ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 5, 2012

UVCCM: Uamsho wamo serikalini


  Wasira naye awashukia
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira
Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) imewaonya baadhi ya viongozi waliomo ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar ambao walihusika katika vurugu za hivi karibuni zilizofanywa na Jumuiya ya Uamsho kujitoa katika serikali.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, jana mjini Dodoma, wakati wa kikao cha Baraza Kuu ka jumuiya hiyo.

Shigela aliwataka viongozi wa serikali ambao wanajijua kuwa walijihusisha kwa namna mmoja au nyingine katika machafuko hayo kujiondoa mara moja kabla vijana hao hawajawafuata na kuwataja.


“Dk. Shein (Rais wa Zanzibar) alisema atakula nao sahani moja, sisi tutakula nao kijiko kwa kijiko,” alisema Shigela huku akishangiliwa na wajumbe wa baraza hilo.

Hata hivyo, alipoulizwa na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi zaidi, Shigela, alikataa kuwataja.

Tangu kutokea kwa vurugu hizo zilizoanza Mei 26 hadi Mei 28 mwaka huu na kusababisha athari kubwa kutokana na uchomaji moto wa makanisa, kuvunjwa baa na kuharibiwa kwa mali za watu, zimekuwa zikitolewa kauli zikidai kuwa baadhi ya viongozi wa SUK walihusika kuchochea kutokana na kuwa washirika wa Uamsho.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna majina ya wanasiasa yaliyotajwa moja kwa moja kuhusiana na tukio hilo.

WASIRA NAYE AWASHUKIA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira, amesema kuwa Kikundi cha Jumuiya ya Uamsho kimevunja sheria kwa kujiingiza katika masuala ya siasa kutokana na kuhoji masuala ya Muungano ambayo ni ya kisiasa kitu ambacho ni kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake.

Akizungumza jana katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, alisema kikundi cha Uamsho kilianzishwa kutekeleza majukumu ya kidini, lakini katika hali ya kushangaza kimeanza kujihusisha na mambo ya siasa hali iliyopelekea kuzuka kwa vurugu Visiwani Zanzibar.

Wasira alisema kimsingi, dini ya Kiislamu haina mgogoro na dini nyingine, lakini kitendo cha kikundi cha Uamsho kuzusha vurugu zilizopelekea kuchomwa moto kwa makanisa kadhaa ni uvunjaji wa sheria kwa sababu suala la Muungano halina uhusiano na makanisa.

“Wakatoliki na Waanglikana walikuwepo visiwa vya Zanzibar tangu miaka 100 iliyopita wakati Muungano una miaka 45 tu, lakini tunashangaa wenzetu wa Uamsho wametoka kwenye masuala ya kidini wamejiingiza kwenye mambo ya kisiasa,” alisema Wasira.

Wasira alisema wanaosema kwamba Rais Jakaya Kikwete amezuia masuala ya Muungano yasijadiliwe ni waongo kwani Rais alichokisema ni kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyoiunda haijaundwa kwa  lengo la kutaka kuvunja Muungano.

Alisema tume hiyo iliyoundwa kwa kushirikisha makundi yote yakiwemo ya kidini, kisiasa na jamii imepokelewa na Watanzania kwa furaha kubwa bila malalamiko hivyo kinachotakiwa ni kwa kila mtu kutoa maoni kwa tume ili kuwe na Katiba nzuri yenye ushiriki wa maoni mbalimbali ya wananchi.

Wasira aliwashukia watu wanaodai kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ina wajumbe wengi wa dini fulani na kusema siyo kweli kwani dini haikuwa sehemu ya sifa za kuteuliwa kwenye bali vigezo na sifa vilizingatiwa.

MAWAZIRI WALIOTEMWA

Alisema mawaziri walioachwa kwenye mabadiliko ya baraza jipya la mawaziri haina maana kwamba wote ni wezi kama inavyoelezwa na baadhi ya watu, bali kilichotokea wamewajibika kutokana na makosa pengine yaliyofanywa na wasaidizi wao.

Aliongeza kuwa watu wanapotosha ukweli kwa kueleza kuwa waliongoza mashambulizi yaliyopelekea kuondolewa kwa mawaziri hao ni wabunge kutoka vyama vya upinzani, alisema ni uongo kwani wabunge wa CCM ndiyo waliongoza mapambano hayo.

MAKUNDI NDANI YA CCM

Wasira alisema hakuna chama ambacho hakina makundi, lakini makundi yaliyopo ndani ya Chama cha Mapinduzi ni ya kawaida ambayo yanashughulikiwa kichama, lakini kinachooneka yanakuzwa na baadhi ya vyombo vya habari.

“Matatizo ndani ya chama yapo, lakini siyo ya ajabu maana huwezi kuwa na chama kikubwa kama CCM utegemee kisiwe na na tatizo hata chama cha malaika ni lazima kinaweza kuwa na matatizo, lakini CCM ni chama kikubwa chenye uwezo wa kuhimili mawimbi mengi, “alisema Wasira.

Alisema mpango wa CCM wa kujivua gamba unatafsiriwa vibaya na baadhi ya vyama ambapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekuja na falsafa ya kusema vua gamba vaa gwanda.

Wasira alisema CCM ilikuja na kauli mbiu hiyo kwa lengo la kukabiliana na wanachama wake wanaoutaka uongozi kwa kutumia rushwa wasiendelee na rushwa na kwamba kama Chadema wanataka watu wanaotoa rushwa ndio waondoke CCM wakajiunge kwao ni sawa.
 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

INSHALLAH BIIZ NI LI LLAH TUTAPATA NCHI YETU ,NA KUREJESHA HASHI NA MILA NA HULKA ZETU ZA KIZANZIBARI TUTAIPATA NCHI YETU BI IZNI LI LLAH