WIKI iliyopita katika sehemu ya tatu ya makala haya, nilieleza kwamba huwezi kujifananisha na mtu mwingine, vilevile kwa mwenzi wako, haipendezi pia haitakiwi kumlinganisha na yeyote yule. Kila mmoja yupo tofauti kwa sababu kadhaa. Pamoja na ukweli ni kwamba suala la kumtazama mtu na kumuona anakuzidi linaweza kukupa unyonge lakini ujinga wa kupindukia.
Watu wengi husumbuliwa na mawazo kuwa wenzi wao wanaweza kuwaacha na kwenda kuanzisha uhusiano na wengine wenye ubora kuliko wao. Kama mpenzi wako aliwahi kuvutiwa na mtu mwingine kabla yako, huwezi kujua, muhimu ni kuzingatia kile ambacho amevutika kwako.
Zingatia kuwa endapo mwenzi wako angekuwa amedata kwa mtu mwingine tofauti na wewe, huwezi kujua lakini ukweli ni kwamba msingekuwa na uhusiano wa kimapenzi mlionao leo. Achana na mawazo yasiyojenga, amini kuwa mwenzako amedata kwako ndiyo maana leo mpo pamoja.
Jenga utaratibu mzuri wa kuheshimu jinsi mwenzako alivyo. Kadhalika jiamini kwamba duniani hakuna mtu bora kama wewe, kwa hiyo usiishi kwa kumuogopa mtu kutokana na fedha zake au sifa nyingine yoyote. Dunia imeumbwa na vitu tofauti, hivyo na watu wametofautiana, ingekuwa wote tunafanana, hakika ingekuwa ni ulimwengu ‘unaoboa’ kuishi.
4. BADILI WIVU KWA HISIA CHANYA
Jifunze kutafsiri matendo yake kwa upendo. Vuta picha na ujipe hamasa chanya badala ya kuumia kwa kila atendalo. Katika hili, ni vizuri ukaongozwa na subira, kwani asili ya watu wenye wivu wa kupindukia, hukimbilia kupandwa na jazba, badala ya kuuliza kwa utaratibu na kupokea jibu linalojitosheleza.
Hata siku moja usije ukadanganywa kwamba ukiwa mkali ndiyo kutamfanya mpenzi wako asikusaliti. La hasha! Wekeza upendo kisha muishi kwa maelewano, hapo utaweza kumpa sababu ya kuishi kwa uaminifu. Utafiti unaonesha kuwa kundi la wasaliti wa uhusiano wao, huundwa na idadi kubwa ya watu waliochoshwa na migogoro ya kimapenzi.
Mantiki hapa ni kuwa mtu yupo kwenye uhusiano wake lakini anaamua kutoka nje baada ya kuona hana maelewano na mwenzi wake. Hivyo basi, ni vizuri ukawa unafuata hatua zinazofaa katika kupata ufumbuzi wa kila jambo unaloona halipo sawa kwa mwenzi wako, badala ya kugombezana. Itakugharimu.
Kama wivu wako unakufanya ujione wewe ni dhaifu, huna jambo la kufanya zaidi ya kuhakikisha unaishinda hali hiyo. Ukiwa na tabia ya kujiamini, itakusaidia kuufunika wivu, japo bado utaendelea kuwepo ndani yako lakini jinsi utakavyokuwa unashughulikia mambo yako na mwenzi wako, itakupa heshima zaidi.
Wivu ukizidi ni hatari kwa sababu unaweza kukuweka roho juu muda wote, ukaonekana mapepe na jamii ikakucheka kutokana na jinsi kichwa chako kilivyo rahisi kushika moto. Hii ina maana kuwa kudhibiti wivu ni kujiongezea heshima. Tafakari mwenyewe, unataka uheshimiwe au udharauliwe?
Unajidharau? Unakosea sana, muonekano wa juu hubadilika kutokana na wewe mwenyewe unavyoamua na kujipanga. Tatizo ni nguo? Mbona hivyo ni vitu vya kununuliwa? Unayo nafasi ya kutafuta na kupata, kwa hiyo punguza kuchachawa, wekeza upendo kwa sababu ndiyo dawa ya kila kitu.
Jambo lingine ni kuwa hutakiwi kumlazimisha mwenzi wako kuwa kama unavyotaka wewe lakini si vibaya kumshauri akawa na muonekano ambao unakuvutia. Labda anavaa akiwa anaacha wazi maungo yake, haitakiwi upandwe na jazba kisha kumtolea maneno makali, kaa naye mjadili mavazi sahihi.
Mapenzi ni diplomasia, hivyo wewe zungumza halafu muachie nafasi na yeye aseme linalompendeza. Hakikisha hutumii maneno ya kuudhi katika mazungumzo yenu. Vilevile na yeye anapaswa kudhibiti hasira zake. Mwisho mnakubaliana kwa upendo. Vuta picha inavyokuwa, mapenzi yanataka hivyo.
3. UNARUHUSIWA KUULIZA
Kuna jambo linakutatiza au umeona mwenzi wako anawasiliana na watu ambao huwaelewi, inawezekana pia akawa karibu na mtu wa jinsi yako, kwa hiyo unahisi kwamba unaweza kuibiwa.
Itaendelea wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake