ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 21, 2011

Umma wataka serikali iwashughulikie Luhanjo na Jairo



Wanasiasa, wasomi na wanaharakati wameunga mkono mapendekezo ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya  kuitaka serikali kuwawajibisha viongozi wake wandamizi kwa kutumia ofisi vibaya.
Juzi wabunge hao walitoa mapendekeza hayo baada ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la rushwa dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo kuwasilisha  ripoti yake bungeni.
Wabunge hao walipendekeza mamlaka zinazohusika  kuwatimua kazi, Jairo na Katibu Mkuu Kiongozi (Ikulu), Philimon Luhanjo.

Viongozi wengine waliotakiwa kuchukuliwa hatua ni pamoja na Waziri wa  Wizara ya Nishati na Madini, William Ngeleja, Naibu wake, Adam Kigoma Malima  na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.


Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti jana, wasomi, wanaharakati na wanasiasa walisema wana imani kwamba serikali itachukua hatua dhidi ya viongozi hao na kuwataka wananchi wawe na subira.

Mhadhiri wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Palamagamba, alisema Bunge lina mamlaka kamili na kwamba maazimio yake ana imani mapendekezo hayo yatafanyiwa kazi.

Hata hivyo, Profesa Kabudi alisema hawezi kutabiri kama mapendekezo hayo yatafanyiwa kazi au la lakini na kutaka kazi hiyo iachwe ibaki kwa mamlaka husika.

"Mapendekezo yatazaa matunda au hayatazaa siwezi kutabiri cha msingi ni taasisi za Mahakama na Bunge ziiimarishwe zaidi ili ziweze kufanya kazi vizuri na mwisho wa siku mambo yote yatakwenda vizuri," alisema  

Alitoa mfano wa nchi za Italia na Japan kuwa zinakumbwa na misukosuko mingi kama ambayo imetokea  nchini kwa viongozi wa serikali kukumbwa na kashfa, lakini  zinaweza kuvuka vikwazo hivyo kutokana na kuwa na taasisi imara ambazo zinafanya kazi kwa kujitegemea na kwa kufuata sheria.

Alilipongeza Bunge kwa kufikia hatua hiyo na kusema kuwa chombo hicho kina mamlaka ya kisheria kuisimamia serikali na ndicho kilichofanyika. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya, alisema ana imani kwamba hatua sahihi zitachukuliwa na kuwataka wananchi wawe na subira.

Nkya alisema ni mapema  kuanza kutabiri ama kuhoji kama serikali inaweza kuwachukulia hatua wote waliotajwa katika ripoti hiyo na mapendekezo ya wabunge.

"Tusubiri tuone kama mamlaka ambazo viongozi hao wapo chini yake zitawachukulia hatua na tujipe muda mpaka mkutano mwingine wa Bunge utakapokaa Januari mwakani kama tukiona hakuna hatua zozote ndipo tuanze kusema," alisisitiza. 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba alisema hana imani kama serikali itachukua hatua kama ilivyopendekezwa na wabunge na kamati hiyo teule lakini na kwamba yeye na wanaharakati wengine wanajipa muda ili kuona kitakachoendelea.

Bisimba alisema muda utakapofika baada ya kuona hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na serikali wao watasimama na kutoa tamko lao.

Alisema anakosa imani kwa serikali kwa sababu kabla Bunge halijaunda Kamati Teule kuchunguza sakata la Jairo, Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo aliwahi kumsafisha Jairo dhidi ya tuhuma zilizokuwa zinamkabili.

Aliitahadharisha serikali kuacha utaratibu wa kuwahamisha wizara na idara   watumishi wake wanaokumbwa na kashfa ama vitendo vingine vya utovu wa nidhamu.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye alisema yeye sio mpiga ramli kujua kama serikali itachukua hatua kwa kuwa bado ni mapema.

Hata hivyo, alisema ana imani kuwa hatua zinazostahili zitachukuliwa dhidi ya wote waliotajwa kuhusika na sakata hilo.

"Mimi sio mganga wa kienyeji nijue dhamira ya serikali kama itawachukulia hatua watu hao au la cha msingi ni kusubiri na kuzipa mamlaka muda kwa kuwa tukio lenyewe limetokea jana (juzi)," alisema Nape.

Aliwataka waandishi wa habari kuwa wazalendo na wavumilivu yanapotokea masuala mazito kama hayo na kuiachia serikali ifanye kazi yake.
CHANZO: NIPASHE

No comments: