CUF nao watishia kuandamana
Pinda asema ni kero, ataka mwafaka
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amesema mtindo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kufanya maandamano kila mahali umekuwa ukiipa tabu serikali kwa kushindwa kufanya kazi nyingine zinazohitajika na badala yake kukaa kufikiria maandamano hayo.
Pinda asema ni kero, ataka mwafaka
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amesema mtindo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kufanya maandamano kila mahali umekuwa ukiipa tabu serikali kwa kushindwa kufanya kazi nyingine zinazohitajika na badala yake kukaa kufikiria maandamano hayo.
Aliyasema hayo bungeni jana wakati akijibu maswali ya
papo kwa papo ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.Akiuliza swali la nyongeza, Mnyika alisema hivi sasa suala la mgogoro wa Umeya wa Jiji la Arusha Mjini, limevuka mipaka ya kivyama na limekuwa la kitaifa na kisha kusambaa maeneo mbalimbali ya nchi.
Alihoji kama yupo tayari kutoa maelekezo mengine ama ushauri mwingine ili upande wa pili ujue hatma ya suala hilo na ujue hatua gani za kuchukua.
Akijibu swali hilo, Pinda alimtaka Mnyika kutokuza jambo hilo na kwamba hakuna ukweli kwamba limesambaa nchi nzima.
“Style (mtindo) yenu ya maandamano kila mahali sisi tulioko serikalini tunapata taabu sana, tunataka kufanya kazi nyingine ambazo zinahitajika lakini muda wote unakaa unafikiria maandamano, tuteremke chini kidogo tuanze kuona maslahi mapana ya nchi, tuone ni mambo gani ya msingi yanahitajika, kwa pamoja tuweze kwenda mbele.”
Pinda alisema uanaharakati unampa tabu lakini kama umakini utakuwepo, yeye haoni tatizo watu kukaa na kuzungumza suala hilo.
“Katika hali ninayoiona mimi, `peoples power' (nguvu ya umma) kila kukicha, haiwezekani ni changamoto kwenu na CCM, ili kuona hali inapokuwa hivyo unafanyaje. Tunahitaji kubadilika kidogo ili na sisi muweze kutupa imani kwamba chama hiki makini sasa kipo tayari kutatua tatizo,” alisema.
Katika swali lake la msingi Mnyika, alisema Pinda aliahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la mgogoro wa umeya Arusha, lakini maelekezo aliyoyatoa kwa barua kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, hayajatekelezwa kwa kiwango cha kutosha na upande wa pili.
“Hali hiyo imesababisha matatizo ya Arusha kuendelea hadi hivi sasa, sote tunaheshimu mahakama lakini matukio ya Arusha ni pamoja na Mkuu wa Mkoa kuingilia kazi za mahakama, ningependa kupata kauli kutoka kwako,” alisema.
Aidha, alisema kuwa viongozi wa Jeshi la Polisi juzi usiku walikubaliana na viongozi wa kitaifa wa chama kwa lengo la kukaa mezani.
Alihoji iwapo Pinda yupo tayari kuongeza nguvu katika majadiliano hayo ili kunusuru hali hiyo iliyosambaa nchi nzima ya udhalilishaji na uvunjaji wa haki za msingi.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema, “Mnyika anazo taarifa ambazo mimi kwa bahati mbaya sina kwamba viongozi mkoani wamekubaliana na wa taifa. Sina la kusema kwa hilo lakini kwa upande wa pili ni kweli nilichofanya nilidhani kingepelekea kupata ufumbuzi wa tatizo la Arusha.”
Alisema tatizo hilo si la kiserikali bali sehemu kubwa ni la kichama na kwamba amemweleza Msajili wa Vyama vya Siasa, kuwasiliana na vyama hivyo ili waone mgogoro upo katika sura gani ili wakutane na kupata suluhu la kisiasa.
Alisema ameona nakala ya barua ya CCM kwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ikieleza kuwa katika hilo hawaoni la kuzungumza lakini kama kuna maeneo Chadema inaona yapo ya kuzungumza yawasilishwe, yaelezwe ili waone pa kuanzia.
Wakati huo huo, Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani, alihoji sababu gani zilizosababisha serikali kumnyima dhamana Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.
Alisema Tanzania imekuwa ikiheshimika duniani kwa amani lakini ameshangaa kila siku akisikia mgogoro Arusha.
“Sasa hivi utalii na biashara za wananchi Arusha zimeharibika na inasemekana serikali yako ndiyo inazuia kumtoa mbunge wa Arusha Mjini (Godbless Lema), je ni sababu gani inasababisha suala hilo?” Alihoji Ngonyani maarufu kama Profesa Maji Marefu.
Akijibu maswali hayo Pinda alikiri kuwa Arusha kuna migogoro mingi ambayo imeingiliana lakini anaamini kuwa mji huo bado ni tulivu.
Wakati Pinda akieleza hayo, jijini Dar es Salaam, Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walitanda katika eneo la Kimara na kufanya doria, kwa ajili ya kuwatawanya wafuasi wa Chadema.
Askari hao ambao walifurika mapema jana alfajiri, walikuwa kwenye magari manne wakiwa wamevalia mavazi maalum ya kujikinga na mashambulizi, huku wakiwa wamebeba silaha mbalimbali, yakiwemo mabomu ya machozi.
Mfuasi mmoja wa Chadema aliliambia NIPASHE kwamba, aliwasili eneo la Kimara Kona, kwa ajili ya kuanza maandamano yaliyolenga kupinga unyanyasaji wa Polisi dhidi ya chama hicho na kuwakuta askari wa FFU.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Chadema, Mwita Waitara, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wameamua kuyasitisha maandamano hayo kwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, yupo katika mazungumzo na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI).
"Sisi tumeyasitisha kwa sababu Mwenyekiti wetu yupo kwenye mazungumzo na DCI, sio kwamba polisi wametuzuia…tupo tayari kwa lolote na endapo mazungumzo yao hayatakuwa na haki, ni lazima tuandamane nchi nzima,” alisema.
FFU walifanyakazi ya ziada kwa kuwa walikuwa wakitawanya kikundi chochote cha watu hata watatu, walioonekana kwenye eneo hilo kwa kuwataka waondoke mmoja mmoja.
Alieleza kushangazwa na idadi kubwa ya FFU waliotanda kuzima maandamano hayo, “utadhani wanawawinda wahalifu.”
Alisema leo watakuwa na kikao ambacho kitawakutanisha wanachama wote, kwa nia ya kujadili yaliyofikiwa kwenye kikao baina ya Mbowe na DCI.
CUF WAMLAANI CHAGONJA
Chama Cha Wananchi (CUF), kimelaani vikali amri ya kusitisha maandamano ya amani nchini kote kwa muda usiojulikana, iliyotolewa na Jeshi la polisi na kutaka amri hiyo iondolewe mara moja ili kurudisha imani kwa jeshi hilo.
Amri hiyo ilitolewa juzi na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jashi hilo, Paul Chagonja.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa amri hiyo ya polisi iliyoambatana na kuwatisha wananchi, ni pigo kubwa kwa demokrasia nchini.
Mtatiro alisema amri hiyo ni pigo kwa vile si tu kwamba, inapingana na Katiba ya nchi, ambayo inatamka wazi katika Ibara ya 20 kuwa wananchi wanayo haki ya kukutana kwa hiari, kuchanganyika na kutoa mawazo yao hadharani, bali inapingana na mikataba mbalimbali ya Kimataifa, ambayo Tanzania imeridhia, kama vile Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) juu ya haki za kiraia na kisiasa wa Machi 23, mwaka 1976.
“Tamko la Jeshi la Polisi linalenga katika kukuza matatizo madogo madogo ya kisiasa na kuyafanya kuwa makubwa na kuitumbukiza nchi katika machafuko kama yale yaliyowahi kutokea Januari 26 na 27 mwaka 2001 dhidi ya wanachama wa CUF na Watanzania wapenda mabadiliko,” alisema Mtatiro.
Aliongeza: “Kwa maana hiyo, CUF inapendekeza amri iliyotolewa ya kusitisha maandamano ya amani iondolewe ili kurudisha imani kwa Jeshi la Polisi.”
Pia anataka vyama vya siasa, ikiwamo CUF viendelee na utaratibu wa kutoa taarifa ya kufanya maandamano na kuitisha mikutano ya hadhara kama utaratibu ulivyowekwa katika Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi, Sura ya 322 kama ilivyoandikwa upya mwaka 2002.
Aliwahakikishia Watanzania kuwa chama chake kitaendelea na programu zake za kisiasa kama zilivyopangwa na kinaungana na Watanzania wapenda amani kuwa kitaendelea na mikutano yake na shughuli nyingine za kisiasa kwa weledi mkubwa na kwa kuzingatia sheria za nchi.
Hivi sasa wamewatuma makada wake katika mikoa sita ya Tanzania Bara kwenda kufanya mikutano ya hadhara na shughuli nyingine za kisiasa; ukiwamo mkoa wa Mtwara, Lindi, Mwanza, Tabora, Kagera na Tanga.
Imeandikwa na Sharon Sauwa (Dodoma), Beatrice Shayo, Muhibu Said na Samson Fridolin (Dar).
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment