala kwa shughuli ambayo nilikuwa natakiwa kuifanya kwa dakika tatu lakini ilichukua dakika 20 kwa sababu aliyekuwa akinihudumia ndio alikuwa akiwafungulia watu waliokuwa wakitaka kuingia katika chumba hicho. Mheshimiwa Spika kwani ni lazima tutumie kadi wakati wa kutoka?, mi nakubaliana kabisa na kuingia kwa kutumia kadi zetu, utawala unaweza kumwelekeza mkandarasi aliyeweka electroniki kadi kutumia vitufe kufungulia mlango,” alishauri. Akijibu mwongozo huo, Spika Anne Makinda, alisema idara ya utawala italishughulikia jambo hilo.
Naye Mbunge wa Mbinga Mashariki (CCM) Gaudence Kayombo, aliomba mwongozo akitaka Bunge liahirishe kujadili hoja ya dharura.
Alisema wakulima wa Nyanda za Juu Kusini wamelima mahindi mengi na serikali imekuwa ikununua, lakini Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, ameandika waraka akiagiza mahindi hayo yasinunuliwe tena wakati wakulima wameshakodisha magari kutoka umbali wa kilometa 50 kwa ajili ya kupeleka mahindi katika maghala hayo.
Alisema muda mfupi ujao wizara hiyo itapeleka pembejeo za ruzuku na kutokana na hali hiyo wakulima hawatakuwa na fedha hivyo kushindwa kuzinunua.
Akijibu mwongozo huo, Spika Makinda, alisema ni kweli mambo hayo yamejitokeza na kutaka ofisi ya Waziri Mkuu kulishughulikia jambo hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: