Wednesday, February 15, 2012

CECAFA kuwaleta Zambia Dar

Katibu Mkuu wa CECAFA,
Nicholas Musonye



Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limesema kuwa litawaalika mabingwa wapya wa Kombe la Mataifa ya Afrika, timu ya taifa ya Zambia 'Chipolopolo' katika mashindano yake ya Kombe la Chalenji mwaka huu ambayo huenda yakafanyika nchini kwa mara ya tatu mfululizo.
Maamuzi ya mwisho kuhusu mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Chalenji yataamuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao watatakiwa kusaka wadhamini wengine washiriki huku Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), inayomaliza mkataba wake wa miaka mitatu mwaka huu ikiwa na nafasi ya kuchangia juu ya kuyabakisha mashindano hayo nchini.

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili kutoka Gabon, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, alisema kuwa ameshampa taarifa Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Zambia (ZFF), Kalusha Bwalya kuhusiana na nia hiyo ya kuwaleta mabingwa hao kama sehemu ya kuzipa changamoto timu za ukanda huu.
Musonye ambaye alikuwa kwenye fainali hizo kama mmoja wa makamishna wa mechi mbalimbali alisema kwamba kushiriki kwa Zambia kwenye mashindano ya mwaka huu wakiwa na taji la Afrika kutawaongezea morari wachezaji wa timu nyingine ambao watatumia uzoefu wa vinara hao kukuza viwango vyao.
"Inajenga na inaimarisha timu pale wachezaji wanapokuwa wanajiandaa kwa mechi dhidi ya mabingwa wa Afrika au klabu kubwa, timu au yenye nyota wa kimataifa," alisema Musonye.
Alisema kuwa kama ilivyokuwa kwa TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliyoalikwa katika mashindano ya klabu ya Kombe la Kagame baada ya kutwaa ubingwa wa Afrika, ndivyo mwaka huu watakavyojaribu kuwapata Zambia ili kutoa fursa kwa wachezaji wa ukanda huu kupata uzoefu kutoka kwao.
Alisema kwamba anaamini Zambia ambayo ni mwanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA), itatoa maandalizi mazuri pia kwa timu ambazo zitakuwa zimefuzu kushiriki fainali zijazo za Afrika (AFCON) ambazo zitafanyika Januari mwakani nchini Afrika Kusini.
Tanzania ambayo iliyokuwa mwenyeji wa mashindano ya Chalenji mara mbili mfululizo, ilitwaa ubingwa mwaka juzi lakini ‘ikachemsha’ mwaka jana baada ya kuishia katika hatua ya nusu fainali na mwishowe kombe likatua kwa Uganda ‘The Cranes’.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake