ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 1, 2012

Taifa Stars mapepe-Habari Leo

TAIFA Stars 'mapepe' ndivyo unavyoweza kusema baada ya timu hiyo ya soka ya Tanzania kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Msumbiji katika mechi ya kuwania fainali za Kombe la Mataifa Afrika iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam. 

Matokeo hayo yamewahuzunisha Watanzania wengi waliofika uwanjani kushuhudia mechi hiyo, kwani licha ya Stars kufika langoni mwa wapinzani wao mara kwa mara, lakini washambuliaji wake walishindwa kuzifumania nyavu. 

Baada ya mechi hiyo kwisha mashabiki hao walianza kuimba 'hatumtaki, kocha wenu, hatumtaki, kocha wenu,'. Wageni ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza katika mechi hiyo katika dakika ya 22. 

Bao hilo lilifungwa na Clesio Bauque baada ya kutumia vizuri uzembe uliofanywa na mabeki wa Stars. 

Stars walisawazisha bao hilo kupitia kwa Mwinyi Kazimoto katika dakika ya 41 baada ya kupokea pasi ya Vicent Barnabas kabla ya kuachia shuti kali nje ya 18 lililokwenda moja kwa moja wavuni. 

Kama wachezaji wa Stars wangekuwa makini wangeweza kuibuka na mabao mengi jana, lakini Hussein Javu alishindwa kufunga katika dakika ya 76 baada ya kupokea pasi safi ya Kazimoto lakini shuti lake alilopiga likagonga mwamba. 

Dakika mbili baadae, John Bocco alikosa bao la wazi akiwa peke yake na kipa wa Msumbiji. 

Dakika ya 84 nusura Juma Nyoso aizawadie Msumbiji bao shukrani kwa kipa Juma Kaseja aliyefanya juhudi binafsi kuondoa hatari hiyo.

No comments: