Kundi moja la wapiganaji wakiwa silaha kali wamedhibiti barabara ya ndege katika uwanja wa ndege jiji kuu la Tripoli, Libya. Waasi hao wamekuwa wakitaka kuachiliwa kwa kiongozi wao wanaodai alikamatwa Ijumaa wiki jana.
Kundi hilo la al-Awfia brigade liliingia katika uwanja wa ndege hali iliyolazimisha ndege nyingi kubadilisha safari. Haijabainika ikiwa kiongozi wa kundi hilo anazuiliwa na serikali ili kuhojiwa.
Wapiganaji hao wamepinga kuondoka uwanja huo hadi masharti yao yatekelezwe.Mwandishi wa BBC Rana Jawad amesema makumi ya wapiganaji wakiwa na silaha kali wangali kwenye uwanja huo.
Rubaa zaidi zinasema baadhi ya maafisa wamekuwa wakiwasihi wapiganaji hao kuondoka eneo hilo.Magari kadhaa ya kijeshi yamefika katika uwanja huo.
Mmoja wa waakilishi kutoka eneo linalodhibitiwa na wapiganaji hao la Tarhouna magharibi mwa Libya amekuwa akishauriana na waasi hao ili kuondoka uwanja wa ndege.
Duru katika uwanja wa ndege zinasema kampuni tatu za ndege zimefuta safari zake.Safari kadhaa za kimataifa zimerejesha huduma zake nchini Libya baada ya amani kurejea kufuatia mapigano ya kumuondoa madarakani Kanali Muammar Gaddafi.
Serikali ya Libya ilichukua udhibiti wa uwanja wa ndege kutoka kwa wapiganaji ambao wamekuwa wakilinda uwanja wa ndege kwani hakuna kikosi rasmi cha jeshi la polisi.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake