ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, November 22, 2011
Rais Kikwete akubali kukutana na Chadema
Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amekubali kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa Chadema kusikiliza madai yao juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011, uliopitishwa bungeni juma lililopita.Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu jana jioni ilieleza kuwa Rais amelipokea ombi hilo kwa furaha kwa sababu ni jambo jema.
“Kufuatia kukubali kwake ombi hilo, Rais ameagiza mawasiliano yafanyike ili kupanga tarehe mwafaka ya kukutana na viongozi hao wa Chadema na kuzungumzia suala hilo,” ilieleza taarifa hiyo.
Kabla ya Kurugenzi hiyo kutoa taarifa hiyo, Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Premi Kibanga akizungumza na gazeti dada la hili, The Citizen alisema Rais amepokea jambo hilo kwa furaha.
“Tumepokea barua ya Chadema muda mfupi uliopita (jana jioni), ikiomba kukutana na Rais Kikwete na bahati njema Rais pia amependekeza kuwa yuko tayari kukutana na viongozi kutoka vyama vya siasa,” alisema Kibanga.
Uamuzi huo wa Rais umekuja siku moja baada ya Chadema kuunda kamati ndogo ya watu sita kwa ajili ya kuonana na Rais Kikwete na kuwasilisha madai yake juu ya muswada huo wa sheria.
Kamati hiyo iliyoundwa katika mkutano wa dharura wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, inataka kujadiliana na Rais kuhusu kile ilichoeleza kuwa ni upungufu uliopo katika muswada huo uliopitishwa na Bunge na kutaka Rais atafakari kama ausaini kuwa sheria au la.
Akisoma tamko hilo kwa vyombo vya habari katika mkutano uliofanyika makao makuu ya chama hicho, Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kamati hiyo ya watu sita, ilikuwa ikifanya taratibu za kumuona Rais Kikwete.
Mbowe alisema ushiriki wa Chadema katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya utategemea mazungumzo hayo baina ya wajumbe wa kamati ya chama chake na Rais Kikwete.
Ijumaa iliyopita, Rais Kikwete akizungumza na wazee wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu uchumi na mchakato wa Katiba, alisema atautia saini kuwa sheria muswada huo licha ya kelele za wanasiasa za kuupinga.
Alitoa kauli hiyo huku akipangua hoja zote kuhusu mchakato huo zilizokuwa zikitolewa na Chadema kuwa muswada huo haukuzingatia kanuni zitakazowezesha demokrasia.
Kauli hiyo ya Rais ilikuja saa chache baada ya Bunge kupitisha muswada wa mabadiliko ya Katiba ambao ulisusiwa na wabunge wa Chadema na NCCR-Mageuzi kwa madai kuwa mchakato mzima una kasoro.
Kamati Kuu CCM bado siri nzito
Huko Dodoma, ajenda kuhusu Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ilijitokeza kwa sura isiyo rasmi wakati Kamati Kuu (CC), ilipokuwa ikijadili taarifa ya uchaguzi mdogo wa Igunga iliyowasilishwa na aliyekuwa Kiongozi wa Kampeni za CCM, Mwigulu Nchemba lakini haikudumu.
Habari kutoka katika kikao hicho zinasema mmoja wa wajumbe wa CC ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi akichangia hoja ya uchaguzi wa Igunga alisema hali ya vijana wa jimbo hilo na kwingineko nchini kukichukia CCM ni kutokana na Umoja wa vijana kutotekeleza wajibu wake, badala yake kujishughulisha na mambo mengine yasiyokuwa na tija.
Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Isimani, Iringa alinukuliwa akitoa kauli hiyo baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira kusema kuwa tatizo katika uchaguzi mdogo wa Igunga walikuwa ni vijana wengi ambao walionyesha chuki kwa CCM wakati wa uchaguzi huo, wakidai kutoshughulikiwa kwa matatizo yao.
Uchaguzi Igunga
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa katika siku ya kwanza ya kikao chake juzi, CC ilipokea taarifa ya uchaguzi mdogo wa Igunga ambao ulimwingiza bungeni, Dk Dalaly Kafumu.
Ripoti ya Igunga iliyowasilishwa na Nchemba iliweka bayana kwamba hali katika uchaguzi huo ilikuwa mbaya kiasi cha kuwepo kwa hofu ya CCM kushindwa uchaguzi.
Nchemba alinukuliwa akieleza mitafaruku kadhaa iliyotokea wakati wa kampeni kiasi cha kuwafanya madiwani wa CCM Igunga kutishia kujitoa katika chama na kuingia upinzani, lakini akasema suala hilo lilimalizwa kwa kutumia busara, hatua iliyokiwezesha kupata ushindi.
Baada ya taarifa ya Mwigulu, Mwenyekiti wa kikao hicho, Rais KIkwete anadaiwa kwamba alihoji ukweli wa taarifa za baadhi ya makada wa chama hicho kuwapigia kampeni wapinzani kwa kutumia kauli mbiu ya “Tushindwe ili tuheshimiane”, swali ambalo hata hivyo, halikupata majibu kutokana na wajumbe kukaa kimya.
“Mwenyekiti aliuliza tena kwamba kuna watu waliompigia simu na kumtumia meseji (ujumbe mfupi wa simu wa maandishi), kwamba kuna makada waliokuwa wakiwapigia kampeni Chadema, lakini wote walikaa kimya na ndipo aliposema kwamba tuache majungu na fitina,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya mkutano huo.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment