Ni mkanganyiko juu ya uhalali wa mchakato wa katiba
Yaelezwa unavyoendela sasa unavunja katiba iliyipo
Yaelezwa unavyoendela sasa unavunja katiba iliyipo
Kutokana na hoja za Kamati hiyo iliyokutana mwishoni mwa wiki, serikali kupitia kwa Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema,
wanatakiwa kufika mbele ya kamati kuzungumzia uhalali wa mchakato huo.Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Kamati viliiambia NIPASHE kuwa hali ya kutaka maelezo ilifikiwa na Kamati baada mjumbe mmojawapo, Christopher ole Sendeka, (Simanjiro- CCM), kumuuliza mtoa mada katika kikao cha mwishoni mwa wiki kama mchakato wa sasa una uhalali wowote kwa kuwa hadi sasa hakuna ibara ya katiba inayoruhusu kuanzishwa kwa mjadala wa kuivunja katiba ya sasa.
Mtoa taarifa wetu alisema kuwa Sendeka alitaka kujua kama njia ya kuanzisha mchakato huo hauvunji katiba, kwa sababu kimsingi hakuna ibara yoyote ya katiba ya sasa inayoruhusu kujadili kifo cha katiba yenyewe kwa kuwa wote walioko madarakani walikula kiapo cha kuilinda.
“Ndugu mwenyekiti, naomba niseme tu wenzetu wa Kenya wakati wanaanzisha utaratibu wa kuandika katiba mpya, walifanya mambo mawili kwa pamoja, kwanza waliwasilisha muswada wa marekebisho ya katiba iliyokuwapo kwa kuweka kifungu cha kuruhusu kuiua, lakini wakati huo huo wakiwasilisha muswada wa kuanzisha kwa mchakato wa katiba mpya kama tunavyotaka kufanya sisi,” chanzo chetu kilimkariri Sendeka.
Habari zinasema kuwa mtoa mada katika semina, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, James Jesse, naye alikubaliana na hoja ya Sendeka, kiasi cha kufikiwa kwa maamuzi ya kusikia upande wa serikali juu ya hatari ya mchakato wa katiba mpya kuwa batili.
Sendeka ni mjumbe mpya kwenye kamati hiyo akiwa ameongezwa na Spika sambamba na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF) na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
Wabunge hao wameongezwa ili kuiongezea nguvu kamati hiyo kutokana na uzito wa muswada wa katiba. Kadhalika, wajumbe waliohoji uhalali wa wabunge wa sasa wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na wengine watakaoteuliwa kama watakuwa na uhalali kuwa Bunge la Katiba.
Hoja hilo iliibuliwa kwa sababu Katiba ya Tanzania ibara ya Ibara ya 8 (1) (a) inaeleza wazi kuwa chimbuko la mamlaka yote ni wananchi, na kwa maana hiyo hakuna mwenye uwezo wala mamlaka ya kuaamua vinginevyo isipokuwa wananchi.
Kwa maana hiyo, hoja ilitolewa kwamba wabunge na wawakilishi wa sasa hawakuchaguliwa kwa ajili ya kuunda Bunge la Katiba, ila walichaguliwa kwa majukumu mahusi ya kawaida ya ubunge, kwa maana hiyo kama kuna haja ya kuundwa kwa Bunge la Katiba mamlaka hayo ni ya wananchi na ni lazima wananchi waamue nani aingie kwenye Bunge hilo na si uteuzi.
“Inavyoelekea ni kama Bunge la Katiba litakuwa limeteuliwa na Rais, hii ni kinyume cha chimbuko la mamlaka yote ya nchi,” chanzo chetu kilidokeza kuhusu mjadala wa juzi ambao ulikuwa mkali na wenye hoja nzito za kisheria hasa kutoka na utaratibu ambao kamati hiyo imaanzisha wa kukaribisha marafiki wa kamati ambao ni watu wenye taaluma ya sheria hususan mambo ya katiba ili kuisaidia katika kazi zake.
Mtoa taarifa wetu alisema kwa mujibu wa marafiki wa kamati ambao wamekwisha kutoa mada kwa kamati hiyo, kuna uwezekano rais yeyote kwenda mahakamani na kuwasilisha hoja kwamba katiba inavynjwa, na mahakama itamsikiliza.
“Lakini si hilo tu, ilionekana wazi kwamba nchakato huu unaweza kufika mwisho, lakini ukadhihirika kuwa ni batili. Hatujua, labda kuna tatizo la kisiasa na kisheria, wale wanaomshauri Rais badala ya kuichukua nia yake njema ya kuanzisha mchakato wa kwa kuuweka katika msingi ya kisheria wao, wanajipendekeza kwake au hawajui wafanyalo,” alisema.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, alisema Katiba ya sasa haina kipengele kinachoruhusu kuandika mpya na badala yake, Ibara ya 98 imeweka sharti la kuifanyia marekebisho.
Lissu ambaye kitaaluma ni Mwanasheria, alisema ili kuondoa mgongano wa kuvunja Katiba iliyopo, Bunge linapaswa kuifanyia marekebisho ambayo yangeruhusu kuandika mpya. Akieleza kasoro za muswada wa Katiba, alisema kumpa mamlaka ya kura ya turufu Rais wa Zanzibar, ya ama kupinga au kukubali kuandikwa kwa Katiba ni kuvunja iliyopo ambayo inaeleza kwamba kiongozi huyo hana mamlaka ya masuala ya Muungano katika Tanzania Bara.
Kadhalika, alisema kuna vifungu vinavyowapa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kushiriki kwenye uandikaji wa Katiba ya Jamhuri ni kinyume cha iliyopo ambayo imewazuia kufanya hivyo.
Hata hivyo, NIPASHE ilipomtafuta Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, hakukubali wala kupinga hoja hizo na badala yake alisema kwa ufupi “siwezi kusema chochote kwa sababu watu wanazungumza tu bila kusoma na kuielewa Katiba wala muswada.”
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alikataa kuzungumzia hoja hiyo na kutaga gazeti hili kuwasiliana na Spika wa Bunge, kwa maelezo kwamba ameshakabidhiwa muswada tayari kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni kwenye Mkutano unaoanza kesho.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake