Daniel Mjema
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Balozi Khamisi Kagasheki ameendeleza wimbi la kuisafisha wizara hiyo iiliyogubikwa na kashfa mbalimbali na safari hii akiwasimamisha kazi vigogo wawili wa wizara hiyo. Maofisa hao ni wale waliotajwa Bungeni Aprili mwaka huu na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira wakihusishwa na kashfa ya usafirishaji wanyama hai kwenda nje ya nchi. Kusimamishwa kazi kwa vigogo hao kumekuja wiki moja baada ya Waziri Kagasheki kuwasimamisha kazi wakurugenzi wanne na askari wanyamapori 28 kwa kashfa ya kuuawa kwa Faru wawili.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na Waziri Kagasheki zilisema vigogo hao walikabidhiwa barua zao mwanzoni mwa wiki wakitakiwa kusimama kazi kusubiri hatua nyingine. “Ni kweli hili jambo lipo lakini nitalitolea tamko rasmi na kama nilivyosema tangu mwanzo, hakuna jambo litakalofanywa kwa kificho na hili nalo tutaliweka wazi kwa umma,” alisema Balozi Kagasheki.
Waliosimamishwa kazi ni Boneventura Tarimo ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi; Idara ya Wanyamapori na Mohamed Madehele, Ofisa Wanyamapori mkuu wa Idara hiyo. Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge James Lembeli alipoulizwa na gazeti hili jana alimpongeza Waziri Kagasheki kwa ujasiri na uzalendo wake wa kusimamia rasilimali za nchi na kusema ni maamuzi mazito aliyoyafanya katika kipindi kifupi.
“Nimesikia juu ya kusimamishwa kazi kwa hao watumishi na kwa kweli mimi na kamati yangu tunampongeza Waziri na tunaunga mkono hatua zote anazozichukua,” alisema Lembeli. Akiwasilisha ripoti ya kamati yake Bungeni mjini Dodoma, Lembeli alipendekeza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa Madehele kwa kutoa kibali cha kukamatwa twiga wawili kinyume cha utaratibu. Kibali hicho kilitolewa Aprili 29, 2011 kwa kampuni ya Jungle International Limited (JIL) ili kukamata twiga hao kwa ajili ya kuwahifadhi kwenye hifadhi ya wanyamapori wanaofugwa (Zoo) bila kuonyesha Zoo hiyo iko ndani au nje ya nchi.
“Kwa kufanya hivyo kamati iliridhika kuwa jambo hilo lilifanywa kwa makusudi kuficha ukweli wa mahali ambapo anyama hao wangetakiwa kupelekwa,” alisema Lembeli katika taarifa hiyo. Lembeli alisema bado kuna utata mkubwa kuhusu mahali walipopelekwa twiga hao kwa kuwa barua ya JIL kwenda wizarani ilisema wanyama hao walikuwa wakipelekwa shamba la wanyama la Savanah Plain International School mkoani Shinyanga lakini kibali cha wizara kilionyesha wanapelekwa nje.
Kibali hicho kilielekeza pia ukamataji wanyama ufanyike katika wilaya tatu ambazo ni Longido, Simanjiro na Monduli jambo ambalo ni kinyume cha kanuni ya 3(4) na 5 za sheria ya wanyamapori. “Idhini ya kukamata wanyama wa taifa wakiwamo twiga inatakiwa kutolewa kwa kibali maalumu na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kinyume kabisa na inavyoonekana katika kibali hiki”alisema. Kibali hicho kilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na kusainiwa na Madehele ambaye ni Ofisa Wanyamapori Mkuu kinyume na kifungu cha 26(1) na 58(1) cha sheria hiyo. Pia kamati hiyo ilibaini kuwa JIL sio kampuni halali kuendesha biashara ya wanyamapori kwani taarifa za Msajili wa Kampuni (Brela) zinaonyesha kampuni hiyo ilibadili jina na shughuli zake 2001.
Tangu 2001, kampuni hiyo imesajiliwa kama kampuni ya udalali kwa jina la Jungle Auctioneers & Brokers Company na kwa msingi huo, Madehele anatuhumiwa kutoa kibali kwa kampuni hewa. Katika uchunguzi wa kamati hiyo, ilibainika pia kuwa mwaka 2009, Tembo wanne jike walisafirishwa kwenda katika Zoo huko Karachi nchini Pakistan, mchakato ambao haukuwa na tija yeyote kwa taifa. Wakati kukiwa hakuna uthibitisho kama tembo hao jike walipokelewa na serikali ya Jiji la Karachi, wizara iliendelea kutoa vibali vya kusafirishwa kwa wanyama hai kwenda katika Jiji hilo.
Katika mwendelezo huo Julai 19,2010 Midala alitoa kibali ruhusu kusafirishwa kwenda Jiji la Karachi nchini Pakistan, Pofu wanne, Tandala wadogo wawili, Tembo wanne na Viboko wawili. Uchunguzi wa kamati hiyo ulibaini kuwa kulikuwa hakuna uthibitisho wowote wa maandishi au vielelezo kuthibitisha kuwa serikali ya Pakistan ilikuwa imeomba kupelekewa wanyama hao.
Kwa mujibu wa Lembeli, makubaliano yaliyoingiwa kati ya mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori na aliyeonekana kuwa ni mwakilishi wa serikali ya Jiji la Karachi, Kamran ulikuwa ni ulaghai mtupu. “kitendo hiki kinatoa mwanya wa fikra kuwa yawezekana Idara ya Wanyamapori ilihusika katika biashara isiyokuwa na maslahi kwa taifa”alisisitiza Lembeli katika taarifa hiyo ya kamati. Kamati hiyo ikapendekeza Serikali iwasimamishe kazi Midala, Madehele na Dk. Erasmus Tarimo aliyekuwa Mkurugenzi wa Wanyamapori ambaye tayari ameshastaafu Utumishi wa Umma.
No comments:
Post a Comment