Friday, March 2, 2012

CUF yameguka mkoani Mara

NAIBU Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, amepata pigo baada ya viongozi wa chama hicho mkoani Mara kutangaza kujiuzulu nafasi zao na kujivua uanachama wa chama hicho katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kuimarisha chama hicho mkoani Mara. 

Viongozi waliotangaza kuachia nafasi zao na kukihama chama hicho huku wakitumia usemi wa kujinyonyoa manyoya, ni Mwenyekiti wa Musoma Mjini, Didi Koko na Katibu wa Musoma Mjini, Jumanne Magafu.
 

Wengine ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake na Mkurugenzi wa Fedha Musoma Mjini, Maimuna Matola, Kamanda wa Blue Guard, Aman Chogo na wajumbe sita wa Kamati ya Utendaji wakiongozwa na Amidu Waitare. 

Pia waasisi wa chama hicho zaidi ya 10 wakiongozwa na Adam Gunje na Iddy Mtani walikabidhi kadi zao na za wanachama wengine karibu 900 ambao pia wamehama. 

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kutangaza kujiondoa kwenye chama hicho, Koko alisema wamefikia hatua hiyo kwa kuwa CUF imepoteza mwelekeo kwa kushindwa kuheshimu Katiba yake na ya nchi na sheria zake. 

“Viongozi wetu wa CUF kitaifa hawaheshimu uongozi, wameshindwa kutambua msingi wa chama na kujua ni wapi walipotoka na walipo, badala yake wamekuwa wakiendesha chama kwa maslahi binafsi, si yetu sisi wanachama,” alidai Koko. 

Alidai chama hicho kilianzishwa na misingi, lakini hivi sasa kimevamiwa na kundi la watu wasio na maadili ya kutumikia wanachama na Watanzania kwa jumla, jambo linaloonesha wazi kupoteza mwelekeo kwa kuendeshwa kisultani na kufanya wanachama kuwa kama mateka. 

Maimuna ambaye alikuwa pia Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa wa CUF na aliyepata kugombea ubunge wa viti maalumu kabla ya kudai kuchakachuliwa na viongozi wa Taifa, alidai kuwa uamuzi wake wa kujiondoa unatokana na viongozi wa CUF kutojali matakwa ya wanachama na kuzuia haki za msingi zikiwamo za kugombea nafasi za juu ndani ya chama. 

“CUF imekuwa genge la watu fulani na si chama tena cha wananchi, kimekuwa kikigandamiza haki za msingi za wanachama kwa kuzuia wanachama kugombea nafasi fulani eti ukifanya hivyo tu, unaitwa muasi … hii ni kinyume cha Katiba ya chama chetu,” alisema Maimuna. 

Gunje alidai mtazamo wa chama hicho kuwa cha wananchi haupo tena, bali kimebaki kuwa cha usultani kwa kufukuza watu bila utaratibu. Mtani alisema malengo ya CUF sasa hayatekelezeki, kwa vile usemi wa ‘haki sawa kwa wote’ umegeuka kuwa ‘haki sawa kwa wachache’. Alidai kuwa mabadiliko hayo yamemfanya kujiondoa mapema ili asiwe sehemu ya laana itakayokikumba chama hicho. 

Muasisi wa CUF Musoma Vijijini, Elly Lyako alitangaza kujiondoa na kuwakilisha chama hicho Musoma Vijijini kwa kudai hivi sasa CUF Musoma Vijijini imefungwa, baada ya kuona viongozi wa kitaifa wakiongoza chama hicho kama kampuni binafsi. 

Walipotakiwa kueleza mustakabali wao kisiasa, viongozi hao walidai kuwa wanafikiria hatima yao kisiasa baada ya kujiondoa CUF huku hatua yao hiyo, ikisababisha ofisi ya CUF mtaa wa Iringo kufungwa. Mtatiro ambaye ni mzaliwa wa wilayani hapa, alipopigiwa simu kueleza namna alivyopokea uamuzi huo, alisema kundi hilo ni linalomuunga mkono Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na kwamba tayari walishafukuzwa chamani siku chache zilizopita. 

Alipotakiwa kutoa vielelezo vya kufukuzwa kwa wanachama na viongozi hao, Mtatiro alidai barua hizo ziko kwa Kaimu Katibu wa CUF wa Musoma Mjini ambaye hakumtaja huku akiomba muda wa kuziwasilisha.


Habari Leo

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake