Mgombea ubunge jimbo la Arumeru Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi,Sioi Sumari(kulia) akisalimiana na wajumbe wa mkutano mkuu wa jimbo hilo eneo la Usa River,wilayani Arumeru kabla ya upigaji kura za maoni za chama hicho juzi.Picha na Filbert Rweyemamu
Waandishi Wetu
MVUTANO mkali umeripotiwa kutokea ndani ya kikao cha Kamati ya Siasa ya CCM, Mkoa wa Arusha kuhusu ni mapendekezo yapi yapelekwe mbele ya Kamati Kuu (CC) ya chama hicho baada ya matokeo ya kura za maoni kwa wanaowania kupitishwa na chama hicho kuwania ubunge katika uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema mvutano huo ulisababishwa na baadhi ya wajumbe wa kutaka kuondolewa kwa jina la mshindi katika kura hizo, Sioyi Sumari kwa madai kwamba ushindi wake wa kura 761 uliambatana na vitendo vya rushwa hivyo hafai kuwa mgombea wa CCM.
Katika matokeo ya uchaguzi uliorudiwa juzi, Siyoi aliibuka mshindi kwa kupata kura 761 ambazo ni sawa na asilimia 67.8 ya kura halali 1,122 zilizopigwa, dhidi ya asilimia 32.2 za mpinzani wake, William Sarakikya ambaye anadaiwa kwamba anapigiwa chapuo na viongozi wa CCM na Serikali katika ngazi za wilaya, mkoa na taifa.
Katika uchaguzi wa awali wa kura za maoni uliofanyika Februari 20 mwaka huu, Siyoi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Jeremia Sumari aliyefariki hivi karibuni, aliongoza kwa kupata kura 361 akifuatiwa na Sarakikya aliyejinyakulia kura 259.
Habari zinasema wakati kikao kikiendelea jana, mmoja wa vigogo wa Serikali ambaye ni mjumbe wa kikao hicho anadaiwa kuomba kwenda kufuata ripoti ya tuhuma za rushwa katika Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), mkoani Arusha.
Baada ya muda inadaiwa kwamba alirejea na kile kilichodaiwa kuwa ni ripoti hiyo kisha kuiwasilisha mbele ya kikao akiwaonyesha wajumbe vielelezo mbalimbali vilivyopo ndani yake.
Taarifa hiyo ndiyo inayodaiwa kusababisha vuta nikuvute kutokana na baadhi kuipinga huku wengine wakiiunga mkono. Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda alipoulizwa juu ya taarifa hizo alikanusha akisisitiza kwamba kikao hicho kilikuwa ni cha siri na taarifa zake haziwezi kuzungumzwa hadharani.
Imeelezwa kwamba kutokana na mvutano huo ndani ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Arusha, wajumbe waliamua kwamba majina yote mawili, ya Sioi na Sarakikya yapelekwe mbele ya CC kama matokeo ya kura za maoni yanavyoonyesha yakiambatanishwa na maelezo na kile kilichodaiwa kuwa ni vithibitisho vya rushwa.
Kamati Kuu leo
Kutokana na hali hiyo ni dhahiri kwamba kikao cha Kamati Kuu kinachokutana Arusha leo chini ya Rais Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa mwisho wa mgombea atakayebeba bendera katika uchaguzi huo, kitakuwa na wakati mgumu kufikia uamuzi kwa kuzingatia mambo makubwa mawili.
Kwanza kuamua kumweka pambeni Sumari kutokana na tuhuma hizo za rushwa zinazomwandama baada ya wanaodaiwa kuwa wafuasi wake kukamatwa na Takukuru lakini pili kumpitisha mgombea huyo kwa kuzingatia ushindi wa kura nyingi alizopata kwa wana CCM wenzake wa Arumeru.
Akichambua mwenendo wa kumpata mgombea wa CCM katika jimbo hilo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema uamuzi wa wapiga kura unapaswa uheshimiwe.
“Tatizo letu Watanzania hatufuati misingi kamili ya demokrasia. Tunafuata tu matakwa ya watu binafsi. Kama kwenye kura za maoni za kwanza, Siyoi alishinda na kwa mara ya pili ameshinda, kuna haja gani tena ya kujadili jinsi ya kumpata mgombea?” alisema Profesa Mpangala na kuongeza:
“Kule tu kurudia kura za maoni ni ukiukwaji wa demokrasia. Hakukuwa na sababu za msingi za kurudia kwani mshindi alishapatikana. Hizi ni siasa za kizamani za chama kimoja. Kama wanafuata matakwa ya wakubwa kwa nini kuwe na uchaguzi? Kwa nini kampeni zipigwe kwa miezi miwili na zaidi? CCM inapaswa kubadilika na kusikiliza uamuzi wa wananchi.”
Huku akimnukuu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, Profesa Mpangala alisema utaratibu wa kurudia kura za maoni haupo hata kwenye Katiba ya CCM isipokuwa hutokea tu kwa matakwa ya watu fulani.
“Nape alisema japo utaratibu huo haupo, lakini hutokea tu kwa nyakati fulani. Alitoa mfano wa kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM mwaka 1995 ambapo Rais Kikwete alishinda, lakini ikaamuliwa kuwa kura zirudiwe na ndipo aliposhinda Mkapa.
Kimsingi kura za maoni huwa hazirudiwi. Mimi sijui kwa nini zimerudiwa huko Arumeru. Kama Sioyi alishinda na sasa ameshinda, basi hiyo ni dalili ya kukubalika kwa wananchi. Ikiwa kikao cha Kamati Kuu kitamwengua, basi tutajua kuwa CCM hakifuati misingi ya demokrasia.”
Wafanyakazi wa Lowassa
Wakati hayo yakijiri, kamatakamata ya Takukuru iliendelea na safari hii ilianza kuwakumba pia wanahabari.
Miongoni mwa wanahabari waliothibitika kutiwa mbaroni jana ni Meneja wa Kituo cha Redio 5, Jimmy Mtemi. Kituo hicho kinamilikiwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa
Wana CCM wengine watatu walikamatwa kwenye msako huo wa Takukuru. Chanzo cha habari kutoka kwenye Redio hiyo kilieleza kwamba maofisa hao walitumia siku nzima ya jana kumtafuta Ofisa mmoja wa Redio hiyo, Pili Sirikwa.
“Hawa jamaa baada ya kumkosa Pili walikuja huku Njiro kilipo kituo cha redio wakamwulizia, walipoambiwa hayupo wakaondoka. Baada ya muda kupita walirudi tena sasa hapo ilionekana kuwa ni kwa ugomvi kwani mlinzi aliyekuwa getini walimsukuma na kuvamia ndani kisha kwenda moja kwa moja ofisini kwa Meneja.
“Baada ya kufika hapo walimweleza kuwa wanahitaji kuondoka naye hadi ofisini kwao kwa ajili ya mahojiano. Lakini kabla ya kuondokana naye walimpora simu zake za mkononi na kuzizima,” alidai mtoa taarifa wetu.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Mbengwa Kasomambuto alipoulizwa kama ana taarifa zozote za kukamatwa kwa Meneja wa Redio 5, alisema bado hajapata taarifa hizo kwani alikuwa nje ya ofisi.
“Nipo nje ya ofisi nadhani kesho nitakuwa na taarifa sahihi,” alisema Kasomambuto.
Chadema nao leo
Kwa upande wake, Kamati Kuu ya Chadema leo pia inatarajia kufanya kikao hapa Arusha kutangaza jina la mgombea wao, Joshua Nassari kuwania kitu hicho.Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema juzi kuwa kikao hicho kitafanyika wilayani Arumeru na tayari wajumbe kadhaa wamewasili Arusha.
“Wanachama wa Arumeru na viongozi wao wamekwishaamua juu ya mgombea wao na wametuletea mapendekezo yao na sisi tutatangaza mgombea,” alisema Dk Slaa.
Matokeo ya kura za maoni ndani ya chama hicho zilizopigwa Jumatano iliyopita yanaonyesha kwamba Nasari aliibuka na ushindi wa kishindo wa kura 805, sawa na asilima 90.6 ya kura zote 888 zilizopigwa akifuatiwa kwamba mbali na Anna Mghiwa aliyepata kura 23. Wagombea wengine na kura zao kwenye mabano ni pamoja na Samuel Kimutho (10), Yahane Shami (6), Antthon Musami (8), Rebecca Magwisha (12) na Goodlove Temba aliyepata kura 18.
Imeandaliwa na Elias Msuya Dar na Mosses Mashalla, Peter Saramba na Mussa Juma, Arusha.

Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake