JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro, limekamata shehena ya meno ya tembo
iliyokuwa ikisafirishwa kutoka mji wa Tarakea mpakani na Kenya kwenda
mjini Moshi.
Shehena hiyo ilikuwa ikisafrishwa ndani ya gari aina ya Toyota
Noah lenye namba za usajili T 557 BST linalodaiwa kumilikiwa na askari
polisi wa kituo cha Tarakea, Koplo Phabian.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alikiri jana
kukamatwa kwa shehena hiyo na kwamba watu wawili wanashikiliwa kwa kosa
la kukutwa na nyara za serikali.
Kamanda Boaz alisema gari hilo baada ya kupekuliwa lilikutwa likiwa na
vipande sita vya meno ya tembo, ingawa hakuweza kufafanua zaidi meno
hayo yalikuwa yasafrishwe kwenda nchi gani.
Waliokamatwa kwa mujibu wa Kamanda Boaz ni Sharifa Athuman (35) ambaye
ni Mtanzania anayeishi eneo la Kimana nchini Kenya na Raphael Emmanuel
(25) mkazi wa Magamba mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa kamanda, gari hilo lilikamatwa jana saa 2 asubuhi na
askari polisi waliokuwa kwenye kizuizi cha barabara katika mji mdogo wa
Himo Wilaya ya Moshi Vijijini.
Kukamatwa kwa meno hayo ya tembo kunakuja siku chache baada ya Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki, kukiri kuwapo na mtandao
mkubwa wa majangili wanaojihusisha na biashara ya meno ya tembo na pembe
za ndovu.
Kagasheki alikiri kuwapo kwa mtandao huo wenye nguvu kifedha wakati
akipokea faru watatu weusi kutoka nchini Uingereza, ambao walipelekwa
katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
No comments:
Post a Comment