
Frederick Katulanda, Mwanza
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe ameishauri Serikali kuhakikisha inajenga uwezo wa ndani kutibu magonjwa ambayo teknolojia yake inawezekana badala ya kuwapeleka viongozi wake nje ya nchi kwa matibabu.
Zitto ambaye anafanyiwa upasuaji wa kichwa na madaktari wa Hospitali ya Apollo iliyopo Bangalore, India alitoa kauli hiyo jana kwa njia ya Mtandao.
Alisema kufika kwake India kwa matibabu ameweza kubaini kuwa Serikali ya Tanzania imekuwa ikigharamia matibabu ya zaidi ya Watanzania 800 kila mwaka nchini India kwa ajili ya matibabu mbalimbali ambayo hayapatikani nyumbani na kwamba nusu ya wagonjwa hao ni watoto wenye matatizo ya moyo.
Alisema tofauti na dhana inayojengeka kwa kasi kubwa, amegundua kuwa watu wengi ambao wamekuwa wakipelekwa India kwa matibabu ni Watanzania wasio na nyadhifa za kisiasa kama alivyoweza kujionea mwenyewe.
Alisema akiwa wadini mwake jana alipata bahati ya kutembelewa na wananchi wa kawaida ambao wako hospitalini hapo kwa matibabu mbalimbali na kubainisha kuwa Watanzania hao ni wanawake wanaotoka Wilaya za Hai na Moshi mkoani Kilimanjaro.
“Hawa ni wananchi wa kawaida kabisa na mmoja mama Modesta Mmari ni Mfanyakazi wa Hospitali ya KCMC Moshi, Mama Joyce Kileo ni mama wa nyumbani kutoka Bomang'ombe huko Hai. Mama Mmari anarudi nyumbani leo baada ya Matibabu yake,” alifafanua.
Zitto alisema ukiondoa nchi za Kiarabu, ni Serikali ya Tanzania peke yake katika nchi za Kiafrika inayolipia matibabu raia wake nje ya nchi kwa ajili ya matibabu na kubainisha kuwa licha ya kusaidia wananchi kutibiwa lakini ufike wakati Serikali kuangalia upya uwezekano wa matibabu kama hayo kufanyika nchini.
“Hata hivyo, ni dhahiri kwamba umefika wakati kujenga uwezo wa ndani kutibu magonjwa ambayo teknolojia yake inawezekana kabisa. Natambua mradi wa Hospitali ya Moyo pale Muhimbili na Mradi wa Apollo East Africa kati ya NSSF, UDSM na Apollo India, lakini ni vyema kuharakisha miradi hii ili kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za matibabu ya Watanzania nje ya nchi na hasa India” alieleza.
Akizungumzia matibabu yake alisema kuwa, anatarajiwa kufanyiwa upasuaji leo kuanzia majira ya saa 4:30 asubuhi ambapo ni sawa na majira ya saa 6: 30 kwa saa za Tanzania na kuomba Watanzania kuzidi kumuombea.
Zitto aliondoka Ijumaa iliyopita kwenda India akimbatana na kaka yake, Salum Kabwe na mmoja wa wauguzi wa Muhimbili ambaye jina lake halikufahamika mara moja na jana alisema matarajio yake ni kuwa upasuaji wake utakwenda vyema na kusisitiza Watanzania kuendelea kumuombea kwa Mungu.
“Nawashukuru mno kwa salamu zenu za pole na sala pia dua zenu ambazo mmekuwa mkiniombea. Naomba mniombee zaidi wakati huu nikiwa katika Surgery yangu saa nne na nusu asubuhi. Inshaallah itakwenda vizuri na kurudi tena kuendeleza jalamba la kazi za kuleta mabadiliko nchini kwetu,” alieleza Zitto.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake