Mtoto wa Sumari apata machungu
Kura za maoni sasa kupigwa upya
Ni sarakasi nyingine za kutafunana
Uamuzi huo ambao si wa kawaida, ulifikiwa jana baada ya Kamati Kuu kukutana kupitisha jina la mgombea wa kiti hicho cha ubunge kilichoachwa wazi na Marehemu Jeremiah Sumari aliyefariki Januari 19, mwaka huu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Mnauye, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa uamuzi huo umechukuliwa kufuatia wanachama waliochukua fomu kuomba kuteuliwa kuwania ubunge katika jimbo hilo kushindwa kufikisha asilimia 50 ya kura za maoni zilizopigwa wiki iliyopita.
Alisema Kamati Kuu imeamuru wanachama watakaorudia uchaguzi wa kura za maoni ni Siyoi Jeremiah Sumari aliyeshika nafasi ya kwanza katika kura za maoni na William Sarakikya aliyeshika nafasi ya pili.
Katika kura za maoni, Siyoi Sumari alipata kura 361, William Sarakikya (259), Elirehema Kaaya (205), Elishilia Kaaya (176), Anthony Musani (22) na Rishankira Urio (11).
Hata hivyo, katika kura za maoni kuwania uteuzi wa kugombea ubunge kupitia CCM zilizofanyika mwaka 2010 katika uchaguzi mkuu, wagombea wote walipitishwa kwa kuwa na idadi kubwa ya kura na si kuwa na kura zaidi ya asilimia 50.
Nape alisema kutokana na uamuzi huo Mkutano Mkuu wa Jimbo wa uchaguzi wa kura za maoni utafanyika Machi mosi, 2012.
Alisema utasimamiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Kapteni John Chiligati na Mjumbe wa Kamati Kuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kagera, Costancia Buhiye.
Alisema baada ya mchakato wa kura za maoni kukamilika, Machi 2, 2012 asubuhi, Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Arumeru itakutana kupitia kura za maoni na jioni siku hiyo Kamati ya Siasa ya Mkoa itakutana kupitia mapendekezo yaliyotolewa na wilaya.
Aliongeza kuwa Kamati Kuu itakutana Machi 3, 2012 kwa ajili ya kupitisha jina la mwanachama atakayependekezwa kugombea Jimbo hilo.
“Kama mtakumbuka katika kura za maoni za mwanzo hawa Sioyi na Sarakikya ndio watu waliokuwa wa kwanza na wa pili, lakini katika kura zao hakuna aliyefikisha asilimia 50 ya kura zilizopigwa na kuendelea, kwa hiyo CC (Kamati Kuu) imeamuru kura za maoni zirudiwe apatikane mshindi atakayefikisha asilimia 50 na zaidi,” alisema Nape.
Nape alisema suala la kurudia kura za maoni mgombea anapokuwa hajafikisha zaidi ya asilimia 50 halipo katika katiba ya CCM, lakini limo katika kanuni za uchaguzi hivyo hakuna haja ya kuona suala hili kama ni jipya.
Alisema kwa mfano, katika mchakato wa kupata mgombea urais wa mwaka 1995, Halmashauri Kuu ya CCM ilipeleka majina matatu katika Mkutano Mkuu ambao ni Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Cleopa Msuya ambapo Kikwete aliongoza kwa kura, lakini hakufikisha asilimia 50 hivyo ikaamuriwa kura zipigwe upya na Mkapa akaibuka mshindi.
Alipoulizwa kwamba uchaguzi wa kupata mgombea urais wa CCM mwaka 1995 ulirudiwa siku hiyo hiyo, lakini kwa uchaguzi wa Arumeru Mashariki Kamati Kuu imeamuru urudiwe wakati tayari vikao vya chama ngazi ya wilaya na mkoa vimeshatoa mapendekezo kwa wagombea wote, Nape alisema hilo siyo tatizo kwani hata uchaguzi mkuu wa 2010 hali hiyo ilijitokeza Zanzibar, hivyo hakuna haja ya kuchukulia suala hili kama ni jambo geni ndani ya CCM.
“Ngoja niwakumbushe hasa kwa wale wanaotaka kuendeleza umbeya, mwaka 1995 Halmashauri Kuu ilipeleka majina matatu, Mkapa, Kikwete na Msuya, kura zilipopigwa Kikwete akaongoza, lakini hakufikisha asilimia 50 zikarudiwa na Mkapa akashinda, tusitengeneze hili suala kama ni ‘special case’ nendeni kwenye kanuni zetu za uchaguzi mtapata majibu,” alisema Nape.
Kuhusu madai kwamba Sioyi Sumari siyo raia wa Tanzania, alisema Kamati Kuu imelichunguza suala hilo na haukupatikana ushahidi unaoonyesha kwamba siyo raia wa Tanzania na kwamba vyombo vyote vimethibitisha kuwa suala la uraia halina tatizo.
Nape pia alizungumzia suala la baadhi ya wanachama Umoja wa Vijana mkoa wa Arusha (UVCCM) kumpigia debe Sioyi kwamba vikao vya juu vya chama vimpitishe yeye tu, alisema hayo yalikuwa ni mawazo ya mtu na siyo ya UVCCM kama taasisi ya CCM.
Tangu kutangazwa kwa Sumari kuwa msindi wa kura za maoni, zimeibuliwa hoja mbalimbali juu ya uhalali wake, nyingine zikieleza kuwa jimbo hilo linageuzwa kuwa ni la kifalme kutokana na kujipanga kumrithi baba yake.
Pia kumekuwa na hisia kwamba harakati za kuwania jimbo hili zinajithihirisha katika makundi yanayojipanga kusaka urais mwaka 2015, huku wengine wakitumia karata ya uraia ili kumwengua Sumari.
KURA ZA MAONI CHADEMA KESHO
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinatarajia kufanya uteuzi wa awali kesho kwa kupitisha jina la mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho Arumeru Mashariki.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Arumeru, Totinan Ndonde, alisema uteuzi huo wa awali utatokana na jina ambalo wajumbe wa chama hicho 1,186 watalipigia kura na kuongoza.
Alisema baada ya wajumbe hao kupiga kura watatangaza majina ya wagombea wote na yule aliyeongoza, baada ya wapigakura kumchagua ndio Kamati ya Utendaji itakaa na kutoa maoni yake, kisha Kamati Kuu itakaa na kuteua jina la mgombea wake.
Aidha alisema wagombea wote wamerudisha fomu ambao ni Anna Mghwira, Godlove Temba, Joshua Nassari, Samueli Shamy, Yohane Kimuto na Rebecca Magwisha.
Aliwasihi wajumbe wa Chama hicho kujitokeza kwa ajili ya kuchagua jina la mgombea.
Uchaguzi wa mdogo jimbo la Arumeru Mashariki unafanyika kutokana na kifo cha mbunge wake, Jeremiah Sumari, aliyefariki mwezi uliopita. Kura zitapigwa Aprili mosi mwaka huu.
Thobias Mwanakatwe, Dar na Cynthia Mwilolezi
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake