ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 16, 2012

Pinda: Benki zitoe riba nafuu kwa wakulima


Waziri Mkuu,Mizengo Pinda
Boniface Meena
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amezitaka benki nchini kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima  ili waweze kuendelea kilimo.

Pinda alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Chama cha Kilimo Vijijini Afrika (Afraca).

Katika hotuba hiyo Pinda alisema kwamba, ni muhimu benki hizo zikafika vijijini ili wakulima hao waweze kupata fedha za kuendeleza kilimo chao.

"Wakulima wadogowadogo wanashindwa kupata mikopo ya kutosha kwa sababu benki za biashara zinawatoza riba kubwa na kuhitaji dhamana,"alisema Pinda.

Alisema kutokana na hali hiyo, wakulima hao wamekuwa wakishindwa kupata mikopo kwa kuwa wanaonekana hawawezi kulipa.

"Kutokana na hali hii, taasisi za fedha zijenge uhusiano wa karibu na vyama vya kuweka na kukopa ili kupunguza kukoseka kwa mikopo hasa maeneo ambayo benki hazijafika,"alisema.

Alisema ni matumaini yake kuwa mkutano huo utaangalia jinsi ya kutatua changamoto hiyo ya upatikanaji wa fedha ili sekta ya kilimo iweze kukua.

No comments: