Wednesday, November 16, 2011

Ngono ni kipimo cha huba?

RAFIKI ni siku nyingine tunakutana katika uwanja wetu wa kupeana darasa juu ya maisha yetu ya uhusiano.
Bila shaka utakuwa mzima wa afya njema na unaendelea na majukumu yako salama. Ukiwa mdau wa kona hii, huna cha kupoteza, utaongeza ujuzi wako kila kukicha.

Mapenzi hayatakutesa kama ukisoma na kuyashika yanayoandikwa hapa. Hata hivyo, unao uhuru wa kusoma na kuchagua cha kushika; si lazima kila kilichoandikwa ukifuate.


Leo nataka kuzungumzia jambo moja la msingi ambalo limekuwa likiwatatiza sana hasa dada zetu, suala la kukutana faragha na wenzi, hasa wapya. Jambo hili huzua mjadala mkubwa sana.

Wanaume wengi wanatumia kigezo hiki kama kuthibitisha au kudhihirisha mapenzi ya dhati. Utamsikia mwingine anasema: “Sasa kama hutaki kufanya mapenzi na mimi, utakuwa hunipendi.”

Kwa sababu wanawake nao wanaogopa kuachwa au wanatamani ndoa, kwa kuamini kwamba tendo hilo ni kila kitu wanajikuta wakikubali; sasa hapo inategemea, mwisho unaweza kuwa mzuri au mbaya!

Nakumbuka hii mada niliwahi kuifafanua huko nyuma ingawa kwa juu juu, lakini kutokana na maswali ambayo nimeulizwa wiki hii, nalazimika kuinyambulisha kwa mapana zaidi.

Wapo wasomaji watatu, kwa nyakati tofauti walipata kuniuliza maswali ambayo yanafanana. Hebu twende ukaone maswali yao, halafu turudi kwenye mada yenyewe. Dawa itapatikana hapa
leo rafiki.

KUTOKA TEMEKE
Hello brother Joseph! Hongera kwa kazi yako ya kuelimisha jamii hasa sisi vijana. Mimi ni mfuatiliaji mkubwa sana wa kazi zako, zinanielimisha sana.

I’m a girl of 22 yrs, elimu yangu ni form six, najiandaa kwenda chuo mwakani, kwa sababu mwaka huu nilichelewa. Nina mpenzi wangu ambaye yupo chuo mwaka wa pili Mzumbe, Morogoro.

Tuna uhusiano kwa miaka miwili sasa lakini hatujawahi kukutana kimwili hata siku moja. Mimi ni bikra na nimeshamwambia juu ya jambo hilo.
mwanzoni alikubaliana na mimi kwamba atasubiri, lakini siku hizi ananisumbua sana akitaka penzi langu.

Nimemwambia asubiri mpaka ndoa, amesema tutafunga mpaka atakapomaliza chuo lakini kwa sasa tuwe tunakutana faragha.

Nampenda sana na sitaki kumpoteza, nifanyeje? Nikubali au nikatae? PLEASE HELP ME!

KUTOKA DODOMA
Hongera kwa kazi zako, leo nami nimeona nijitokeze kuuliza jambo ambalo linanisumbua kwa muda mrefu. Mimi ni msichana mwenye miaka 21, ni mwanachuo wa chuo kimoja hapa Dodoma. Nyumbani kwetu ni Dar.

Ninaye mpenzi wangu, nimekuwa naye kwa muda mrefu sana, lakini tulikubaliana kwamba hatutafanya mapenzi mpaka tutakapofunga ndoa, lakini siku hizi amenibadilikia. Anasema eti nina wanaume wengine ndiyo maana namkataa.

Nampenda sana, lakini naogopa kupoteza usichana wangu kabla ya ndoa. Lakini kubwa zaidi ninalowaza, itakuwaje kama hatanioa wakati atakuwa ameshanipotezea usichana wangu? Hapo ndipo ninapochanganyikiwa kabisa.

Naomba msaada wako kaka’ngu, nipo njia panda. Nashindwa hata kuhudhuria baadhi ya vipindi kutokana na stress. Nasubiri msaada wako.

KUTOKA MOROGORO
Habari uncle Shaluwa. Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 26, nina mtoto mmoja, lakini mwanaume niliyezaa naye tumeachana. Kuna mtu amejitokeza, anasema ananipenda na anapenda anioe.

Nimeshamweleza kila kitu kuhusu historia yangu. Kiukweli nawaogopa sana wanaume na sipo tayari kuuacha mwili wangu uchezewe tena. Huyu jamaa ananing’ang’aniza sana mapenzi, yaani mpaka nachanganyikiwa.

Anasema kama sitaki, inamaana kwamba simpendi. Je, nifanyeje kaka yangu? Kumpenda nampenda, ndoa pia naitaka. Naomba unisaidie jamani.

MMEONA EEH?
Rafiki nadhani umeona hali halisi ilivyo.

Hawa wadada nilimalizana nao vizuri, niliwapa elimu ambayo bila shaka itakuwa imewasaidia kwa kiasi kikubwa sana.

Hata hivyo, kichwani mwangu niliamini wapo wengine wengi wenye shida kama yao.

Wapo ambao wanakutana na changamoto hii lakini wanashindwa mahali pa kuanzia.

Je, ni kweli tendo hilo humaanisha penzi la dhati? Twende tukaone hapa chini.

MAPENZI NI NINI HASA?
Kila mmoja anaweza kuwa na maana yake, lakini kimsingi mapenzi hayana maana ya moja kwa moja! Kwa ujumla mapenzi ni hisia zenye msisimko wa pendo la dhati zinazotoka moyoni mwa mmoja kwenda kwa mwingine.

Pendo hukamilika ikiwa wawili hao kwa wakati mmoja watahisi hisia hizo, ingawa wakati mwingine mmoja ndiyo huwa wa kwanza kuanza kuhisi hisia hizo.

Tafsiri hii nimewahi kuitaja mara kadhaa katika makala zangu, kama wewe ni mdau wa kona hii utakuwa unakumbuka, kama ndiyo kwanza unasoma hapa, basi si vibaya maana utakuwa umeingiza kitu kichwani mwako.

Wakati mwingine inawezekana mkajikuta mmependana tangu siku ya kwanza tu mlipokutana, lakini wengine huchukua muda mrefu kidogo kabla hisia hizo hazijachukua nafasi sawasawa. Wapo wanaofikiria mapenzi ni ngono au ngono ni sehemu ya mapenzi.

Hawa nitapingana napo kwa nguvu zangu zote.

Kwa nini? Wiki ijayo tutazungumza, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni mshauri wa mambo ya mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Lets Talk About Love vilivyopo mitaani.  

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake