Monday, March 5, 2012

Lipumba kupasua jipu mgogoro CUF

Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba (kushoto) akifanya mahojiano na Mubelwa Bandio wa Changamoto Yetu Blog, Bethesda, Maryland, Nchini Marekani.

MWENYEKITI wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba anatarajiwa kurejea nchini Jumapili ijayo kutoka safarini Marekani alikokuwa kikazi kwa zaidi ya miezi mitano huku chama chake kikisambaratika kutokana na mgogoro wa uongozi uliokikumba. 

Baada ya kuwasili, Lipumba atapokewa na wanachama wakiwa na msafara wa magari 200 
utakaoanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na baadaye anatarajiwa kuzungumza na wananchi katika eneo la Karume.
 

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Sheweji Mketto jana katika kikao na waandishi wa habari hakutaka kufafanua atakachozungumza Profesa Lipumba, zaidi kuelezea mapokezi hayo. 

Kwa mujibu wa Mketto, kutoka uwanja wa ndege msafara wa Lipumba utapitia barabara za Nyerere, Mandela, Morogoro, Kawawa, Uhuru na kuishia eneo la Karume ambako atazungumza. 

Profesa Lipumba anarejea nchini na kukutana na mgogoro unaoendelea uliosababisha baadhi wa wanachama na viongozi wa CUF, kujivua uanachama huku wengine wakijiunga kuanzisha chama kipya. 

Hamad kususa Kutokana na mgogoro huo, mmoja wa viongozi maarufu wa CUF na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed ambaye alivuliwa uanachama na kuzuia utekelezaji wake mahakamani, alisema jana kuwa hatahudhuria mapokezi hayo. 

Alifafanua kuwa hatua hiyo inatokana na hatua ya chama hicho kumfukuza uanachama. 
“Mimi ni mwanachama kwa nguvu ya Mahakama, kwa hiyo sitahudhuria mapokezi hayo… 
lakini pia gharama inayotumika ni kubwa ambayo ingetumika kuimarisha chama,” alisema 
Hamad. 

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Ilala, Doni Waziri alidai anasikitikia ujio wa Profesa Lipumba kwani anakifuata chama ambacho kilishakufa. 

Naye aliyekuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Segerea, Mussa Ayubu alidai kurejea kwa 
Profesa Lipumba sio kujenga chama, bali ni kuzika chama. 

Pamoja na kauli hizo za ‘uasi’, Mketto alisema CUF itadhihirisha nguvu zake katika mapokezi hayo na kwamba wanachama wake watawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 7 mchana wakiwa na msafara wa magari 200 yaliyoandaliwa tayari kwa 
mapokezi hayo. 

*CUF na msimamo 
Mketto alisema baada ya kazi ya kuwaengua wanachama wasiofaa, sasa CUF imenusurika kwa 
madai kuwa kama wasingewatimua wanachama hao, chama hicho kingekuwa katika wakati mgumu. 

“Katika kila uchaguzi, idadi ya kura za CUF ilikuwa inazidi kushuka… wanachama hao walikuwa na mkakati mzito wa kukihujumu chama na kufika kwa Profesa Lipumba tutadhihirisha uimara 
wetu,” alidai Mketto. 

Nchini Marekani Profesa Lipumba alichaguliwa katika jopo la wanataaluma wanaochambua, 
kupanga na kurekebisha uchumi wa dunia. 

“Kuitwa kwa Profesa Lipumba nchini Marekani kumemkutanisha na wataalamu wa masuala ya uchumi duniani ambao walikuwa na kazi ya kuchambua na kupanga namna ya kurekebisha uchumi wa dunia kwa miaka 25 ijayo,” alisema Mketto. 

Lengo lingine la mapokezi hayo mbali na utamaduni wao kwa mujibu wa Mketto, ni kumpongeza Profesa Lipumba baada ya kuchaguliwa kuwa Mweyekiti wa jopo la wataalamu wa uchumi wa dunia kwa kuwa Serikali ya Tanzania haikumpongeza. 

“Tulisikia katika vyombo vya habari Serikali ya Rwanda ikimpongeza Profesa Lipumba kwa kazi nzuri anayoifanya akiwa Umoja wa Mataifa, hiyo inatokana na kutambua mchango wake kwa nchi za Afrika Mashariki,” alisema Mketo.

Habari Leo

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake