![]() |
| Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Idd. |
MWITO wa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho wa kuiomba Serikali ya Zanzibar kuchukua hatua za haraka kupiga marufuku uingizwaji wa vifaa vya analoji nchini, nauwekea uzito.
Spika Kificho aliyekuwa Mwenyekiti wa semina ya siku moja ya utoaji elimu ya uingizwaji wa mfumo wa digitali iliyoandaliwa kwa pamoja na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetoa ushauri huo wakati muafaka.
“Uingiaji wa vifaa vya analogi hapa Zanzibar hivi sasa umeongezeka kwa vile ni kituo kikuu cha kupokea na baadaye kusifirisha katika mwambao wa Afrika Mashariki,” anasisitiza Spika Kificho.
Spika Kificho anasema kuendelea kupokea vifaa hivyo kwa sasa ni kuwatia hasara wananchi pamoja na kuchafua mazingira kwa vile ni miezi michache tu, Taifa linakaribia kuingia katika mfumo huo wa digitali.
Tatizo linaloikumba Zanzibar, Tanzania Bara haiwezi kuwa kisiwani, ni wazi kutokana na mageuzi ya utumiaji mfumo wa analogi na kuingia mfumo wa digitali, nchi zilizotangulia zitatumia nchi hizi kuwa dampo la bidhaa hizo za analogi.
Ushauri wa Spika Kificho wa kutaka runinga zote za analogi zizuiwe kuingizwa nchini ili wananchi wasidanganyike wakanunua na baadaye kuingia gharama za kuwa na ving’amuzi,
unatakiwa kupewa uzito unaostahili katika pande zote za Muungano.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, sambamba na Spika Kificho wametoa ushauri huo kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati ikitolewa elimu kwa umma kuhusu utangazaji wa kutumia digitali.
Balozi Seif anasema seti nyingi za runinga za analogi zimekuwa zikiingizwa kwa wingi katika nchi ambazo hazijaanza matangazo ya digitali athari ambazo zimeikumba Zanzibar. Serikali imedhamiria kwenda sambamba na mageuzi ya utangazaji chini ya ZBC, Taifa hilo linaingia katika Teknolojia ya digitali kabla ya Desemba 2012.
“Serikali yetu inafanya mazungumzo na Benki ya Exim ya China kwa lengo la kuipatia mkopo kwa ajili ya kununua mitambo ya kurushia matangazo na kuimarisha studio za kutangazia
kuendana na mabadiliko ya teknolojia,” anasisitiza Balozi Seif.
Katika semina hiyo ambayo mada nyingi kuhusu elimu ya utumiaji teknolojia ya digitali, zilitolewa zote zililenga kueleza uzuri wa kuingia kwenye mfumo wa digitali, ambao kama nchi ni lazima iingie.
Moja ya mada hizo ilitolewa na Mrajis wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Abdulla Hassan Abdulla, ambaye amesema kuhusu utafiti mdogo uliofanywa unaonesha kwamba Zanzibar
ina takribani seti za runinga 300,000 za mfumo wa analogi hivyo akasema changamoto ipo ili kwenda sambamba na mfumo wa teknolojia kwa vile tayari dalili za gharama kubwa za seti zinazoingizwa nchini zimeanza kuonekana.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Tanzania, Ali Gunze, akitoa mada ya uhamaji kutoka analogi kwenda digitali katika sekta ya runinga wala si redio, anasema mfumo wa digitali
utawawezesha wananchi kupata huduma nyingi na bora zenye taaluma ya kiwango cha juu kwani chaneli zitaongezeka kutoka 21 hadi 69 wakati masafa yataongezeka kutoka 760 hadi
862 kwa mujibu wa azimio la Tume ya Kimataifa ya Mawasiliano ( ITU).
Mwakilishi wa TCRA, Innocent Mungy, akitoa mada ya mkakati wa elimu kwa umma juu ya uhamaji wa mfumo mpya wa digitali anasema, mkakati wa kutoa elimu ni muhimu na wa lazima kwa wananchi na jamii na ni vyema ikafurahia huduma za digitali.
Tanzania ikiwamo Zanzibar pamoja na za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zinatakiwa kutekeleza maazimio ya mkutano wa Geneva, Uswisi, ya mwaka 2006 ya kuanza kurusha
matangazo kwa mfumo wa digitali badala ya mfumo wa sasa wa analogi.
Katika kutekeleza maagizo ya mkutano huo wa Geneva, Tanzania inatakiwa kuwaandaa watu wake, kuwajulisha faida za kujiunga na gharama watakazopata katika kununua runinga na ving’amuzi vipya vya mfumo wa digitali.
Katika kwenda sambamba na kasi ya mageuzi, TCRA inatarajia kuzima mitambo yake ya matangazo inayotumia mfumo wa analogi ili kuibadilisha na kuanza kutumia mfumo wa
digitali mwaka huu.
Uamuzi huo wa kuzima unaofanyika kwa lengo la kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya teknolojia hiyo duniani, ambayo Tanzania kama nchi haina budi kukubaliana nayo.
Meneja wa Kanda ya Kati wa Mamlaka ya Mawasiliano, Maria Sasabo, siku chache zilizopita amewaeleza wananchi wanaotumia runinga za analogi kuwa watalazimika kununua ving’amuzi vya digitali ili kuendelea kupata matangazo mbalimbali.
Kauli inayoashiria wazi kuwa wananchi wajiandae kuachana na kununua runinga za analogia kama Spika Kificho alivyoshauri kisiwani Zanzibar ili kupunguza gharama za kununua vifaa
ambavyo matumizi yake yatadumu mufa mfupi na watunze fedha kwa ajili ya kununua ving’amuzi vya digitali.
Katika mkutano mmoja na wadau wa mawasiliano nchini, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Prof. John Nkoma, amesema mamlaka yake inawasiliana na Serikali ili kuona uwezekano wa
kuondoa kodi kwenye ving’amuzi vya runinga ili kupunguza gharama na wananchi wa kawaida wavinunue.
Jambo ambalo linatanabaisha kuwa TCRA imebaini kuwa kuna nyongeza ya gharama kwa wananchi waliokuwa wakitumia runinga za analogia kwenda mfumo wa digitali, ambapo
watatakiwa kununua ving’amuzi vipya kwa lengo la kuendelea kupata matangazo ya runinga.
Uamuzi wa kuomba nafuu ya kodi kwa ving’amuzi vya runinga za digitali kutasaidia mashirika yaliyopewa dhamana ya kuuza ving'amuzi hivyo Star Times,Ting Agape TV, Sahara Communication na IPP Media, kuuza kwa bei nafuu.
Ni ukweli usiopingika pamoja na mafanikio ya kuingia mfumo mpya, bado mabadiliko hayo kutoka analogia kwenda digitali yatawaongezea Watanzania gharama nyingine ya maisha ya
kulipia huduma za ving’amuzi kama wanavyolipia huduma nyingine nyingi.
Kabla ya mabadiliko hayo, walitumia minara ya kawaida tu, wakawa na uhuru wa kupata stesheni mbalimbali bila kulipia gharama za ziada, hivyo mabadiliko hayo yataongeza gharama nyingi zikiwamo hizo za kununua ving’amuzi, lakini pia ving’amuzi hivyo havioneshi stesheni nyingine za hapa nyumbani, jambo ambalo linatakiwa kuangaliwa kwa macho mawili.
Wakati mfumo wa analogia ukitakiwa kuondoka sokoni, kasi ya uingizaji runinga za analogia ni kubwa mno, kiasi cha kuonekana Tanzania inakuwa dampo la vifaa hivyo ambavyo
havitatumika muda mrefu kutokana na mabadiliko hayo.
Zanzibar wameliona hilo, ndio maana Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif amelikemea kuwa makini nalo, jambo ambalo Tanzania haitaepuka, inatakiwa kutolewa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuingia kwenye digitali na kuchana runinga za analogia.
Miradi ya majaribio kuhusu matumizi ya digitali inafanyika katika mikoa minne ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Arusha, imeonesha mafanikio makubwa, hivyo kampeni
inatakiwa kuongezeka ili kuhakikisha nchi nzima mwishoni mwa mwaka inaingia katika mfumo wa digitali.
Ifikapo mwakani, Tanzania na nchi zingine za Afrika Mashariki, zitakuwa ziwe zimeingia katika mfumo wa digitali utakaowawezesha wenye televisheni kuangalia matangazo yao kwa ubora zaidi, lazima kila mmoja atalazimika kuingia kwenye mfumo huo.
Habari Leo

No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake