ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 15, 2012

Majeshi yacharuka kashfa ya vyeti

Patricia Kimelemeta
SIKU moja baada ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), kueleza kwamba askari zaidi ya 948 wamegundulika kutumia vyeti vyenye majina yanayofanana na waajiriwa wengine serikalini Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Polisi wamesema wanajipanga kuifanyia kazi taarifa hiyo kwa gharama zozote
.

Juzi, Nida ilitoa taarifa ikionyesha udanganyifu wa vyeti vya elimu JWTZ na polisi na kuonya ni moja ya changamoto zinazoukabili mchakato mzima wa utoaji wa vitambulisho hivyo.

Jana kwa nyakati tofauti, JWTZ na Polisi walitoa tamko na kusema watachunguza kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) na Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Nida na watakaobanika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

JWTZ
JWTZ liliitisha mkutano na waandishi wa habari jana kuzungumzia tuhuma hizo za baadhi ya askari wake kughushi vyeti.
Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema uamuzi huo umekuja baada ya Nida kutoa taarifa ya kuwepo kwa wanajeshi 248 walioghushi vyeti hiyo na kujiunga na jeshi.

Alisema kitendo hicho ni kinyume na sheria na kwamba mwanajeshi atakayebainika amefanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kushtakiwa kwenye mahakama za kijeshi na uchunguzi ukikamilika na ikatokea amethibitika kughushi, atafukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani.

“Tumepata taarifa kutoka kwenye vyombo vya habari, tukafanya vikao ili kujadili hatua zitakazochukuliwa dhidi ya wanajeshi walioghushi vyeti na kujiunga na sisi ili tuweze kuwafikisha kwenye mahakama za kijeshi na ikiwa watabainika tutawafukuza pamoja na kuwafikisha mahakamani,” alisema mgawe.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi Aya ya 8.26(1)(c) kinasema: “Mwanajeshi yeyote anayegundulika kuwa alidanganya katika taarifa anazotoa wakati wa kujiunga na jeshi, atashtakiwa katika mahakama ya kijeshi na kwamba akipatikana na hatia, anapewa adhabu kali zinazoambatana na kufukuzwa.”

Alisema kutokana na hali hiyo, JWTZ itashirikiana na wadau hao ili kuhakikisha kuwa wanajeshi waliofanya vitendo hivyo wanabainika.
Kanali Mgawe alisema mara nyingi kumekuwa na taarifa kama hizo na kwamba waliwafukuza baadhi ya waliobainika lakini sasa hivi ni mapema kuthibitisha madai hayo ya Nida bila ya kufanya uchunguzi wa kina.

Alisema JWTZ imeanza mchakato wa kufuatilia ajira kwa wanajeshi wake, hatua ambayo itasaidia kubaini tuhuma hizo hatua itakayosaidia jeshi katika kutekeleza uamuzi wake.

“Jeshi ni kubwa na taarifa hizi tumezipata kwenye vyombo vya habari. Nida hawajatuletea taarifa za kiofisi ila tumesema tutashirikiana nao ili tuweze kuwabaini kwa sababu watakuwa wamelidanganya jeshi letu wakati wanajua ni kosa kisheria,” alisema na kuongeza:

“Tutazunguka kila kona ili kuhakikisha kuwa uchunguzi huo unafainikiwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa watakaobainika.”

Polisi
Kwa upande wake, polisi wametoa taarifa kwa umma na kusema baada ya kusikia taarifa hiyo ya Nida, imeunda timu maalumu itakayofuatilia suala hilo kwa karibu zaidi na kuchukua hatua zinazostahili.

Taarifa iliyotolewa jana na jeshi hilo na kusainiwa na msemaji wake, Advera Senso imesema baada ya kuipokea taarifa hiyo, limeunda timu maalumu kutoka makao makuu ya polisi itakayowahusisha maofisa mbalimbali.

Alisema maofisa hao ni kutoka Kamisheni ya Utawala, Operesheni na Upelelezi ambao watafanya uchunguzi yakinifu kuhusu taarifa hiyo na kwamba kwa kuwa suala hilo linalihusisha jeshi, miiko na taratibu za kijeshi zitafuatwa katika kulipatia ufumbuzi.


Mwananchi

No comments: