ANGALIA LIVE NEWS
Saturday, April 28, 2012
Mahojiano ya Mwananchi na Rais wa Malawi
NI JOYCE BANDA, MWANAMKE WA KWANZA KUSHIKA MADARAKA HAYO, AAPA KUTOLIPIZA KISASI, KUJIKITA KUWAKOMBOA WANANCHI, AWAWEKA ROHO JUU VIONGOZI WAZEMBE
Mahojiano maalum na Rais mpya wa Malawi, Mheshimiwa Joyce Hilda Mutila Banda, yaliyofanyika katika Jiji la Blantyre, Jumamosi Aprili 21, 2012 na Mhariri wa Mwananchi Jumamosi, Neville Meena. Swali: Ukiwa Rais wa sasa wa Malawi ni nini maono yako kwa wananchi wako? Jibu: Maono yangu kwa Wamalawi ni kuwa na Taifa ambalo watu wake watakuwa wanaishi kwa utulivu na usawa, wawe wanaume au wanawake. Lakini ajenda yangu kuu kuloko zote ni kuondoa umasikini.
Unaweza kuuliza, kuondoa umasikini kwa namna gani? Tunaamini kwamba lazima tujenge uwezo wa kipato kwa watu wetu. Ili kujenga uwezo wa kipato, lazima tutengeneze ajira kwa wanawake na wanaume,vijana na watu wazima haijalishi ajira zikiwa ni watu kuajiriwa au kujiajiri wenyewe. Swali: Unaposema kujenga uwezo wa kipato kutokana na ajira, unamaanisha nini? Jibu: Kama unavyofahamu kuanzia mwaka 2004 hadi 2009, Malawi ilipata maendeleo makubwa ya kukua kwa uchumi wake. Kwa hili lazima tumpongeze aliyekuwa rais wetu (Hayati Bingu wa Mutharika), ambaye alipoanza kuingoza Malawi na aliwaambia wananchi kwamba Malawi siyo nchi masikini bali watu wake ndiyo masikini.
Na kwamba ikiwa tunaweza kubadili mitizamo na mawazo yetu, tunakuwa tumejipa wajibu wa kuleta mabadiliko makubwa katika hali zetu za kimaisha.
Lakini kati ya mwaka 2009 na sasa tulishuhudia Malawi ikirudi nyuma na hivi tunavyozungumza naweza kusema tuko kwenye mgogoro wa kiuchumi. Kuna sababu nyingi tu ambazo zimetufikisha hapa tulipo na baadhi ya sababu hizi tunaweza kuzibaini wenyewe.
Lakini ili kuweza kurejesha uchumi wetu katika njia sahihi, kuna hatua kadhaa za haraka na za muda mfupi ambazo tunaweza kuzichukua.
Kwanza ni kukubali ukweli kwamba asilimia 40 ya bajeti yetu inatoka kwa wafadhili. Kwa maana hiyo ni bajeti inayotegemea ufadhili, kwahiyo lazima tujiulize leo ni mambo yapi yaliyosababisha wafadhili wetu kuondoka? Kwahiyo hili ni jambo la wazi, lazima tuwarejeshe wafadhili wetu, lazima turejee katika mpango wa IMF (Shirika la Fedha la Kimataifa). Haya yakifanyika wafadhili wetu watarejea.
Isitoshe hivi sasa zikiwa ni wiki mbili tangu niingie ofisini (kama Rais) hatua tulizokwishachukua zimewavutia na sasa wanasema kwamba wanasubiri kauli ya IMF kwamba sisi tupo tayari kufanya kazi na wafadhili hao na baada ya hapo wataaanza tena kutoa misaada ambayo walikuwa wameizuia kwa miaka miwili iliyopita. Jambo la pili ni kuhusu nchi ya Uingereza ambayo ni moja ya wafadhili wetu wakubwa.
Nadhani unafahamu kilichotokea kwamba kulikuwa na kutokuelewana baina yao na Serikali yetu iliyopita na aliyekuwa Rais (Mutharika) alimfukuza aliyekuwa balozi wao hapa nchini.
Kutokana na hilo pamoja na mambo mengine yanayohusu Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambayo Serikali ya Uingereza ilikuwa ikiyafuatilia hapa nchini, iliamua kuondoa misaada yake yote.
Kwa hiyo hivi sasa tumekuwa na mazungumzo ya kina na Serikali ya Uingereza na kuna kila dalili kwamba sikuchache zijazo uhusiano wetu utarejea na kuimarika pia.
Hayo ni kwa kuanzia tu na siku si nyingi tutauona uchumi wetu ukikua na kuelekea katika njia sahihi kutokana na mambo hayo machache tuliyoyafanya na tunayoendelea nayo. Swali: Itawachukua muda gani Malawi kama nchi kutoka katika mitego ya uchumi unaotegemea wafadhili?
Jibu: Ninachokueleza ni kile tunachopaswa kufanya kama suluhisho la muda mfupi la matatizo tuliyonayo. Ikiwa asilimia 40 ya bajeti yetu inatoka kwa nchi wahisani, hakuna njia nyingine, kabla ya kuangalia mipango yetu wenyewe, lazima hatua ya kwanza iwe ni kuirejesha hiyo asilimia 40.
Tukishairejesha hiyo asilimia 40 tutaweza kurejea katika nafasi tuliyokuwa nayo awali, na hapo ndipo wananchi wa Malawi wanapotaka kutuona tukiwa sasa. Kwa hiyo tukiwa katika nafasi hiyo, utakuwa ndio wakati muafaka wa kuanza kuangalia jinsi ya kujikwamua kwa kutumia miaradi yetu wenyewe tukianza kutekeleza maono ambayo nimekwambia kwamba ninayo kwa wananchi wa Malawi.
Kuanza kufanya shughuli za kukuza uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo si kwamba tuna kazi ya kuwarejesha wahisani tu, la hasha. Lakini unafanyaje katika mazingira haya huna mafuta, hatuna umeme, hatuna fedha za kigeni; nakdhalika, tunahitaji kuweka mambo haya sawa kwanza na katika kujiweka sawa tunahiitaji hiyo asilimai 40. Hii ndiyo maana tunapozungumza sasa Waziri wetu wa Fedha yuko Washington (Marekani) katika mikutano ya IMF na ni jana tu walikuwa na majadiliano na wahisani.
Kwahiyo nina kila sababu ya kuamini kwamba wahisani wetu wanasubiri taarifa kutoka IMF kamba sisi tupo tayari kufanya nao kazi. Pia nimeeleza utayari wetu kwa wahisani kwamba tunayafanyia kazi mambo mengine kama vile Utawala Bora, Haki za Binadamu na mengine muhimu ambayo wameonyesha kuguswa nayo. Kwa hiyo tunapata hiyo asilimia 40 tunarejea kwenye mipango yetu. Kwa yale ambayo nimekwambia kuwa ni maono yangu kwa Wamalawi, hayawezi kutoka kwa wafadhili, lakini hii asilimia 40 tunaihitaji ili kuurejesha uchumi wetu katika hali yake ya kawaida. Badaye tutaanza kusonga mbele kwa kuzingatia mipango ambayo itakuwa imepitishwa na Serikali yangu. Na kwakuwa kuondoa umasikini ndiyo ajenda yangu kubwa basi lazima turejee kwenye mpango unaowalenga masikini.
Katika chama chetu People’s Party (PP), tumechagua sekta kumi za vipaumbele kwani kama nilivyosema mwanzo lazima tutengeneze ajira.
Kwa mfano moja ya sekta hizo ni kilimo ambayo tunaitizama kama Hayati Mutharika alivyoitumia kutuwezesha kujitosheleza kwa chakula. Na ninapenda kusema kwamba lazima katika hili tumpongeze raisi wetu kwamba alifanikiwa kiasi cha dunia nzima kusimulia jinsi Malawi ilivyoweza kuondoka katika uhaba wa chakula na kuwa na uhakika wa chakula. Hali hiyo ilituwezesha kuwa na uwezo wa kutoa msaada kwa nchi nyingine. Kwahiyo tukiiangalia hiyo hiyo sektka ya kilimo, inaweza kuwa chanzo cha maelfu kwa maelfu ya ajira.
Tutaangalia jinsi ya kukifanya kilimo kuwa cha kibiashara, ni kwa jinsi gani tunaweza tukakihusisha na viwanda, kuongeza thamani ya mazao yetu, masoko na haya yote ni kuwasaidia wakulima wetu wadogo nchini kote. Watu walewale ambao walifanya miujiza ya kuwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula, ndio haohao tutakaowawezesha ili kutengeneza idadi kubwa ya ajira zinazohitajika. Katika sekta zote hizo ndiko tutakakoelekeza nguvu zetu ambazo zitatengeneza ajira kwa watu wetu.
Ninafahamu kwamba sisi huwa tunazalisha sana mazao ambayo huharibika kwa sababu tu hatuna namna ya kuyasindika.
Kwa hiyo kama tuna nyanya kwa mfano na tukawa na vikundi vya kutenegenza kiungo kutokama na mazao haya maana yake ni kwamba tayari tutakuwa tumetengeneza ajira katika sekta hiyo.
Sekta nyingine ni mifugo, ikiwa tutawekeza nguvu katika sehemu hii, pia tutatengeneza maelfu ya ajira. Wamalawi wanafahamu kwamba Joyce Banda hawezi kuzungumza chochote ambacho hajawahi kukifanyia majaribio.
Kwahiyo mambo yote ambayo nimekwambia ni kwasababu niliwahi kujaribu. Niliwahi kujaribu kuwasaidia watu kujishughuisha na mifugo na niliona jinsi walivyoweza kubadili mfumo wao wa maisha.
Kwa hiyo ninapozungumzia kutengeneza ajira sisemi kwamba eti ajira ziko pale watu wakaajiriwe, ninamaanisha ajira ambazo watu hao wanaweza kuzitengeneza kutokana na mazingira wanamoishi. Swali: Wewe ni Rais wa nne wa Malawi lakini una sifa ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke, kuwa rais mwanamke kuna maana gani kwa taifa kama Malawi? Jibu: Naweza kusema kwamba nimekuwa na hii fursa ya kuwa wa kwanza, kwanza kwanza! Kwasababu nilikuwa mwanamke wa kwanza kuwa mwenyekiti wa Shirila la Umma, nikawa mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais na sasa ni mwanamke wa kwaza kuwa Rais wa Malawi. Wajibu wangu kwanza ni kuleta mtizamo wa jinsia yangu katika suala la uongozi, mtizamo na hisia za mwanamke katika uongozi, jinsi tunavyoyatizama mambo na hasa mambo yanayozigusa jamii, mambo ambayo viongozi kama mimi wanaume wasingeyapa umuhimu.
Nimekuwa nikifanya hivyo katika maisha yangu yote na ninaamini kwamba nikiweka mawazo yangu katika mwelekeo huo na kuzipa umihimu hisia za aina hii, ni imani yangu kwamba kile kilicho ndani, kilicho ndani ya mwanamke kitaonekana kikibadili maisha na hali za wananchi wa Malawi. Niliwahi kufanya hivi kabla kwahiyo ninafahamu kile ninachokizungumza. Nimeona katika nchi nyingi na pia kwenye Bunge la Malawi, mbunge mwanamke huwa anapenda kuyapa umuhimu masuala yanayoigusa jamii kuliko afanyavyo mbunge mwanaume. Na kwa uzoefu wangu wanawake wanapopata fursa ya kuwa viongozi katika ngazi yoyote hufukiria kwanza kuhusu masuala ya kijamii yanayowagusa watu wao.
Ninamwomba Mungu kubaki na msimamo huu. Katika uwezo wangu binafsi niliweza kuanzisha Taasisi ya Joyce Banda (Joyce Banda Foundation) ambayo imekuwa ikijihusiha na upatikanaji wa chakula, utoaji wa elimu, upatikanaji wa maji safi na uwezeshaji wa wanawake na vijana. Wanaonufaika na shughuli hizi ni watu wasiopungua 950,000.
Kama nimeweza kufanya hivyo kwa jitihada zangu binafsi, basi nataka ufahamu kwamba niko tayari kisaikolojia na kiakili kufanya mambo haya katika mtizamo mpana zaidi. Naitizama Malawi na kuwa na imani kwamba Wamalawi wanasonga kwani tulishaanza kusonga kwa kubadili fikrsa zetu kama nilivyosema mwanzo kwamba kila mmoja wetu atambue kwamba kuna rasilimali za kuweza kubadilisha maisha yetu sasa na siku zijazo.
Kwa maana hiyo tunaweza kubadili Malawi ikawa katika kiwango cha maendeleo tunachotaka iwe. Swali: Utawala uliopita ulishuhudia Malawi ikilaumiwa kwa kikiuka misingi ya demokrasia na utawala bora.
Mifano hai ni kutokuwapo kwa madiwani kwa miaka kadhaa lakini pia Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) haina makamishna. Una mtizamo gani katika suala hili? Jibu: Naam, kuna mambo ambayo nitayafanyia kazi haraka, kuna mambo mengine lazima nirudi kutafuta ridhaa ya Bunge. Lakini mengine lazima nirudi kwenye Baraza la Mawaziri. Kwa hiyo jambo ambalo nimekwishalifanya kuhusu Tume ya Uchaguzi ni kwamba nimeielekeza ofisi yangu kuviandikia barua vyama vya siasa. Kitu gani kilikuwa kinafanyika siku za nyuma ni kwamba Sheria inasema; Rais atateua tume ya uchaguzi kwa kushaurina au baada ya kushauriana na vyama vya siasa.
Sasa marais walionitangulia jinsi walivyotekeleza sheria hiyo waliviomba vyama vya siasa kuwasilisha mapendekezo ya majina ambayo miongoni mwake Raisi aliteua watu kuunda Tume ya Uchaguzi Malawi. Lakini Raisi aliyepita, (Mutharika) yeye aliamua kuteua tume kisha kuvijulisha vyama vya saisa.
Kwa maana hiyo mimi nimechagua ule utaratibu wa awali na ndiyo maana nimeviomba vyama vya siasa viteue majina ambayo miongoni mwake nitawateua wajumbe wa wa MEC.
Kwahiyo kufikia katikati ya mwezi ujao tayari tutakuwa na tume ya uchaguzi. Kuhusu madiwani sasa hilo linagusa masuala ya kisheria, kwamba ilipelekwa Bungeni ambako sheria ilipitishwa.
Kwamba kutakuwa na uchaguzi wa Serikali za mitaa (madiwani) wabunge na uchaguzi wa Rais. Kwahiyo ikiwa ninahitaji kubadili utaratibu huo basi lazima nirejee tena Bungeni.
Mimi ninatamani kama tungefanya uchaguzi wa Serikali za mitaa hata kesho, kwa sababu nina mtezamo wangu kwamba uchaguzi wa utatu kwa wakati mmoja ni tatizo hasa kuhusu elimu ya uraia inayopaswa kutolewa kwa wananchi wa kada ya chini.
Sasa ninachoweza kufanya ambacho kiko kwenye uwezo wangu ni kuunda Tume ya Uchaguzi ya Malawi haraka. Swali: Ulichukua nafasi ya urais kutoka katika nafasi yako ya awali ya Makamu Raisi kwa mujibu wa Katiba ya Malawi. Ni nini malengo yako katika uchaguzi ujao wa 2014? Jibu: Kwanza niliweke hili sawaswa. Ni kwamba nilichaguliwa kuwa Makamu wa Rais. Nchini Malawi huwa hatuteui Makamu wa Rais. Rais analazimika kukuchagua kuwa mgombea mwenza wake kwenye uchaguzi na kwa maana hiyo nyote wawili lazima muwepo kwenye sarakasi ya kupigiwa kura. Kwahiyo wote nachaguliwa. Kwa hiyo basi nilifanya kazi za Makamu wa Rais mpaka pale nilipofukuzwa kwenye chama (cha DPP). Baada ya kufukuzwa kutoka kwenye chama cha DPP (Democratic Progressive Party) niliunda chama kingine cha PP.
Chama hiki bado hakijafanya mkutano wake mkuu, hakijaamua bado ni nani atakuwa mgombea wetu wa Urais. Msimamo wangu katika hili uko wazi na nilishasema tangu mwanzo kwamba, tutakwenda kwenye mkutano mkuu ambao utafanyika kati ya Juni na Julai, ikiwa watanichagua kuwa Rais wa chama na hivyo kuwa mgombea wa urais, basi niko tayari kubeba changamoto hiyo. Lakini pia ikiwa tutakwenda kwenye mkutano na wakamchagua mtu mwingine, nitakubaliana na matokeo na kumuunga mkono mtu huyo (atakayetauliwa).
Kwetu ndani ya PP hatujali ni nani ambaye anaongoza chama, kwahiyo chama kitaamua ni nani atakayekuwa mgombea wetu wa urais.
Msimamo wangu hivi sasa ni kama nilivyosema kama wakiniteua kuwa mgombea wao wa urais nitakubaliana na changamoto hizo na nitaikubali. Swali: Unaweza kuzungumzia kidogo uzoefu wa kuwa Makamu wa Rais ukiwa chama cha upinzania?
Jibu: Wakati nilipoapishwa kuwa Makamu wa Rais tayari nilikuwa nafahamu majukumu yangu katika nafasi hiyo, kama nilivyokuwa nimefafanuliwa na rais wakati aliponiomba kuwa mgombea mwenza wake. Hata hivyo, tulipoanza kazi mambo yalikuwa tofauti. Japokuwa napenda kuamini kwamba nilijitahidi kwa uwezo wangu. Sasabu kubwa iliyonifanya mimi nifukuzwe uanachama kutoka DPP ilikuwa ni ya kisiasa na urithi wa madaraka. Kundi moja (ndani ya chama) lilidhani kwamba mdogo wake rais (Peter Mutharika) anapaswa kuwa rais wetu ajaye lakini kundi jingine lilidhani kwamba haikuwa haki kwangu, kwamba na mimi (nilikwishaonyesha nia) nilipaswa nipewe fursa ya kwenda na kushindana katika mkutano mkuu kwa usawa.
Kwa sababu hiyo lazima nikiri kwamba kama Serikali tulihama kutoka kwenye ajenda ya maendeleo na kupoteza muda katika vita ya kuwania madaraka kwa miaka miwili.
Kuwa kwangu nje ya chama nilikuchukia kama fursa adhimu. Sijui kama unafahamu hili, kwamba mimi natokea katika familia ya mashirika ya kijamii kwa hiyo ilikuwa ni vigumu kwangu kuona mambo yanakwenda vibaya halafu eti nikae kimya nisiseme kitu.
Kuona haki za binadamu zinakiukwa halafu niache mambo yaende hivyo tu! Hapana. Isitoshe kila mmoja anafahamu kwamba nilikula kiapo wakati nilipoapishwa kuanza kazi ya Makamu wa Rais.
Kiapo hicho ni cha kuitetea na kuilinda Katiba ya nchi. Katiba inasema wananchi wa Malawi kuishi ni haki yao. Wana haki ya kupata elimu, wamepewa haki ya uhuru wa kutoa maoni na ikiwa haya mambo hawayapati, watalazimika kuandamana kudai.
Haya mambo yote niliyoyasema yamo kwenye Katiba. Sasa mimi nilikula kiapo kwamba nitailinda Katiba. Kwahiyo ikiwa mambo yanakwenda vibaya, kinyume cha Katiba na mimi sisemi kitu nakaa kimya, ninakuwa nimeondoa uhalali wa nafasi yangu ya uongozi. Kwahiyo kuwepo kwangu nje ya chama nikiwa Makamu wa Rais na kule kutengwa kwangu, vilinipa fursa ya kuzungumza kwa uhuru kwani nilikuwa na hakika kwamba Katiba inanilinda. Katiba inasema Rais hana uwezo wa kunifukuza kazi. Ninafahamu kwamba kulikuwa na mpango wa kunifukuza, hata kulitumia Bunge kutekeleza mpango huo kwa kunipigia kura ya kutokuwa na imani na mimi, hata hilo pia halikuniogofya.
Nilifahamu kwamba hata wangefikia hatua hiyo Katiba ilikuwa bado inanilinda. Kwamba nilikuwa lazima niwe nimefanya makosa ambayo asili yake ni uvunjaji wa Katiba, lakini kwakuwa mimi nilikuwa nikiitetea Katiba.
Kwahiyo nisema kwamba nilifurahia nafasi yangu ya Makamu wa Rais kwa babau ilinipa nafasi zaidi ya kuwatumikia watu na kuwalinda.
Hili ni dhahiri kwamba unapochaguliwa kwa kura, unakuwa umeajiriwa na wao. Swali: Kuna hofu katika makundi mbalimbali ya watu hasa wanasiasa kwamba huenda ukalipiza kisasi kutokana na mabaya uliyofanyiwa wakati ulipofukuzwa kutoka DPP. Ni nini msimamo wako katika hili?
Jibu: Nadhani wananchi wa Malawi wanafahamu kile Mungu alichonijalia, moyo wa upendo na kusamehe.
Na wengi hapa nchini pia wanafahamu kwamba nilinyanyaswa sana na kusingiziwa lakini naomba nikiri kwamba katika hayo yote sikuwahi kumjibu mtu awaye yote. Hata hivyo siwalaumu wale wenye mawazo kwamba labda nina mpango wa kulipiza kisasi. Lakini kwa mtizamo wangu nilionao sasa utakuwa ni upotezaji wa muda wa hali ya juu katika mchakato wa maendeleo ya nchi yetu na wala (ulipizaji kisasi) hauwezi kuwa na manufaa yoyote kwa Wamalawi. Nimekula kiapo cha kuwalinda na kuwaendeleza wananchi wa Malawi, halafu eti nipoteze muda eti nalipiza kisasi? Nadhani hilo halitakuwa na manufaa yoyote kwa nchi.
Historia itakuwa inajirudia kwani kwa miaka yote miwili iliyopita tulipoteza muda katika vita ya madaraka na sasa tena tuongeze miaka mingine miwili kujaribu kulipiza visasi, sitapenda kufanya hivyo. Lakini hili halina uhusiano kabisa na utekelezaji wa majukumu mengine niliyonayo kama Rais wa Malawi.
Hapa namaanisha kwamba kama kuna mtu anafanya kazi asiyo na uwezo nayo, anajihusisha na rushwa, huyo siwezi kumvumilia eti tu kwasababu tu nikimchukulia hatua watu watafikiri kwamba ninalipiza kisasi. Nimetumia wiki zangu mbili kujifunza ndio maana sikuwa na haraka katika kufanya mabadiliko ya nafasi mengine katika utumishi na uongozi.
Nimepata fursa ya kuwasikiliza Wamalawi wanasema nini na kweli wanasema kwamba sistahili kumvumilia mtu yeyote ambaye amekuwa akitumia ofisi ya umma vibaya.
Kwahiyo ikiwa nafasi ya hiyo iko ndani ya uwezo wa mamlaka yangu kama rais wa nchi hii, sitasita kumchukulia hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu za kazi.
Nilitaka wewe pia ufahamu kwamba Wananchi wa Malawi wameteseka sana na pia nikuthibitishie kwamba kutokana na hilo tumedhamiria kuleta mabadiliko makubwa katika nchi yetu. Swali: Lakini mheshimiwa rais tumeona mabadiliko kadhaa katika Baraza la Mawaziri na baadhi ya nafasi… Jibu: Ndiyo! (anarukia na kujibu kabla swali halijamalizika) Ilikuwa ni sehemu ya masahihisho ambayo yalizingatia matakwa ya wananchi wa Malawi. Mathalani hatua za kumuondoa kazi aliyekuwa Waziri wa Habari (Patricia Kaliati), ilikuwa ni kutekeleza matakwa hayo ya umma, kwani hadi sasa bado sijambadilisha waziri mwingine yoyote.
Kama ni kuliunda upya Baraza la Mawaziri, nilitaka kwamba hebu tumalize mazishi (ya Mutharika) kwanza na hapo ningeweza kukaa chini na kuangalia Baraza la Mawaziri na nafasi nyingine za uongozi.
Lakini kulikuwa na msukumo wa umma kwamba wakati tukisubiri mazishi, tumedhalilishwa vya kutoshwa na kutukanwa vya kutosha kama Wamalawi.
Kwa hiyo nilichukua hatua kuitika wito wa umma. Kwa nafasi nyingine kama ile ya Mkuu wa Polisi (IG) na Katibu Mkuu Hazina, ilikuwa ni katika utaratibu huohuo wa kufanya masahihisho, kwamba tulihitaji kuchukua hatua na kusafisha.
Katibu Mkuu wa Hazina ni mtu ninayemfahamu ijapokuwa sikuwahi kuwa na mazungumzo naye ya muda mrefu. Yeye hajawahi kunifanyia jambo baya, kwahiyo kuondolewa kwake ni kwamba nimetekeleza wajibu wangu.
Ninamaanisha kwamba ninalazimika kulinda kile kilicho miliki ya Wamalawi. Ninafanya uamuzi ambao ninadhani unalinda maslahi ya wananchi wa Malawi. Swali: Una historia ya kuwa mjasiriamali. Bado una mapenzi na eneo hili? Kama jibu ndiyo, unaliwazia nini kundi hili? Jibu: Katika maisha yangu ninaamini katika uwezeshaji wa kiuchumi na hayo ndiyo maono yangu, kuwasaidia wanawake na vijana, kuwawezesha kisiasa na kimaisha kwa kuwapa elimu yenye mwelekeo.
Ninaamini kwamba uwezeshaji wa kiuchumi ni ufunguo wa kujenga uwezo wa kisiasa na kimaisha.
Hapo ndipo tunapoweza kuanzia. Taasisi ya Joyce Banda (The Joyce Banda Foundation) ina wanawake 110,000 wanaojishughulisha na biashara mbalimbali. Hivyo ndivyo watu wanavyoweza kusonga kuelekea kwenye mafanikio. Kuwa na sehemu wanakoweza kukutana na kushirikishana mambo kadha wa kadha na kujenga uwezo wa kufanya uamuzi katika ngazi zao za maisha kupitia mipango ya uwezeshaji wa kijamii. Kwahiyo jibu fupi kwa swali lako ni kwamba, ndiyo na hasa hilo ndilo ninalolilenga. Kutenegeza ajira kwa watu kujiajiri, ninaposema hivyo ninamaanisha uwezeshaji wa kiuchumi kwa wananchi.
Swali: Mheshimiwa Rais Banda, sasa ujumbe wowote kwa wananchi wako….. Jibu: Nadhani kwanza niwashurukuru Wamalawi wote kwa kuniunga mkono wakati nilipotita kwenye mazingira magumu na hata sasa. Lakini pia niwaombe kwamba tunahitaji kuendelea kumwomba Mungu kwa pamoja, tunahitaji kuendelea kuomba. Tunahitaji kuendelea kusimama tukiwa wamoja kama taifa moja. Uogozi wangu hautaongoza kwa misingi ya makabila, nitaongoza Malawi kama nchi ya Wamalawi na ni ushauri wangu kwamba hakuna mtu atakayekuja kutuendeleza. Rais wetu (Marehemu Mutharika) alitwambia kwamba nchi yetu siyo masikini ila Wamalawi ndiyo masikini. Kwangu nilivyoelewa, alichokuwa akijaribu kusema ni kwamba Wamalawi tutahitaji kutumia rasilimali zetu, zituwezeshe kusonga mbele kimaendeleo.
Tunahitaji kuutumia utajiri uliopo nchini kwetu. Kwa maana hiyo ujumbe wangu kwa wananchi wangu ni kwamba tunapaswa kuyapa umuhimu maneno hayo ya busara.
Kwahiyo tuamke twende na kutumia rasilimali na fursa zilizopo kwani hakuna mtu yoyote atakayekuja kutufanyia, lazima tufanye sisi wenyewe. Ninaamini kwa dhati kabisa tutasonga mbele tukiwa na dhamira ya dhati na kwa uwezo wa Mungu tutaweza. Mwanachi: Asante sana mheshimiwa rais kwa muda wako, pole kwa kifo cha Rais wenu na sisi tunakutakia kila la heri katika uongozi wako ukiwa Rais wa Malawi. Mwisho…
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
big up mama banda,we need leaders like you in TANZANIA,tumechoshwa na viongoz wetu uchwara,safi sana mizembe mipenda rushwa adhabu yao ni kuwa fired tu,na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Post a Comment