![]() |
| Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo |
Mamia ya wanavijiji wanaodai kuporwa ardhi yao na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) katika vijiji vya kata za Moshono na Mlangarini, wameandamana hadi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, kwa lengo la kuishinikiza Serikali kutatua mgogoro wa ardhi.
Maaandamano hayo makubwa ambayo hayajawahi kutokea, yalisababaisha kazi kusimamama katika ofisi za Manispaa ya Arusha na ya Mkuu wa Mkoa huo na barabara kadhaa kufungwa.
Wakazi hao walikuwa wamebeba mabango mbalimbali mengi yakitaka JWTZ Kikosi cha 977 KJ kung'oa mbao za matangazo waliyoweka ambayo yanawazuia kufanya jambo lolote katika ardhi yao.
Maandamano hayo pia yalisababisha shule kadhaa kukosa wanafunzi kufuatia wengi kujiunga na wakazi hao.
Viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Raymond Mushi na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, jana asubuhi walifika katika vijiji hivyo kuwashawishi wasitishe maandamano lakini walikurupushwa na wakazi hao na kuwaambia hawana jipya.
Katika hali ambayo haijazoeleka, polisi waliwaongoza waandamanaji hadi kwenye ofisi ya mkuu huyo wa mkoa.
Mmoja wa wanakamati waliokuwa wakifuatilia suala hilo kwa muda mrefu, Emmanuel Masamaki, aliwaambia viongozi hao kuwa wakazi hao wanamtaka Mkuu wa Mkoa tu na si vinginevyo.
“Tumeamua kuandamana leo (jana) na watoto wetu tukafie kwa mkuu wa mkoa kwani tumenyimwa kulima, kujenga na kuchunga katika ardhi yetu,” alisema " Masamaki.
Baada ya kufika kwa Mkuu wa Mkoa, wakazi hao walitoa madai yao wakitaka askari kung'oa vibao vya matangazo ya kuwanyima kufanya lolote katika ardhi yao.
Loningo Kipuyo, alisema mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa jamii yao inakabiliwa na tishio la njaa kufuatia kunyimwa kulima kwa miaka mitatu na kupewa vitisho vya askari wa jeshi hilo.
“Tutakula nini mkuu, watu wetu wanategemea kilimo leo tumenyimwa kulima tutakula nini sisi, tunaishi kama wakimbizi katika nchi yetu, ”alisema Kipuyo.
Mulongo aliwaahidi mwafaka utajulikana Machi 20, mwaka huu baada ya kukutanisha pande hizo zinazovutana.
“Jambo hili tunaendelea kulitafutia ufumbuzi ndugu wananchi naomba mvute subira wiki ijayo tutafikia mwisho wa malumbano haya naomba mniamini mimi na serikali yenu kuwa tuna nia ya dhati ya kumaliza tatizo hili, ”alisema Mulongo.
Kutokana na mgogoro huo, wakazi wa vijiji hivyo wanalazimika kuzika wafu wao katika vijiji vya jirani kutokana na zuio la jeshi jeshi hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake