Tuesday, March 20, 2012

Je, ni kweli wanawake hawajitambui kwenye mapenzi? Tujadili-2

 
MULLY ni mmoja wa waathirika, wapo wanaume wengi waliotendwa na wapenzi wao ambao waliwalea na kutumia fedha nyingi kuwasomesha. Mambo yao yalipokaa sawa na kupata kazi, wakasahau walipotoka na kuanzisha uhusiano na wengine. Kipya kinyemi, mume aliyemsomesha akatupwa mbali.

Janette na wengine wenye tabia za namna hiyo ni muendelezo wa dhana zinazowaharibia wanawake kimapenzi. Wanatakiwa wajirekebishe ili mambo yakae sawa. Wasiwaponze wengine wenye tabia safi, wenye akili hai za kulea familia yenye mafanikio tele.
Ipo dhana nyingine kuwa mwanamke akipendwa sana, hujenga kiburi na matokeo yake humdharau mwanaume anayeonesha mahaba ya ndani kabisa. Kwamba anaweza kumgeuza mwanaume punda kwa sababu tu anajua anampenda. Hachukulii upendo ni tunu, yeye anaubeba kama fimbo ya kuchapia.
Nimeshakutana na watu kadhaa, wananieleza matatizo yao na jinsi walivyoshauriwa na watu mbalimbali. Mathalan, mtu mke wake anamsumbua, anamueleza mshauri kila kitu kinachozunguka mgogoro ndani ya familia yake. Mwisho katika kushauriwa anaambiwa: “Tatizo, umemuonesha mkeo unampenda sana.”
Je, kumuonesha mtu kuwa unampenda ndiyo igeuke adhabu kwako? Ni wazi kuwa mapenzi ya siku hizi, yanatawaliwa na nguvu kubwa ya Shetani ndiyo maana tafsiri yake inakosewa. Ukweli wa mapenzi ni kuwa wawili wanaoamua kupendana ni lazima upendo wao uwe wa ndani ya nyoyo zao na waudhihirishe kwa vitendo.
Ni mateso kujilazimisha kuficha mapenzi, eti unahofia ukimuonesha atajua na atakufanyia vitimbi. Kufanya hivyo ni mateso, bora kutopenda kabisa. Inatupasa kupendana bila kuwa na shaka yoyote ndani. Kila mtu ausikilize moyo wake namna unavyomuongoza na atende pasipo kuhofia kuitwa Bushoke.
 Wakati nashauri kwa watu kuruhusu nyoyo zao ziwaongoze katika kudhihirisha mapenzi yao bila kuogopa jinsi watakavyochukuliwa na jamii, vema nikatoa angalizo kwa wale wanaooneshwa mapenzi, kuheshimu hisia za wenzao. Maisha ya sasa, kupata mtu anayekupenda, anayekujali na kukuheshimu kwa dhati ni bahati.
Ukigundua ni bahati, basi ni vizuri kuitunza kwelikweli, vinginevyo unaweza kuichezea, ukaipoteza, matokeo yake ni kujuta baadaye. Usimfanye mwenzi wako ashindwe kukuonesha penzi la dhati. Mpe uhuru na amani juu yako. Mpokee vizuri, zungumza naye kwa lugha tamu ili ajisikie kuwa nawe.
Ni vipi mwenzio kwa mapenzi aamue kukununulia zawadi aliyoona inafaa, wewe kwa sababu unamdharau kutokana na jinsi anavyokupenda kupitiliza, unaitazama kwa nyodo kisha unapotezea. Husemi hata asante. Inawezekana inakuvutia lakini hutaki tu kumuonesha kwa sababu unamuona katuni, kisa anakupenda kupitiliza.
Mwenzio ametulia, anaona akutoe ‘auti’, mwende sehemu mkapate chakula cha jioni. Hisia zako za dharau juu yake, iliyotokana na mtazamo kuwa anakupenda mpaka kero, unaamua kukataa bila sababu: “Sitaki tu kwenda, acha nipumzike nyumbani.”Mpenzi wako anaumia, wewe unajiona “wa shoka” kwa kumchomolea.
Mapenzi hayapo hivyo, yanakutaka utii upendo wa mwenzio kwako, kwa maana ukiuchezea, unaweza kujuta kwa muda mrefu ujao. Ni sawa na kuchezea almasi na kuipoteza katika kipindi ambacho ulikuwa ‘bize’ ukikusanya mawe. Ukirudi ulipoiacha, utakuta ilishachukuliwa na mwingine anayejua thamani yake.
Hivi kupendwa ni kero? Ndivyo wengine wanavyoona lakini ukweli ni kwamba wanakosea kupita kiasi. Ni dhana ambayo inawashambulia wanawake wengi, ila ipo pia mifano ya wanaume ambao huonesha dharau ya hali juu kwa wanawake wao ambao huwaonesha wanawapenda kupita kiasi.
Mwanaume kumuonesha mwenzi wake kwamba yeye siyo mwaminifu, kwa kigezo kuwa mwanamke hawezi kufanya chochote. Akiona SMS, atalia na kumshukuru Mungu lakini atabaki palepale kwa sababu anampenda sana. Huku ni kujidanganya, ipo siku atachoka na kuondoka.
Asili ya moyo hupenda sana, endapo utatendewa haki, basi utazidi kupenda na kuridhika pale ulipo. Ukipata mapokeo hasi, huumia, ukiumia mara nyingi, hufa ganzi. Ukifikia hatua hiyo, hisia za kupenda hutoweka. Ni hapo utamsikia mwanamke anasema, anawachukia wanaume au mwanaume kuweka wazi kwamba hawapendi wanawake na anaamini ni baba mmoja.
Kimsingi, dhana ambazo nimezitaja kuanzia mwanzo wa makala haya mpaka mwisho, kwa sehemu kubwa zinawaharibia wanawake kimapenzi. Wanaonekana wanaunda tabaka lisilo na shukurani kwa wenzi wao. Jambo jema, wanaligeuza baya na wakifanyiwa baya linakuzwa zaidi.
Hata hivyo, wanawake wanasemwa lakini wanaume pia ni chimbuko la matatizo mengi kwenye uhusiano. Nimejaribu kufafanua kila hatua. Muhimu kuzingatia kwa sasa ni kila mmoja kuheshimu hisia za mwenzake. Ukipendwa na bahati, hebu iwekee mazingira iendelee kuwepo.
Wanawake wanasemwa vibaya zaidi, kwa hiyo mmoja akiharibu, jambo hukuzwa kwa kuonesha kwamba ndivyo walivyo. Wewe ni msomaji wangu mzuri, anza kuwa sehemu ya mabadiliko. Thibitisha kwa vitendo kuwa wanawake mwalimu wao siyo kipofu. Wanawake ndiyo mama, ndiyo walezi. Wanastahili kuwa daraja la juu katika maisha ya kila siku.


www.globalpublishers.info

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake