MKAZI wa kitongoji cha Majengo kijijini Katuma wilayani Mpanda, amejisalimisha mwenyewe Polisi baada ya kumshambulia kwa bakora hadi kufa jirani yake aliyemkuta akimbaka binti yake mwenye umri wa miaka 13.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, tukio hilo lilitokea juzi saa nane za usiku katika kitongoji hicho cha Majengo.
Mwaruanda alidai kuwa siku hiyo, Sayi Masasila (35) ambaye ni baba mzazi wa msichana huyo aliyebakwa, alimkuta jirani yake, Sadock Sideli (30), akimbaka binti yake usiku wa manane chumbani kwa msichana huyo.
Inasemekana kuwa usiku huo wa manane, Sadock alitoka nyumbani kwake na kwenda nyumbani kwa jirani yake Masasila ambako alimkuta binti wa Masasila akiwa amelala kwenye nyumba ndogo iliyopo jirani na nyumba ya wazazi wake.
Kwa mujibu wa Mwaruanda, Sadock alipofika nyumbani hapo alivunja mlango na kuingia ndani na kuanza kumbaka binti huyo ambaye kwa mshtuko mkubwa, alipiga kelele za kuomba msaada ndipo baba yake alipozinduka usingizini na kukimbilia mara moja kwenye nyumba ndogo alimokuwa amelala bintiye.
“Masasila ambaye ni baba wa msichana huyo alipofika kwenye nyumba alimolala binti yake alimkuta jirani yake Sadock akimbaka binti huyo akiwa tayari amejihami na fimbo, Masasila alianza kumshambulia jirani yake huyo kwa kumcharaza fimbo hadi akafa pale pale,” alidai Mwaruanda.
Kwa mujibu wa Polisi, Masasila alijisalimisha mwenyewe katika Kituo cha Polisi cha Mwese baada ya kumuua jirani yake, na sasa anaendelea kushikiliwa hadi atakapofikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake