Wajumbe waja juu kugeuza usultani
Wasema sasa mwisho mihula miwili
Mukama atakiwa atekeleze mabadiliko
Wasema sasa mwisho mihula miwili
Mukama atakiwa atekeleze mabadiliko.jpg)
Jumuiya hiyo inataka wanaoshika nafasi hizo wakae kwa vipindi viwili tu na baada ya hapo waende kugombea katika majimbo na kata.
Wanasema kuna wanawake ambao wamedumu katika nafasi hiyo kwa miaka mingi.
Suala hilo sasa limerudishwa UWT kwa ajili ya kufanyiwa maamuzi, baada ya kamati ya wabunge wa chama hicho kutaka suala hilo litazamwe upya na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.
Kumuiya hiyo ndiyo iliyoibua wazo hilo na kuliwasilisha NEC kisha ikalipelekwa kwa kamati ya wabunge wa CCM ambayo nayo iliamua lirejeshwe NEC.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, wakati akifungua kikao cha kazi cha Baraza Kuu la UWT mjini Dodoma.
“Najua ni tete sio nyeti…linaweza kuwa tete tu, lakini sio nyeti hilo la ukomo wa vipindi viwili kwa ubunge, uwakilishi na mimi na wenzangu kwenye Sekretarieti limezungumzwa na wameomba nilifikishe na maelekezo ya Halmashauri,” alisema.
“Ni maelekezo ya Halmashauri Kuu kuhusu ukomo na ndio sababu napenda nisome ili yasionekane kama ni maneno yangu nayatoa mdomoni, Halmashauri Kuu ya Taifa iliyofanya kikao chake tarehe 14 hadi 15, pamoja na mambo mengine baada ya kupokea taarifa kutoka katika Kamati Kuu, ilielekeza kwamba viti maalum vya ubunge, uwakilishi na udiwani, viwe na ukomo wa vipindi viwili,” alisema huku wajumbe wakishangilia kwa kupiga vigelegele na makofi.
Alisema baada ya kumaliza vipindi viwili vya nafasi za viti maalum, watalazimika kwenda kugombea na wanaume kwenye majimbo.
Alisema uamuzi huo ulifanywa na NEC, kwa kuzingatia kuwa baada ya vipindi viwili wahusika watakuwa wamepata uwezo, ujasiri na kujiamini kugombea katika majimbo.
“Utaratibu huo ulielekezwa uanze kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ili kuwapa wanawake wabunge, wawakilishi na madiwani wa viti maalum kwenda kugombea majimboni,” alisema.
Mukama alisema kamati ya wabunge wote wa CCM katika kikao chao kilichofanyika Februari 7 mwaka huu, ilipendekezwa uamuzi huo wa NEC urudishwe tena na kutazamwa upya ili kusiwe na ukomo.
“Lakini kwa kuwa uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ulitokana na mapendekezo kutoka Baraza Kuu la UWT (wanashangilia tena), tunashauri mjadala wa suala hili urudi tena UWT (wanakataa kwa sauti kubwa), mnataka tuwaambieje?”
Mukama aliwahoji wajumbe wa baraza kama wanaendelea na msimamo wao wa awali wa kuweka kikomo katika ubunge wa viti maalum. “Kwa hiyo tunalifikisha tena kwa sababu lilikuja kama ombi mlitolee uamuzi.”
Akizungumza kabla ya ufunguzi wa kikao hicho, Mwenyekiti wa UWT, Sophia Simba, alisema kikao hicho kinatarajia kujadili mambo mbalimbali yanayohusu umoja huo.
Sophia alisema moja ya mambo ambayo yanatarajiwa kujadiliwa ni uchaguzi wa UWT na marekebisho ya katiba.
“Nyakati za uchaguzi wote tunazijua, nyakati ngumu kidogo wengi tumechaguliwa kama miaka minne iliyopita na sasa tunaingia tena kwenye uchaguzi mwingine, kwa hiyo lazima muelewe inakuwaje kuna mabadiliko hapa na pale,” alisema.
Alisema UWT ndiyo timu ambayo ilihakikisha CCM inashinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na umoja huo ulifanikiwa kwa sababu ulikuwa na ushirikiano.
NAPE: HATUJAWAENGUA WAZEE
Wakati huo huo, CCM imesema uamuzi ulioridhiwa na NEC kuruhusu kuundwa kwa Baraza la Ushauri la Viongozi wa Kitaifa Wastaafu si mpango au mkakati wa kuwaengua makusudi wazee hao kwenye vikao vya Kamati Kuu (CC) na NEC ya chama hicho, bali ni wazo lilitokana na baadhi ya wazee wenyewe wastaafu, wakiongozwa na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenenzi ya CCM Taifa, Nape Nnauye, akizungumza na waandishi wa wahabari jijini Dar es Salaam jana, alisema kilichofanywa na NEC katika kikao chake cha Februari 12, mwaka huu, mjini Dodoma, ni kuridhia tu mabadiliko ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2010 ili kuruhusu kuundwa kwa baraza hilo.
Alisema wazo hilo la wazee lilibainishwa na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, ambaye kabla ya uamuzi huo kuridhiwa na NEC na baada ya kupotoshwa, alithibitisha kwamba, limetokana na wao wenyewe.
“Mwinyi alieleza akasema hili limetokana na sisi,” alisema Nape.
Alisema wazo hilo lilitolewa na wazee hao wakizingatia wingi na urefu wa vikao husika.
“Si mpango au mkakati wa kuwaengua makusudi wastaafu hao kama inavyodaiwa na baadhi ya wapotoshaji,” alisema Nape.
Aliongeza: “Ilikuwa ni ushauri wao kwamba baada ya kustaafu badala ya kulazimika kuhudhuria vikao vya kitaifa kila mara basi wapewe muda wa kupumzika na wanapotakiwa kutoa ushauri watumiwe badala utaratibu wa sasa wa kulazimika kuhudhuria vikao ambavyo kwa kwa kweli ni vingi na wakati mwingine huisha usiku wa manane.”
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake