
Mary Mahundi
VIJANA wa Chama cha Wananchi (CUF), leo wanatarajia kuanzisha kampeni ya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama hicho kwa kile wanachoeleza baadhi ya viongozi wameshindwa kutekeleza wajibu wao. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya vijana hao kulituhumu Baraza Kuu la CUF lililofanyika Dar es Salaam juzi na jana, kuwa limeshindwa kufanya uamuzi mgumu kuhusu waliosababisha chama kufanya vibaya kwenye uchaguzi mkuu mwaka jana na ule mdogo wa Igunga.
Kutokana na hali hiyo, Katibu wa Vijana CUF Wilaya ya Kinondoni, Abdallah Mohamed, alisema leo wameandaa kongamano la vijana kutoka Tanzania bara na visiwani ili kuweka msimamo wao. “Wanachama hatufurahishwi na matokeo ya uchaguzi uliofanyika
.Tunahisi mipango mibovu ya chama ndiyo kikwazo, sasa viongozi tunataka watueleze,” alisema Mohamed. Alilalamika kuwa Baraza Kuu limeshindwa kuchukua hatua mwafaka kutokana na matokeo mabaya ya uchaguzi wa rais uliofanyika Oktoba 30, mwaka jana na uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyiwa Oktoba 2, mwaka huu. "Baraza lifanye uamuzi mgumu kuhusu hali ya kisiasa ya chama chetu kufanya vibaya kwenye uchaguzi,” alisema.
Pia, Mohamed alisema chama kilitelekeza makundi ya vijana na wanawake, hali iliyopelekea uhamasishaji kukosekana wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi. “Viongozi wetu waangalie suala hili kwa umakini juu ya kukijenga chama chetu, pia vijana wenzangu wasiwe misukule (kutumiwa) kusifia viongozi badala ya kutoa changamoto,” alisema Mohamed.
Mohamed alisema wakati baraza la chama lilimaliza vikao vyake jana, wanachana na vijana walisubiri kauli na maazimio ambayo yalitegemewa kuwa ya faraja kwa chama hicho, lakini imekuwa kinyume. Alisema baadhi ya viongozi wa kitaifa wa chama hicho wameshindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo, ndiyo sababu chama kimepoteza mwelekeo hasa Tanzania bara.
Alitaja miongoni mwa viongozi wa kitaifa wanaotarajia kuhudhuria kongamano hilo, kuwa ni Manaibu Katibu Mkuu bara na visiwani, Julius Mtatiro na Ismail Jussa. Mohamed alisema viongozi hao wanatarajia kuwekwa kitimoto na vijana na wakishindwa kutoa maelezo ya kuridhisha, watachukua jukumu la kuweka mkakati wa uvuaji gamba kwa baadhi ya viongozi ndani ya chama. Mtatiro alikiri kuwa na taarifa kongamano hilo, huku Jussa alikataa kupata taarifa hizo ingawa kwa muda mrefu alikuwa Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment