ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 30, 2012

Ni nafasi ya Magufuli, Membe, Tibaijuka


  Wataokolewa kwa utendaji wao
  Wapo wanasubiri miujiza tu
Rais Jakaya Kikwete
Wiki hii itakuwa ya kipekee, itakayotawaliwa na kila aina ya shauku na ubashiri juu ya maamuzi yatakayochukuliwa na Rais Jakaya Kikwete katika kulisuka upya baraza lake la mawaziri.

Hatua hiyo inakuja baada ya  Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Mapunduzi (CCM) Jumamosi iliyopita kuridhia mabadiliko hayo, ikiwa ni utekeleza wa shinikizo la wabunge la kutaka mawaziri wanane waachie ngazi kutokana na ama kushindwa kuwajibika katika wizara zao kiasi cha kucha matumizi ya ovyo kutokea, au wenyewe kutuhumiwa kwa wizi wa mali ya umma.



Kutokana na shinikizo la wabunge wakati wakijadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, kwa mwaka 2009/2010 na ripoti ya kamati za kudumu za Bunge za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali Kuu (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), wabunge wa CCM waliokuwa wamekaa kama kamati ya chama, walipitisha maazimio ya kuwataka mawaziri husika kuachia nafasi zao kwa kuwa  walikuwa wameshindwa kuisaidia serikali kutekeleza majukumu yake, badala yake kugeuka kuwa mzigo kwa wananchi hivyo kuifanya serikali kushindwa kutimiza wajibu wake kwa wananchi.

Kwa kuwa Rais Kikwete wakati wa kikao cha CC Jumamosi aliahidi kufanya mabadiliko hayo haraka iwezekanavyo, bila shaka wiki hii atatengua kitendawili hicho kwa kutangaza Baraza jipya la Mawaziri.

Kwa kuwa mfumo wa Tanzania inatumia mfumo wa Uingereza wa Westminster katika kuunda serikali kwa maana ya kuteua mawaziri kutoka bungeni, kuna uwezekano wa kuwateua kuwa wabunge baadhi ya watu ambao siyo ili waweze kuteuliwa kwa mawaziri kwa imani kuwa wana sifa na watamsaidia Rais katika baraza jipya.

Kutokana na kelele ambazo zimepigwa dhidi ya mawaziri wenye kutuhumiwa, na hasa ikizingatiwa kwamba kwa sasa serikali inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuyumba kwa uchumi, kuanguka kwa sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani, kuzidi kupaa kwa mfumuko wa bei na wananchi kushindwa kuona unafuu wa maisha, kigezo pekee kitakachowapa nafasi mawaziri wa sasa kuibuka katika baraza jipya ni uwajibikaji uliotukuka.

Kwa mtazamo huo na kama ambavyo wananchi wamekuwa wakidai, wakiwamo wabunge na wadau wengine, uteuzi mpya utawaibua wale tu mawaziri ambao tangu wateuliwe mwaka 2010 mwishoni uwajibikaji wa tija na ufanisi ndivyo vipimo vinavyoangaliwa na wananchi kama vigezo pekee vya kuleta mabadiliko katika kipindi cha miaka mkitatu na ushei cha utawala wa awamu ya nne kilichobakia.

Baadhi ya mawaziri ambao utendaji wao umekuwa wa viwango vya juu ni John Magufuli ambaye kwa muda mfupi alioshika Wizara ya Ujenzi miradi mingi ya ujenzi wa barabara imekwenda kwa kasi licha ya serikali kukumbwa na ukata ambao umesababisha wakandarasi kutolipwa kwa wakati na hivyo baadhi ya miradi kukwama.

Magufuli kila wizara aliyopewa ameonyesha uhalali kuanzia mwaka 2005 alipopelekwa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kisha Mifugo na Uvuvi, na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka juzi, akaibukia Ujenzi, wizara ambayo chini ya awamu ya tatu aliitumikia kama Naibu Waziri na baadaye Waziri kamili.

Upepo pia si mbaya kwa Bernard Membe, kwani Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa haijakumbwa na matatizo ambayo yanaweza kusababisha atupwe kando.

Kadhalika, amejitahidi kutumiza wajibu wake kama Waziri wa Mambo ya Nje, kwa kuiwakilisha Tanzania na kuhamasisha sera mpya ya mambo ya nje ya diplomasia ya uchumi vizuri.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, katika kipindi cha uongozi wa waziri wake Ameshughulikia migogoro mingi ya ardhi, kasi ya kupima ardhi na utekelezaji wa miradi mingine ya makazi.

Waziri huyu amethubutu kukabiliana na wavamizi wa maeneo ya wazi kwa kubomoa majengo au uzio uliozungushiwa maeneo ya wazi, kiasi cha kuwatikisa wenye nguvu ya fedha wanaotumia uwezo wao kukiuka sheria za ardhi. Huyu naye kuna kila uwezekano wa kubakia katika baraza jipya.

Waziri wa Sheria na Katiba, Selina Kombani, ameonekana kupwaya katika nafasi hiyo hususan katika kushughulikia suala la mchakato wa katiba mpya.

Waziri huyo alilalamikiwa kwa kukwamisha zoezi la serikali kutafuta maoni ya kabla ya Muswada wa Mabadiliko ya Katiba kuwasilishwa Bungeni Novemba mwaka jana.

Kombani pia alilalamikiwa kutokana na kutoa kauli zilizokuwa zikiashiria kuwa serikali haikuwa na mpango wa kuanzisha mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya.

Kombani kutokana na kutokuwa na taaluma ya sheria kunaweza kumwondoa katika baraza au Rais Kikwete anaweza kumhamishia wizara nyingine, hasa kutokana na kazi nzito ya kuelekea kuandikwa Katiba mpya ufikapo mwaka 2014.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi, ana nafasi ya kubaki kutokana alivyoisimamia vizuri wizara yake ikiwemo kujenga mahusiana ya karibu na wadau, vikiwemo vyombo vya habari na tasnia ya michezo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, bado wizara yake inakabiliwa na matatizo makubwa.

Moja ni migogoro ya kila uchao kati ya Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu na wanafunzi. Pili, kuongezeka kwa kiwango cha kufeli kwa wanafunzi katika mitihani.

Changamoto hizo na nyingine na hadhi ya elimu ya Tanzania kwa sasa zinamweka waziri huyu katika nafasi ngumu kurejea kama kweli kuna nia ya kuitazama elimu ya Tanzania kwa jicho pana na makini zaidi kuiondoa hapo ilipokwama.

Dk. Hussein Mwinyi nafasi yake ya kubaki ni kubwa pengine kutokana na wizara  yake ya Ulinzi na Jeshi la Ujenga Taifa maanuzi yake kutokutegemea sana wanasiasa kwa kuwa hufanywa na wakuu wa vyombo vya usalama wenyewe.

Waziri wa Maji, Profesa Mwandosya, ambaye amekuwa mgonjwa kwa takribani mwaka sasa kwani hata wakati wa mkutano wa Bunge wa  Bajeti mwaka jana hakuweza kuhudhuriwa kuwasilisha makadirio ya matumizi ya wizara yake.

Alilazwa India mwaka jana na kurejea nchini, kisha akarejea tena huko kwa matibabu. Hata mkutano wa saba wa Bunge ulioahirishwa wiki iliyopita hakuhudhuria, amekosa mikutano minne sasa, Juni-Agosti; Novemba; Februari; na Aprili.

Hata kama hatawekwa pembeni kwa  sababu za kibinadamu kwa sababu angali akihudumiwa na serikali, kwa hakika kazi zake zitakuwa zinafanywa na naibu wake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia, anaweza kuondolewa au kuhamishwa kutokana na matatizo makubwa ya kuendelea kuwepo na watumishi hewa wanaolipwa fedha nyingi za walipakodi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, anaweza kubaki kwa sababu wizara yake haijakumbwa na matatizo ya kuathiri utendaji wake.

Amekuwa mstari wa mbele kukemea rushwa ndani ya wizara hiyo, ikiwemo kupambana na maofisa wa uhamiaji wanaoendekeza rushwa.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ana nafasi ya kubaki kutokana na uzoefu wake kama waziri mwandamizi na na pia utendaji wake umekuwa wa tija.

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolokia, Profesa Makame Mbarawa, anaweza kubaki kwa kuwa wizara yake haijakabiliwa na kashfa yoyote kubwa.

Mawaziri wengine wenye nafasi za kubaki ni David Mathayo David (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi); Sophia Simba (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Gaudensia Kabaka (Kazi na Ajira), hata hivyo pamoja na kutokuingia kwenye kashfa yoyote iliyowazi kwa sasa, itakuwa ni vigumu kuteuwa mawaziri wapya wengi zaidi kutokana na sababu za muendelezo wa mipango ambayo tayari imekwisha kuanza ndani ya wizara mbalimbali.

Wengine ambao wanaweza kubaki ni pamoja na William Lukuvi (Ofisi ya Waziri Mkuu –Uratibu na Bunge) na Mary Nagu (PMO- Uwezeshaji).

Katika mjadala uliowaka moto bungeni hivi karibuni, ripoti hizo zilibaini matumizi mabaya ya fedha za umma huku baadhi ya mawaziri wakibainika kushindwa kusimamia wizara, idara na taasisi zilizo katika wizara hizo.

Wakati wa mjadala huo, wabunge wote bila kujali tofauti za itikadi walichachamaa na kutaka mawaziri ambao wizara zao zimehusika katika ufisadi huo wajiuzulu kama njia ya kuwajibika.

 Kabla ya wabunge wa CCM kufikia maamuzi ya kuwataka wenzao wanaoongoza wizara kujiuzulu, walifanya vikao viwili kama kamati ya wabunge wa CCM, hali iliyopokelewa kwa shangwe na makundi mbalimbali ya kujamii, ingawa baadaye ziliibuka taarifa kuwa ndani ya serikali kulikuwa na kutokuelewana juu ya sharti la kuwataka mawaziri hao wajiuzulu.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM, aliahidi kuwa Jumatatu iliyopita angezungumzia suala hilo, lakini hakufanya hivyo siku hiyo jioni wakati akiahirisha mkutano wa saba wa Bunge la 10 zaidi ya kusema kuwa mapendekezo na maoni yaliyotolewa na wabunge serikali itayafanyia kazi.

Katika kuhakikisha kuwa mawaziri hao wanang’olewa, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa POAC, aliomba saini za wabunge ili iwasilishwe hoja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Pinda, zoezi ambalo lilipata mwitikio wa juu kwani  walijiandikisha wabunge kutoka vyama vyote vilivyoko bungeni kasoro UDP pekee, na orodha ilifikia wabunge 75 ikiwa ni juu ya sharti la kikatiba la kupata walau asilimia 20 ya wabunge ambao ni sawa na wabunge 70.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema kuwa hoja hiyo ni batili kwa kuwa kanuni zinataka hoja hiyo iwasilishwe siku 14 kabla.

Miongoni mwa mawaziri waliotajwa katika ripoti hizo ni pamoja na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, ambaye anadaiwa kuhusika katika ubadhirifu wa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC).

Alitajwa kuwa amepotea uaminifu na uadilifu kiasi cha kusema uongo bungeni ili kuficha maslahi binafsi katika ofisi za umma.

Pia Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, alitajwa kuhusika katika kumkingia kifua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Charles Ekelege, kutokana na kusema uongo katika kazi ya ukaguzi wa magari nje ya nchi. 

Ekelege anadaiwa kusema uongo kuwa kuna kampuni zimepewa kazi ya kukagua magari yanayokuja nchini nje ya nchi, ambayo yanalipwa mamilioni ya fedha, lakini kamati ya wabunge iliyokwenda nchi za Singapore na Hong Kong, hawakukuta kampuni hizo.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, naye anadaiwa kushindwa kusimamia matumizi bora ya fedha za umma kiasi cha kuruhusu nyumba yake kukarabatiwa kwa mamilioni ya fedha.

Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika, ambaye anadaiwa kushindwa kusimamia fedha katika halmashauri mbalimbali nchini ambako ufisadi wa kuwango kikubwa umegundulika.

Yupo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, anayetuhumiwa kwa kushindwa kusimamia sekta ya madini na umeme na kuweko kwa manunuzi makubwa ya mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL ambayo yameongezwa bei.

Pia yumo Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, ambaye atauhumiwa kushindwa kudhibiti ubadhirifu katika wizara yake kama ulivyobainika katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii na usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi.

Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, anatuhumiwa kuingilia mchakato wa kumpata mzabuni wa kujenga gati namba 12 na 13 katika Bandari ya Dar es Salaam; Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, anadaiwa kushindwa kudhibiti ununuzi wa pembejeo na ulipaji wa fedha za mdororo wa uchumi.

CHANZO: NIPASHE

No comments: