Monday, March 5, 2012

Polisi watajwa kashfa ya mauaji

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro,
Absalom Mwakyoma
Jeshi la Polisi Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro,limekumbwa na kashfa nzito ya mauaji ya mfanyabiashara, Janes Shayo (44 ), mkazi wa Tarakea wilayani humo, ambaye alifariki dunia muda mfupi baada ya kuachiwa na polisi waliokuwa wanamshikilia.

Wakati familia ya marehemu ikidai ndugu yao amekufa katika mazingira ya kutatanisha na kulitaka jeshi hilo kutoa ukweli wa jambo hilo, Jeshi la Polisi mkoani humo, limedai kuwa kijana huyo amefariki dunia baada ya kunywa sumu kutokana na mazao yake kuuzwa na askari waliokuwa wamemkamata.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma, alisema jeshi hilo linawashikilia  Polisi wawili kwa kosa la kuuza mazao ya mfanyabiashara huyo, kinyume cha sheria na kwamba tayari wameshapelekwa kwenye Mahakama ya Kijeshi ambako kesi inaendelea.


Familia ya marehemu huyo, Tarisisi Shayo ya Tarakea wilayani Rombo, tayari imemwandikia barua ya malalamiko, Kamanda Mwakyoma ya jinsi polisi walivyohusika katika kifo cha kitatanishi cha kijana wao.
Katika barua yao kwenda kwa Kamanda Mwakyoma, ambayo NIPASHE inayo nakala yake, familia hiyo imeeleza mkasa mzima kuwa  mtoto wao (Janes) alikuwa akifanya biashara ya mazao kwa muda mrefu akishirikiana na mfanyabiashara mwenzake, Primu Shayo, ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Tarakea.
“Wakati fulani, biashara yao haikwenda vizuri na kukatokea hasara, familia tulishirikishwa na makubaliano yalifikiwa kwamba kijana wangu
atamlipa mwenzake huyo hasara iliyotokea na kwa kuaminiana zaidi, Mkuu wa Kituo cha Tarakea,  Makundi, alishirikishwa na fedha zililipwa mbele yake,” alisema.
Alisema Januari, mwaka huu, alilipa Shilingi milioni mbili na yeye (mzee Shayo), ndiye aliyezikabidhi  na makubaliano ya awamu ya pili ilikuwa apeleke fedha nyingine Februari 20, mwaka huu.
Hata hivyo, alisema kabla ya tarehe hiyo, alikwenda kwa Mkuu huyo wa Kituo na kumkabidhi Sh. 400,000 na kuomba muda zaidi, ambapo alikubali na kumpa siku tano hadi hapo mzigo wake wa mazao utakapoingia siku ya Ijumaa yaani Februari 25.
Shayo aliongeza kuwa cha kushangaza Mkuu huyo wa kituo alituma askari watatu wakiwa na silaha kwenda kukamata mzigo huo, ambao ni magunia 50 ya maharage yenye thamani ya zaidi ya Sh. 4,592,200 na kuyauza.
“Maharage hayo yaliuzwa bila mwenyewe kuwepo, polisi walishirikiana na Mtendaji wa Kijiji cha Kikelelwa na kisha kufanya makabidhiano ya fedha hizo kwa aliyekuwa anamdai marehemu, zoezi ambalo lilifanyika mbele ya Mtendaji huyo," alisema.
“Tunapata shaka juu ya askari hawa kuwa na nguvu ya kuuza mazao ya mwanangu wakishirikiana na mdai, kisha kumlipa aliyekuwa anadai na mwanangu kushikiliwa mahali pasipojulikana tangu saa nne asubuhi hadi saa 11 jioni, alipofika nyumbani kwake akiwa na hali mbaya na wakati akianza kumuelezea mke wake mkasa mzima, alianguka chini na kukata kauli kisha akaaga dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini,” alisema.
Alisema mke wake alisikia akieleza kuwa Primu (mdai), akishirikiana na Polisi, wamekamata mzigo wake, ambao sio wa magendo na kuuza, ambapo baada ya kumaliza kusema hivyo, alidondoka chini na mke wake alipiga yowe na majirani walifika kumsaidia, lakini alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa hospitali.
“Naomba kupata maelezo juu ya kifo cha mwanangu, pili ni lini Jeshi la Polisi limekuwa Mahakama ya kusimamia mali ya mtu kuuzwa bila idhini yake na mwenyewe kutokuwepo?," Alihoji Mzee Shayo.
Aidha, alisema hadi sasa hawajazika mwili huo wanasubiri ufanyiwe uchunguzi wa kina na kisha familia kupewa majibu yanayoridhisha.
Aidha, alisema kila wanapowauliza Polisi wilayani humo hudai kuwa jambo hilo linashughulikiwa na mahakama ya kijeshi.
Alisema hakuna ushirikiano unaotolewa na jeshi hilo kwa ndugu wa marehemu na kwamba familia wanataka kujua mali ya marehemu imepelekwa wapi na imeuzwa kwa idhini ya nani na walimfanya nini (marehemu) hadi akarudi nyumbani kwa muda mfupi kisha akafariki dunia katika mazingira ya kutatanisha, huku aliyeshirikiana na polisi kuuza mazao akiwa nje ambaye ni kiongozi wa serikali.
Akizungumza na NIPASHE, Kamanda Mwakyoma alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kupokea barua hiyo na kwamba kijana huyo alikunywa sumu baada ya polisi kuuza  mzigo wake na si kweli kuwa polisi wamehusika katika kifo chake.
“Huyu mtu alikuwa anadaiana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Tarakea, walikuwa wanafanyabiashara ambapo mdai (Primu) alitoa Sh. milioni 10 na marehemu alilipa kwa awamu ya kwanza Shilingi milioni tano, awamu ya pili Shilingi milioni mbili na kwamba polisi walipewa taarifa kuwa mdaiwa huyo ameonekana mahali akiuza mazao na nipo polisi walipokwenda,” alisema.
Alisema polisi hao wanashikiliwa kwa kosa la kuuza mazao hayo kinyume cha sheria, kwani hawakupaswa kufanya hivyo, na kwamba kijana huyo alikunywa sumu baada ya kuona mzigo wake umeuzwa.
“Hakuna ubishi kuwa alikuwa anadaiwa, lakini tunachowahoji polisi wetu ni kwanini wageuke na kuuza mzigo wa mtu badala ya kumfikisha kwenye kituo cha polisi, hili ni kosa; wameingilia yasiyowahusu," alisema.
Habari kutoka ndani ya familia hiyo, zinaeleza kuwa kijana huyo ambaye ameishi kwa muda mrefu na mkewe bila kujaliwa mtoto, wamefanikiwa kupata mtoto hivi karibuni, ambaye kwa sasa ana umri wa mwezi mmoja.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake