Idadi ya watu wanaoshikiliwa jijini Mbeya kutokana na vurugu za wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga na Polisi, zilizodumu kwa siku mbili mfululizo kuanzia Ijumaa iliyopita, imeongezeka kutoka 235 hadi 300, kutokana na operesheni ambayo iliendelea juzi na jana.
Idadi hiyo imeongezeka hata baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Mr. Sugu), alipozungumza na wananchi kwenye viwanja vya kituo cha mabasi Kabwe, ambapo aliwashauri viongozi wasichukulie vurugu hizo kama mambo ya siasa na kwamba vurugu za wamachinga zinatakiwa zishughulikiwe kisayansi na siyo kutumia mabavu.
Hata hivyo, kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Itende kimelaumiwa na wananchi wa Jiji la Mbeya kutokana na hatua ya askari wake kutembeza mkong’oto hovyo kwa wananchi na kuwapora simu mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Mbunge Mr. Sugu.
Askari hao wa JKT walitembeza kipigo kwa wananchi hovyo, wakiwemo waandishi wa habari muda mfupi baada ya Mr. Sugu kumaliza kuwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara Jumamosi iliyopita.
Waandishi wa habari waliopata kipigo kutoka kwa askari hao wa JKT, walikuwa wakitekeleza majukumu yao na ndipo askari hao walipowavamia na kuanza kuwapiga kwa marungu na mikanda, ambapo mmoja wa wanahabari aliporwa simu yake ya mkononi na kuchaniwa suti yake na askari hao.
Wakati wakiendelea kuwashambulia wanahabari hao ambao walijitetea kwamba ni waandishi kwa kuwaonyesha vitambulisho vyao vya kazi, askari hao wa JKT walionwa na wakubwa zao na kuwasihi waache kuwashambulia ambapo mwanahabari aliyeporwa simu aliomba arudishiwe simu yake na ndipo askari mmoja aliyeichukua aliamua kuirejeshe baada ya kukemewa.
Hata hivyo, pamoja na hali hiyo kujitokeza, Jiji la Mbeya ambalo kwa takribani siku tatu lilikumbwa na vurugu kubwa baada ya kutokea mapambano kati ya wamachinga na polisi, limeanza kurudi katika hali ya utulivu na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kujitafutia riziki ambapo maduka na mabenki yaliyokuwa yamefungwa sasa yamefunguliwa.
Maeneo ya Mwanjelwa, Soweto, Sai na Uyole, ambayo ndiyo yalikumbwa na vurugu hizo hivi sasa wananchi wameanza kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Anaclet Malindisa, alisema wananchi hao wanaoshikiliwa wataanza kuachiwa leo na kwamba wengine 17, waliojeruhiwa kwenye vurugu hizo wanaendelea vizuri.
Kutulia kwa vurugu hizo kumefanikishwa na Mr. Sugu kuwasili jijini hapa na kuwataka wamachinga watulie na kuwaahidi kuyafanyia kazi madai yao kwa viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya. Wananchi jijini Mbeya wamewatahadharisha viongozi wa serikali kuacha kuhusisha vurugu hizo kwamba zilipangwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kwamba kama wanataka kusaidia kukomesha vurugu hizo katika siku za mbeleni njia ni kuhakikisha wanakaa na wamachinga kuyamaliza madai yao mezani badala ya kutumia mabavu.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, akizungumza na waandishi wa habari juzi, alisema vurugu hizo zina mwingiliano na siasa kwani bendera za Chama cha Mapinduzi (CCM) zilichomwa moto huku za Chadema zikiendelea kupepea mitaani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake